Habari za Punde

Wafanyabiashara Zanzibar Waomba Kuweko na Maabara ya Taifa Kupima Ubora wa Bidhaa

Mkurugenzi Mkuu wa ZBS Khatib Mwadin Khatib akizungumza wakati wa hafla ya Kongamano Maalum la Kutathimini Maendeleo ya Utendaji wa Kazi ya Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al Bahr Mbweni Zanzibar.
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar.
Wafanyabiashara nchini wameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha Maabara moja ya Taifa itakayotumika kwa ajili ya kupima viwango vya ubora wa bidhaa wanazoingiza nchini.
Wamesema kwa sasa Ofisi zinazotumika kupimia ubora zipo maeneo tofauti hivyo iwapo maabara hiyo itakuwa sehemu moja itawapunguzia gharama na urasimu wa kufuata huduma katika maeneo hayo.
Wafanyabiashara hao wametoa ushauri huo walipokuwa katika Kongamano maalum la kutathimini maendeleo na utendaji kazi wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) lililofanyika ukumbi wa Hotel ya Madinat Al Bahr nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Wamesema Taasisi kama Vile ZBS, Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi ZFDA, Ofisi ya Mkemia mkuu na nyingine zinazohusika kupima Ubora wa bidhaa zinapaswa kuwa eneo moja ili biashara iweze kwenda kwa ufanisi.
Akijibu hoja za Wafanyabishara hao Mkurugenzi Mkuu wa ZBS Khatib Mwadin Khatib amesema licha ya kuwepo kwa taasisi hizo katika maeneo tofauti lakini kila Taasisi inatekeleza majukumu yake pasina kuingiliana na Taasisi zingine.
Hata hivyo amesema Sera ya Ubora wa Taifa kwa sasa inajadiliwa katika ngazi ya Viongozi kabla ya kupelekwa kwa wadau mbali mbali.
Amesema kukamilika kwa Sera hiyo kutasaidia kupunguza urasimu na gharama za Wafanyabiashara wa Zanzibar.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Hassan Khamis Hassan aliwaomba Wafanyabiashara wa Zanzibar kuendeleza mashirikiano kwa Serikali ikiwemo kulipa Kodi inayostahiki.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuwaomba kutokupandisha Bei za Bidhaa zao kwa kisingizio cha kupata faida za haraka katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
“Ushauri wangu mkubwa kwa ndugu zangu Wafanyabiashara ni kuwa Waadilifu katika biashara zao hasa kipindi hiki cha Mfungo, tusipandishe bei tutawaumiza wananchi wetu” Alinasihi Naibu Waziri Hassan.
Katika Kongamano hilo Mada mbili ziliwasilishwa na kujadiliwa ambazo ni Utekelezaji wa majukumu ya ZBS, Mafanikio na changamoto zake na Madhara ya Bidhaa zilizo chini ya Viwango.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.