Habari za Punde

Maklamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Ballozi Seif Azungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Afya na Uwekezaji.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya huduma za Afya na Uwekezaji {KAYI} Bwana Batur Engin akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika na Ujumbe wake kufanya mazungumzo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza jambo wakati akizungumza na Ujumbe wa Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Afya na Uwekezaji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza jambo wakati akizungumza na Ujumbe wa Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Afya na Uwekezaji.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Afya na Uwekezaji kutoka Nchini Uturuki. 
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya huduma za Afya na Uwekezaji {KAYI} Bwana Batur Engin baada ya mazungumzo yao yaliyo lenga katika masuala ya Uwekezaji.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Viongozi Watatu wa Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Afya na Uwekezaji kutoka Nchini Uturuki hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Kiongozi wa Ujumbe huo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya huduma za Afya na Uwekezaji {KAYI} Bwana Batur Engin alimueleza balozi Seif kwamba Taasisi hiyo yenye Wafanyakazi 600 inatoa huduma katika Mataifa 200 Duniani.
Bwana Batur alisema Wahandisi wa Kampuni hiyo huendeleza kazi za Miundombinu ya Ujenzi wa Hospitali kubwa za kisasa zenye vifaa vya Teknolojia mpya unaofanywa katika mfumo wa ubia.
Alisema zipo Hospitali kubwa zilizojengwa katika Miji ya Paris Nchini Ufaransa, Istambul Uturuki yenyewe pamoja na Hospiatli Kubwa zilizopo Nchini Kenya zinazotarajiwa kukamilika Ujenzi wake hivi karibuni.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Afya na Uwekezaji alieleza pia Kampuni yake huendesha Miradi mengine ya Miundombinu katika Sekta ya Mawasiliano kwa ujenzi wa Viwanja vya Ndege, Bara bara Kubwa za Kisasa pamoja na Mahoteli Makubwa.
Alifahamisha kwamba mtazamo wa Kampuni yake kwa sasa umezingatia kuwekeza katika Visiwa vya Zanzibar Miradi zitakayoweza kutoa huduma katika Mwambao wa Afrika Mashariki pamoja na Ukanda Mzima wa Nchi za Sahara.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari inaendeleza Miradi mikubwa ya Ujenzi wa Hospitali ya Kisasa katika eneo la Binguni pamoja na mpango wa Ujenzi wa Bandari ya Mizigo katika eneo la Mpiga Duri.
Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa Viongozi hao kutoka Uturuki kwamba Kampuni yao ina fursa ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uimarishaji wa Ujenzi wa Hospitali hiyo inayotarajiwa pia kuwa na Kitengo cha Mafunzo ya Afya.
“ Inapendeza kuona Ujenzi wa Hospitali Kubwa ya Binguni inafanana na mtazamo wa Kampuni hiyo katika uimarishaji wa Miradi yake katika Huduma za Afya na Uwekezaji Vitega Uchumi”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali hivi sasa ina mtazamo wa uwepo wa Hospitali ya Kimataifa itakayolenga kutoa huduma kwa Watalii pamoja na wageni wanaoingia Nchini kwa safari za kimatembezi.
Balozi Seif alisema mtazamo huo umekuja kutokana na Zanzibar kwa sasa kuimarika katika Sekta ya Utalii inayoweza kuchukuwa nafasi ya kwanza ya Uchumi wake.
Alisema kuimarika kwa huduma za Afya katika Sekta ya Utalii kutaipa hadhi Zanzibar kurejea katika hadhi yake ya kutoa huduma mbali mbali za kibiashara ndani ya Bahari ya Hindi kama ilivyokuwa ikifanya karne nyingi zilizopita kutokana na mazingira yake ya kuwa kituo cha Biashara enzi hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.