Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein, Azungumza na Uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiongoza Mkutano wa Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar kwa kipindi cha mwezi wa Julai 2018 hadi Marchi 2019, uliofanyika katika Ukumbi wa Ikulu Ndogo Kibweni Zanzibar leo.14-5-2019. 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein amesisitiza azma ya Serikali ya kuendelea kuwalipa asilimia 80 ya bei ya Karafuu katika soko la Dunia, ili kuwatia moyo wakulima wa zao hilo.

Dk. Shein amesema hayo katika ukumbi wa Ikulu ndogo Kibweni mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda, wakati ilipowasilishwa taarifa ya utekelezaji wa Mpango kazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai 2018 hadi March, 2019.

Alisema pamoja na bei ya zao hilo kupanda na kushuka katika soko la Dunia, Serikali itaendelea na utaratibu wake uliodumu kwa miaka minane sasa wakuwalipa wakulima kiwango hicho, ambapo ni shilingi 14,000/- kwa kilo moja ya daraja la kwanza.

Aliupongeza uongozi wa ZSTC pamoja na watendaji wake kwa utulivu mkubwa unaoliwezesha shirika hilo kupata maendeleo makubwa na kuliendeleza zao hilo.

Dk. Shein, akasisitiza umuhimu wa kufanyika utafiti ili kubaini faida za ziada zitokanazo na zao la karafuu.

Aidha, alisema pamoja na changamoto ya bei ya mwani katika soko la Dunia, Serikali inamatarajio makubwa ya zao hilo kupata ufanisi na bei kuongezeka katika miakai nayokuja.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na  nchi washirika itaendeleza ushirikiano uliopo ili kuhakikisha zao hilo linaendelezwa vyema na kuleta tija kwa wakulima.

Alisema Serikali ina mpango wa kuliimarisha eneo la Chamanangwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa kujenga viwanda vidogo vidogo, ikiwemo vya chumvi.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein alizitaka taasisi zinazosimamia usalama wa chakula kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali nchini zinakuwa na ubora unaohitajika kabla ya kuwafikia walaji.

Alizitaka taasisi hizo kutumia maabara za ndani zilizopo kwa jaili ya uchunguzi, ikiwemo maabara ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali kwa lengo la kuthibitisha usalama wake.

Aidha, aliutaka uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda kuwa na uangalifu mkubwa dhidi ya watu wanaotangaza na kuuza bidhaa zao katika maonyesho yanayoandaliwa na Wizara hiyo, kwa kuzingatia sera na sheria zilizopo.
  
Mapema, Waziri wa Biashara na Viwanda Mhe.Balozi. Amina Salum Ali, alisema hadi kufikia mwezi Marchi 31, 2019 Shirika la Biasharala Taifa (ZSTC) limenunua jumla ya tani 191.40 za Karafuu zenye thamani ya shilingi Bilioni 2.6.

Alisema kupungua kwa kiwango cha zao hilo kutoka tani 3,000 zilizokadiriwa kabla, kunatokana na msimu mdogo wa zao hilo katika kipindi hiki.

 
Aidha, alisema Shirika hilo limeendelea kukifanyia marekebisho kiwanda cha Makonyo kwa kufunga mitambo mipya na vipuri ili kuongeza uzalishaji wa mafuta.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2018/19 kiwanda hicho kilikadiria kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni 1.78, wakati ambapo hadi kufikia Marchi 31,2019 tayari kilikusanya zaidi ya shilingi Bilioni 1.31.
 
Alisema katika kipindi hicho, pamoja na mambo mengine Wizara ilitowa ushauri wa kitaalamu kwa wajasiriamali kutoka vikundi 265 Unguja na Pemba, ikiwemo wazalishaji wa viungo, chumvi, mwani , utenegezaji dawa na asali,miradi ya viwanda vya useremala pamoja na uzalishaji dagaa.

Waziri Amina alibainisha kuwa miongoni mwa changamoto zilizoikabili Wizara ni kuchukuwa mda mrefu zoezi la upimaji wa maeneo ya viwanda, hivyo kuchelewesha utekelezaji wake.

“Wizara tayari imefuatilia kwa karibu suala hili na hati ya umiliki wa eneo la Chamanangwe imekabidhiwa kwa Wizara na maeneo mengine yamo katika hatua za mwisho za kupatiwa hati”, alisema.

Aidha, alisema Wizara imefanikiwa kuyapatia ufumbuzi malalamiko yaliojitokeza kutoka kwa wananchi kuhusiana na ongezeko la bei ya mikate kutofautiana.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.