Habari za Punde

Makamu wa Pli wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Ujenzi wa Barabara,Ujenzi wa Mitaro ya Maji na Maeneo Yaliojaa Maji Kutokana na Mvua za Masika Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi, atembelea Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Barabara ya KibondeMzungu, kujionea maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo linalojengwa na Kampuni ya Mecco, akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.Mhe Ayoub Mohammrd Mahmoud. 






Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi pamoja na Kamati Maalum inayosimamia Rasilmali ya Mchanga kutoa kibali cha upatikanaji wa Mchanga kwa Miradi mikubwa ya Serikali ili kuepusha mkwamo wa utekelezaji wa Miradi hiyo.
Alisema haitopendeza ufikie wakati kuwanyooshea vidole Wahandisi wa Makampuni ya Ujenzi wa Miradi Mikubwa kwa madai ya kuchelewesha kazi waliyopewa wakati baadhi yao tayari wameshatoa indhari ya kukumbwa na changamoto ya upatikanaji wa Mchanga kwa wakati.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kutembelea ujenzi wa miundombinu ya Madaraja, Mitaro ya Maji ya Mvua, kukagua maeneo yaliyoathirika na mafuriko ya Mvua za Masika zinazoendelea pamoja na kuwafariji Wananchi waliopatwa na athari hizo ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema upo Urasimu unaofanywa na baadhi ya wasimamizi wa utoaji wa Vibali vya Rasilmali ya Mchanga jambo ambalo zipo dalili zinazoanza kuonekana za kuchelewa kukamilika kwa baadhi ya Miradi ambayo ni muhimu kwa Taifa na Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kazi kubwa iliyofanywa na Wahandisi wa Makampuni yanayojenga Madaraja ya Kibonde Mzungu na Mwanakwerekwe imeleta faraja kubwa kwa Taifa na Wananchi waliowengi hapa Nchini.
Balozi Seif alisema changamoto ya kujaa kwa maji katika madaraja hayo inaanza kuwa Historia kwa vile licha ya kutokukamilika rasmi kwa Ujenzi wake lakini Wananchi wapitao kwenye Madaraja hayo hivi sasa wanaendelea na harakati zao kama kawaida katika maeneo ambayo ilikuwa mwiko kupita katika kipindi hichi.
Akitoa pole kwa Wananchi waliokumbwa na mafuriko kutokana na Makaazi yao kujaa maji katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Kwamtumwa Jeni, Sebleni na Jong’ombe, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliwanasihi baadhi ya Wananchi kuwa na Utamaduni wa kutupa taka katika sehemu Maalum zilizotengwa.
Alisema Serikali imekuwa ikichukuwa jitihada kubwa za kujenga miundombinu ya Mitaro ya Maji ya Mvua lakini wapo Watu wasiozingatia jitihada hizo jambo ambalo linarejesha nyuma utekelezaji wa mipango ya kuwahudumia katika kuimarisha ustawi wao.
Hata hivyo Balozi Seif aliwataka Wananchi wa maeneo yanayopitishwa ujenzi wa Mitaro mipya ya Maji ya Mvua kuwa na subira katika kipindi hichi cha mpito cha Ujenzi unaoendelea kwa vile ukamilikaji wa miradi hiyo utaleta faraja ya kudumu hapo baadae.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa inajiandaa kufanya Utafiti wa kina kubaini chanzo cha athari iliyosababisha kuzama kwa Kisima cha Maji safi na salama, Mnara pamoja na Tangi lake pembezoni mwa Madrasa Ismailia iliyopo Mwanakwerekwe.
Waziri Aboud alisema kutokana na janga hilo Serikali ililazimika kusimamisha masomo ya Wanafunzi Mia 400 Chuoni hapo ili kunusuru Maisha yao hasa kutokana na mmong’onyoko wa eneo hilo ambapo tayari limeshameza Gari za Kifusi chenye uzito wa Tani 150 hali ikibakia vile vile.
Akitoa ufafanuzi wa Ujenzi wa Mitaro katika Maeneo ya Manispaa ya Mjini Meneja wa Mradi wa Huduma za Jamii Mijini { ZUSP} Nd. Makame Ali alisema tatizo la kutuama kwa Maji ya Mvua katika meneo ya Mji wa Zanzibar linatarajiwa kuondoka baada ya kukamilika kwa Mradi huo.
Nd. Makame alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba jududi kwa sasa zinaendelea kufanywa katika kuunganisha Mtaro Mkuu unaotokea Bwawa la Mwanakwerekwe, kupita Bwawa la kwa Mtumwa Jeni, kuelekea Bwawa la Sebleni litakaounganishwa Mtaro unaojengwa Mikunguni na maji hayo kumalizia Bahari ya Kinazini.
Alisema yapo maeneo yenye kutuama kwa maji ya mvua katika baadhi ya Mitaa ya Wilaya ya Mjini ambayo Wataalamu wa Mradi huo wanayazingatia katika utaratibu wa kuyachukulia hatua za ujenzi wa mitaro midogo itayounganishwa na ile Mitaro mikubwa.
Wakitoa shukrani zao kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Baadhi ya Wananchi wa meeneo mbali mbali ndani ya Mkoa Mjini Magharibi walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali wamekuwa wakizishuhudia kila kukicha.
Wananchi hao walisema Ujenzi wa Mitaro ya Maji ya Mvua ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi umewapa faraja kubwa na kuendelea kujenga matumaini makubwa ya kustawika kwa maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Serikali ya Mkoa huo kupitia Afisi za Wilaya na Kamati za Shehia zinaendelea kuratibu matukio yote yanayosababishwa na Maafa ili pale inapopatikana fursa ya msaada iweze kuwafikia kwa urahisi Wananchi husika.
Mh. Ayoub alisema kazi hiyo inafanywa kwa umahiri mkubwa bila ya ubaguzi wowote kwa vile jukumu la Serikali wakati wote ni kuhudumia Wananchi wake wote na wakati wowote ule kutegemea mahitaji halisi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kuyakagua Madaraja ya Kibonde Mzungu na Mwanakwerekwe kujionea hali halisi ya maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya vivuko hivyo muhimu kwa utokaji na uingiaji wa Maeneo ya Mjini.     
Balozi Seif  pia alipata nafasi ya kuangalia eneo lililodidimia Kisima, Tangi na Mnara wake pembezoni mwa Madrasa Ismailia iliyopo Mwanakwerekwe, Bwana la Kwa Mtumwa Jeni, Bwawa la Sebleni pamoja na Mtaro wa Jang’ombe ambao kwa sasa umezidiwa na muingio wa maji ya Mvua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.