Habari za Punde

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Afanya Ziara Kutembelea Idara za Ofisi Yake Zanzibar.

 Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed akizungumza na Wafanyakazi wa Idara ya Watu wenye ulemavu katika ziara ya kushtukizia.
Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye ulemavu Bibi Abeda Rashid Abdulla akimuelezea Nd. Shaaban majukumu ya Idara hiyo lipofanya ziara ya kushtukizia.



 Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar akimuelezea Ndugu Shaaban changamoto wanazopambana nazo katika kuwapatia elimu Wananchi hasa Vijana.
Nd. Shaaban akisisitiza umuhimu wa kutunzwa kumbukumbu alipozungumza na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na. Othman Khamis OMPR. 
Zanzibar imepiga hatua katika kudhibiti maambukizo ya virusi vinavyosababisha kutokana na takwimu zinazoonesha mambukizi ya virusi hivyo kuwa chini ya asilimia moja (1%) ambapo kwa upande wa unguja ni 0.5% wakati kisiwa cha pemba kufikia 0.2%.
Mkurugenzi Mtendaji wa tume ya Ukimwi Zanzibar Dk. Ahmed Momahed Khatib alieleza hayo katika ziara ya kushtukiza iliofanywa na katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa  Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif  Mohamed  kupitia Idara mbali mbali zilizo chini ya Ofisi hiyo.
Dk. Ahmed alisema Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2016/2017 ambapo kwa sasa tume hiyo bado inaendelea na jukumu la kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya hatua za kuchukua katika kujikinga na virusi vinavyosababisha maradhi hayo.
Alifafanua kuwa kwa sasa bajeti ya tume hiyo imefanikiwa kutegemea bajeti ya ndani kwa asilimia kubwa kutokana na serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuongeza nguvu katika bajeti ya tume hiyo  kila mwaka mpya wa fedha hali iliyopelekea kupunguza kutegemea Mataifa na Taasisi wahisani.
Nae Afisa  kitengo cha sera , mipango na mwiitiko wa kijamii wa tume hiyo Bibi Jogha Bakari Mohamed alisema uwepo wa changamoto ya wananchi wengi nchini hususani vijana kwa kulichukulia tatizo la maambukizi ya ukimwi kama jambo la kawaida na kufanya mambo yao bila ya kujali kuchukua tahadhari yoyote jambo linalopelekea kuenea kwa maambukizi.
Mkuu huyo wa kitengo alisema ni jambo linalosikitisha kuona kesi mpya nyingi zinawahusu vijana wengi wanaoripotiwa kuwepo katika hali hatarishi inayosikitisha na kuhuzunisha ikizingatiwa kuwa wao ndio nguvu kazi na tegemeo la Taifa katika masuala ya Maendeleo ya nchi.
Katika ziara hiyo ya kushtukiza watendaji wa tume ya ukimwi walipata fursa ya kuelezea faraja yao pamoja na changamoto zinazowakabili kwa Katibu Mkuu ikiwemo changamoto ya kuchelewa kukamilika kwa mfumo maalum wa kutunzia kumbukumbu zao. {Data Base System}.
Wakati huo huo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizitembelea ofisi za idara ya watu wenye ulemavu na kumtaka mkurugenzi wa idara hiyo kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa mujibu wa mahitaji yao ambao wanatarajiwa kupangwa katika ofisi za wilaya.
Nd. Mkuu Shaaban amewaeleza watendaji wa Taasisi hiyo kufanya kazi kwa uwadilifu kwa kuzitunza vyema nyaraka za ofisi zao sambamba na kuziwasilisha barua zinazoingia idarani mwao kwa wakati badala ya kusubiri mrindikano wa barua hizo, kwani kufanya hivyo kutasaidia mambo muhimu na ya msingi kuchukuliwa hatua bila ya kuchelewa.
Pamoja na mambo mengine Katibu Mkuu Shaaban amelezea kukerwa kwakwe na mpangilio mbaya ya utunzaji wa baadhi ya kumbukumbu na nyaraka katika idara ya watu wenye ulemavu na kuagiza hatua za haraka kuchukuliwa ili kuzinusuru nyaraka hizo kupotea.
Mapema Katibu Mkuu akibadilishana mawazo na watendaji wa tume ya uchaguzi Zanzibar wakimueleza kuwa kwa sasa tume ipo katika mchakato wa kuimarisha kitengo chake cha mfumo wa teknolojia kwa ajili ya kukamilisha zoezi la usajili linalotarajia kuanza hivi karibuni.
Watendaji hao walimueleza katibu mkuu uwepo wa changamoto kwa wapiga kura wengi kutokana na kutokuwa na elimu ya upigaji kura ingawaje tume ya uchaguzi inaendelea na utowaji wa elimu hiyo hali inayosababishwa na ukubwa wa Maeneo ya Zanzibar  ikilinganishwa na idadi ya watendaji  wa tume hiyo.
Ziara hiyo ya kushtukiza ya Katibu Mkuu imejumuisha tume ya ukimwi Zanzibar, Idara ya watu wenye ulemavu pamoja na tume ya uchaguzi ziara ambayo ina lenga kuimarisha utendaji kazi wa idara zilizo chini ya ofisi ya makamu wa Pili wa Rais.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.