Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Aongoza Wananchi Katika Mazishi ya Mwanasiasa Mkongwe Zanzibar Marehemu.Ramadhan Abdalla Shaban.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji na kumpa pole Mama Mzazi wa Marehemu Maalim Ramadhan Abdullah Shaaban hapo Nyumbani Kwake Uzini Wilaya ya Kati.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Mwana siasa Mkongwe Nchini Tanzania ambae pia ni Waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Ramadhan Abdulla Shaaban aliyefariki Dunia jana Jijini Dar es salaam amezikwa kijiji kwao Uzini Wilaya ya Kati Mkoa Kusini Unguja.
Maarufu Maalim Rama aliyepelekwa kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan Jijini Dar es salaam alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya Figo katika kipindi kifupi.
Umati mkubwa wa Wananchi, Waumini wa Dini Tofauti, Viongozi wa Kitaifa wa Serikali pamoja na wale waandamizi wa Vyama tofauti vya Kisiasa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi walipata fursa ya kumuaga kwenye makazi yake ya kudumu ndani ya Viunga vya Kijiji chake Uzini.
Marehemu Maalim Ramadhan Abdulla Shaaban alizaliwa kijiji kwao Uzini Mnamo Mwaka 1948 na Miaka ya baadae kupata elimu ya Msingi mnamo Mwaka 1964 hadi mwaka 1967 katika Skuli ya Msingi Ndijani Wilaya ya Kati Mkoa Kusini Unguja.
Aliendelea na masomo yake ya Sekondari katika Skuli ya Lumumba kuanzia Mwaka 1968 hadi Kidato cha Nne {FORM 1V} Mwaka 1976 na baadae kujiunga na Mafunzo ya Ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Nkurumah kilichokuwepo mastakimu yake Mtaa wa Beit El Ras.
Wakati Maalim Ramadhan akiteuliwa kufundisha katika Skuli tofauti hapa Nchini hakusita kuendelea kujifunza zaidi kielimu katika mafunzo na fani tofauti ndani na nje ya Nchi zilizomjengea uimara wa kufanya kazi zake kwa kujiamini.
Akisoma wasifu wa Marehemu mara baada ya mazishi ya Mwanasiasa huyo Mkongwe, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Kusini Unguja Nd. Suleiman Mzee Suleiman  {Charas} alisema Marehemu Maalim Ramadhan Abdulla Shaaban alikuwa muumini safi wa Siasa za Ujamaa na Kujitegemea wakati wa Ujana wake.
Alisema Maalum Rama alikuwa Kada wa Afro Shirazy Party YL na muanzilishi wa Chama cha Mapinduzi {CCM} kilichoasisiwa Mnamo Mwaka 1977 katika Viunga vya Uwanja wa Aman Mjini Zanzibar.
Alieleza kwamba baadae alichaguliwa kuwa Balozi wa Nyuma Kumi Katika Kijiji cha Uzini Mwamo Mwaka 1977 na Mwaka 1980 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na kuwahi kushika nafasi za Uwaziri ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mnamo Mwaka 1980 Marehemu Maalim Rama alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hadi Mwaka 1985 ambapo pia akateuliwa kuwa Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Muungano majukumu yaliyokwenda sambamba na kuteuliwa kuwa Kiongozi ndani ya Jumuiya ya Wafanyakazi wakati huo {JUWATA}.
Katika maisha yake ya Utumishi wa Umma Marehemu maalim Rama aliwahi pia kuwa  Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo, Waziri wa  Katiba na Sheria, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, pamoja na Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji Nishati na Maadini.
Pamoja na mambo mengine Marehemu Maalim Ramadhan Abdullah Shaaban  alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi {CCM} nafasi  aliyoifanyia kazi hadi kufikwa na Mauti.
Mwanasiasa huyo Mkongwe Nchini Marehemu Maalim Ramadhan Abdullah Shaaban ambae atakumbukwa na Jamii kutokana na mchango wake mkubwa wa kizalendo uliyolisaidia Kimaendeleo Taifa hili ameacha Vizuka Wawili, Watoto Sita wa Kiume na Watatu wa Kike.
Allah ajaalie safari ya salama, yenye kheir na baraka ya Marehemu Maalim Ramadhan Abdullah Shaaban. Amin.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.