Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia Wafanyakazi na Wananchi Zanzibar katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Day katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein, Chuo Kikuu cha Taifa SUZA Tunguu Zanzibar Wilaya ya Kati Unguja.
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba tangu ilipoingia
madarakani mwishoni mwa mwaka 2010 imechukua hatua mbali mbali katika
kuyaimarisha mazingira ya watumishi ya kufanyia kazi na kuyashughulikia maslahi
yao.
Alisema kuwa kuimarika kwa uchumi kumewesha katika awamu
hii kuyafanya maslahi ya wafanyakazi yawe bora kwa mara nne pamoja na
kuubadilisha mshahara wa kima cha chini kwa asilimia mia moja.
Aliyasema hayo wakati akihutubia wafanyakazi katika
maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, yaliofanyika ukumbi wa Dk. Ali
Mohamed Shein, uliopo katika Kam;pasi ya Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Tunguu
Mkoa wa Kusini Unguja.
Hivyo, alisisitiza kuwa kutokana na mafanikio
yaliyopatikana ya kuimarika kwa uchumi,
kuyasimamia mapato vizuri hapana shaka suala la kuyaimarisha maslahi wafanyakazi ataendelea kulipa uzito unaostahiki
suala la kuimarisha maslahi ya wafanyakazi.
Alisema ujumbe wa mwaka huu wa siku ya wafanyakazi unaosema
‘kuimarika kwa uchumi wa taifa, kuendane na kuongezeka kwa maslahi ya
wafanyakazi’ utaendelea kuzingatiwa na kufanyiwa kazi na serikali kadiri hali
ya ukuaji wa uchumi utakavyozidi kuimarika.
Aidha, alisema kuimarika kwa amani na utulivu,
imeifanya Zanzibar kuwa katika karne mpya ambapo changamoto zote
zinazojitokeza hutatuliwa kwa njia ya majadiliano na hatimae
kupatiwa ufumbuzi.
Alisema viongozi wa serikali na taasisi binafsi
wanaamini kwamba njia pekee ya kutatua matatizo ni kukaa pamoja na kujadiliana
kwa busara na sio kutumia mapambano au mivutano isiyo na tija.
Aidha alisema, mfumo huo ndio unaotekelezwa baina ya
Serikali na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi, kutokana na pande zote
mbili kuelewa kwamba watu wote ni wamoja na wanategemeana katika kuleta
maendeleo.
“Leo tuko katika karne nyengine,karne ambayo kwa mnasaba wa
kudumisha amani na utulivu katika sehemu zetu tunazoishi ,inatupasa tuzitatue
changamoto zinazotukabili kwa utaratibu wa kukaaa pamoja na kujadiliana kwa
busara hadi kufikia ufumbuzi,”alisema.
Alisema serikali inazingatia haja ya kuendeleza na
kuimarisha ushirikiano na vyama vya wafanyakazi sambamba na kuchukua hatua
zinazostahiki kwa dhamira ya kuyashughulikia masuala ya wafanyakazi ili
kuongeza kasi ya maendeleo, kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa awamu zote saba za
uongozi,imekuwa ikithamini na kutambua kuwa wafanyakazi ni nguzo kubwa na
msingi wa kukuza uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema.
Katika hatua nyengine alisema,hoja zote zinazowasilishwa
serikalini na shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar zinafanyiwa
kazi na kutekelezwa.
Alisema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa kwa
wafanyakazi mara baada ya kuimarika kwa uchumi ni pamoja na
kuimarisha mazingira mazuri ya watumishi na kuyashughulikia maslahi yao.
Alisema kwa kutambua kwamba mazingira mazuri ya kufanyia
kazi yanasaidia kuleta utulivu na kufanya kazi kwa umakini na hatimae kuleta
ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi, serikali inaendelea na zoezi la
ujenzi wa majengo ya ofisi za kisasa zinazokwenda na wakati.
Katika kuimarisha zaidi mfumo wa utumishi serikalini,
alisema serikali imetunga na kuzifanyia mapitio sera, kanuni na sheria mbali
mbali zinazohusiana na utumishi bora.
Aliwasisitiza viongozi na wafanyakazi kuzisoma sheria ili
waweze kuzielewa na kufanyakazi kwa kuzingatia miongozo ya kisheria
na kuleta ufanisi zaidi katika maeneo yao ya kazi.
“Natumia fursa hii kukusisitizeni viongozi na wafanyakazi
wenzangu kwamba zitafuteni,zisomeni,mzifahamu na muyazingatie maudhui yaliomo
katika nyaraka hizo ili muweze kufanyakazi zenu kwa kuzingatia miongozo ya
sheria,”alisisitiza.
Alihimiza wafanyakazi kuzingatia maadili ya utumishi kwa
lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wanapatiwa huduma bora.
Aliwaasa wafanyakazi kuepuka vitendo vya ubadhilifu,wizi na
uhujumu wa mali ya umma,rushwa,uzembe na unyanyasaji kwa wale wanaostahiki
kuhudumiwa.
Akizungumzia mwenendo wa uchumi wa Zanzibar, alisema yapo
mafanikio katika ukuaji uchumi na huduma za jamii na nyengine zimeimarika.
Alisema katika mwaka 2018 uchumi wa Zanzibar ulikuwa kwa
kasi ya asilimia 7.1, mfumko wa bei uliendelea kushuka kutoka kasi ya asilimia
5.6 mwaka 2017 hadi asilimia 3.9 mwaka 2018.
Kuhusu makusanyo na matumizi, alisema yamezidi kuwa bora
ambapo hali ya utegemezi wa bajeti ipo chini ya asilimia sita kutoka asilimia
43 iliyokuwa mwaka 2010 wakati serikali ya awamu ya saba ilipoingia madarakani.
Waziri wa Kazi,Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto,
Maudline Castico, alizipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein kwa kuyashughulikia maslahi ya wafanyakazi
huku akipongeza mashirikiano makubwa yaliopo kati ya Wizara yake na Shirikisho
la Vyama vya Wafaanyakazi.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
(ZATUC), Khamis Mwinyi Mohamed. alisifu juhudi zinazochukuliwa na serikali
katika kusimamia migogoro na haki za wafanyakazi na kutatua changamoto 21 kati
ya 23 zilizowasilishwa.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment