Habari za Punde

Hotuba ya Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani ILO Ndg.Welling ton Chibebe Kwa Nchi za Tanzania Kenya Rwanda Burundi na Uganda Kuadhimisha Siku ya Mei Mosi 2019. Zanzibar.

MWAKILISHI wa Shirika la Wafanyakazi Duniani ILO Bi. Getrude Sima akitowa Salama za ILO wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani iliofanyika katika Ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein, SUZA Tunguu Wilaya ya Kati Unguja

Mgeni rasmi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi - Dr. Ally Mohamed Shein.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyaazi,  Ndugu Ally Mwalim Rashid
Makamu wa Pili wa Rasi wa Zanzibar,  Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi.
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto,  Mheshimiwa Mama Moudline Syrous Castico.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyakzai (ZANEMA), Ndugu Abdallah Salah Salim Salah.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mheshimiwa Hassan Khatibu Hassan
Waheshimiwa Mawaziri, Wawakilishi, Wabunge na Viongozi wengine wa serikali mliopo
Viongozi wote mliopo meza kuu na meza jirani na meza kuu,
Katibu Mkuu Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar – ndugu Khamis Mohamed
Viongozi wa vyama vya wafanyakazi, ndugu wafanyakazi, Ndugu waalikwa na wananchi mliohudhuria
Ndugu waandishi wa Habari.
Itifaki inazingatiwa.
ASALAAM ALAYKUM,Heri ya sikukuu ya Mei Mosi 2019     
Ni furaha na heshima kubwa kwangu kuwepo hapa nanyi leo ili kusherekea siku hii kubwa ya wafanyakazi ulimwenguni kote yenye kubeba dhima isemayo”Kuimarika kwa Uchumi wa Taifa Kuendane na kuongezeka kwa maslahi ya wafanyakazi“.

Ni siku iliyo na historia kubwa na inayo-ashiria umoja wa wafanyakazi na kuhimiza kuwepo mazingira staha ya kazi.
Umuhimu wa siku hii unajionyesha pia Zaidi wakati Shirika la Kazi Duniani likiadhimisha miaka mia moja mwaka huu.

Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa,
Shirika la Kazi Duniani lilianzishwa miaka mia moja iliyopita wakati wa mageuzi yaliyotokana na vita ya kwanza ya Dunia. Wafanyakazi walidai haki sawa na kuheshimiwa kazini, mishahara ya kutosha, masaa nane ya kazi kwa siku na uhuru wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi. Kwenye Katiba ya Shirika la Kazi Duniani maneno ya mwanzo yanasema – “Amani ya kudumu ulimwenguni inaweza kuwepo tu endapo kuna haki ya Kijamii”

Muundo wa ILO wa Utatu ndio chanzo cha uimara na ushirikiano.  Wafanyakazi, Waajiri na Serikali hufanya kazi kwa pamoja kupitia misingi ya majadiliano ya Pamoja na kufikia muafaka.

Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa,
Shirika la Kazi Duniani linafurahishwa na ushirikishwaji wake kwenye malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuiendeleza nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020 na kuboresha maisha na ustawi wa watu wa Zanzibar. Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar wa miaka mitano umeonyesha wazi jinsi Serikali itakavyofikia lengo hili.

Hili linatukumbusha kuzingatia kuwa wafanyakazi ni nguzo katika maendeleo na ustawi wa jamii. Wapo mstari wa mbele katika mikakati ya maendeleo na ni vizuri kuyatambua majukumu yao hasa katika – kupatiwa maslahi na mazingira mazuri ya kazi. Wakati tukiangalia kuhusu kazi za Shirika la Kazi Duniani kwa miaka 100 iliyopita, ni vema pia kuangalia mustakabali wa kazi zake, hasa ukizingatia mabadiliko yanayoendelea kutokea kwenye ulimwengu wa kazi. Ripoti ya Kamisheni ya ILO kuhusu Mustakabali wa Kazi, iliyozinduliwa tarehe 22 Januari mwaka huu, inapendekeza kuwepo kwa mfumo wa maendeleo unaolenga maendeleo ya watu katika Mustakabali wa kazi sambamba na kuzingatia kazi zenye staha, kuondokana na umasikini kwa kuendeleza maendeleo ya watu, será za kijamii na ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa,
Shirika la Kazi Duniani (ILO) linaendelea kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na vyama vya wafanyakazi na waajiri nchini katika kuendeleza ajenda ya Kazi zenye Staha kupitia yafuatayo:

§  Kuendeleza ajira kwa kukuza ujuzi kwa njia ya mafunzo yanayotolewa kwa kushirikiana na taasisi ya mafunzo na waajiri katika sekta ya utalii.
§  Sera ya hifadhi ya jamii
§  Programu ya pamoja ya mashirika ya umoja wa mataifa kwa Zanzibar
§  Kuimarisha uwezo wa kamati za utatu kushiriki kwenye majadiliano ya utatu

Mheshimiwa Raisi, Shirika la kazi Duniani linatambua na kupongeza juhudi za serikali yako kupitia sera ya Uchumi wa Viwanda kwani italeta fursa nyingi za ajira kwa vijana wa Zanzibar.

Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa,
Kama ILO tutaendelea kuunga mkono juhudi za serikali, vyama vya wafanyakazi na waajiri katika kukuza ajira zenye staha ili kuimarisha maisha ya watu wa Zanzibar na hasa wafanyakazi. 
Asanteni sana kwa kunisikiliza, na nawatakia sikukuu njema!!

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.