Habari za Punde

Balozi Seif Atowa Pongezi Kwa Kurahisisha Huduma za Usafiri Salama wa Tan Tax.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akizungumza na Timu ya Viongozi wa Mfumo Mpya wa kurahisisha huduma za Usafiri salama na uhakika unaozingatia {Tantax} Ofisini kwake Vuga ilipofika kujitambulisha rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akikabidhiwa Kofia na Fulana na Mwakilishi wa Vijana wa Tan Tax.Bi. Salma Salum Othman, baada ya kufika kujitambulisha Ofisini kwake Vuga leo. wakati wa mazungumzo yao yaliofanyika leo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfumo Mpya wa kurahisisha huduma za Usafiri salama na uhakika unaozingatia wakati Bibi Salma Salum Othman wa kwanza Kulia akifafanua jambo wakati Timu yake ilipofanya mazungumzo na Balozi Seif.
Balozi Seif wa Pili kutoka Kushoto akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Viongozi wa Mfumo Mpya wa kurahisisha huduma za Usafiri salama na uhakika unaozingatia {Tantax}.

Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa anzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza Vijana Wazawa walioamua kubuni mfumo Mpya wa kurahisisha huduma za Usafiri salama na uhakika unaozingatia wakati hapa Nchini uitwao Tan Tax.
Alisema ubunifu wao ambao unaungwa mkono moja kwa moja na Serikali kwa njia moja utasaidia kutoa fursa za ajira ambazo kwa sasa zimekuwa na changamoto kubwa hasa kwa Vijana wanaomaliza masomo yao.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa pongezi hizo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Timu ya Viongozi wa Mfumo huo iliyofika kujitambulisha wakijiandaa kuuzindua rasmi siku chache zijazo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar muda wote imekuwa ikihimiza umuhimu wa ubunifu katika Nyanja mbali mbali ndani ya Jamii ambazo hatma yake huleta faraja ya upatikanaji wa Maendeleo sambamba na kupunguza au kuondosha kabisa Changamoto zinazoizunguuka Jamii husika.
Balozi Seif alifahamisha kwamba wakati umefika kwa Jamii hasa Vijana kuondokana na mawazo ya kufikiria Ajira halisi zinazoweza kustawisha maisha na kipato chao hupatikana ndani ya Taasisi za Umma jambo ambalo wanapaswa kutanua mawazo yao zaidi katika kufikiria njia mbadala za Kimaisha.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mfumo Mpya wa kurahisisha huduma za Usafiri salama na uhakika unaozingatia wakati Bibi Salma Salum Othman alisema lengo la kubuniwa kwa Mfumo huo ni kusuluhisha Usafiri ambapo Dereva atakayemuhudumia Abiria atakuwa katika njia ya salama.
Bibi Salama alisema Dereva au Abiria atakayeridhika kutaka kupata huduma kupitia Mfumo huo katika harakati zake za usafiri wa kila siku atawajibika kujiunga kwenye mfumo husika kupitia Simu yake ya mkononi baada ya kuwasilisha vielelezo vitakavyohitajika.
Naye Mhandisi Mkuu wa Mfumo huo Bwana Haji Masoud Abass alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Dereva ambae atakuwa Mwanachama atasajili Bima, Ruhusa na Bara bara pamoja na  leseni yake ili kuwekwa katika mfumo maalum atakaokuwa akiutumia katika kazi zake.
Mhandisi Haji alisema Abiria Mwanachama anapohitaji huduma za Usafiri atatumia mfumo maalum kupitia simu yake ya mkononi itakayomuwezesha kupata huduma kwa usafiri na Dereva atakayepangiwa.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mfumo Mpya wa kurahisisha huduma za Usafiri salama na uhakika unaozingatia wakati Abass Salum alifafanua kwamba kutakuwa na Ukurasa Maalum katika Njia ya Mtandao wa Mawasiliano katika kutoa Taaluma kwa Umma juu ya mfumo huo.
Abass alisema ukurasa huo utakwenda sambamba na upatikanaji wa matangazo ya mfumo huo kupitia njia za Face Book, Twiter, Whatsap na Instragrum wakati watendaji na wataalamu wa Mfumo huo wakiendelea kuutangaza kupitia Tv Online
Alisema uzinduzi rasmi ya Mfumo huo unatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za kigeni Zanzibar Mnamo Tarehe 7 Mwezi huu ambapo Ofa itatolewa ya Shilingi 15,000/- kwa kila Dereva Mpya ili kuhamasisha mpago huo.
Abass alisisitiza kwamba Mfumo huo utazingatia Gari kulingana na hadhi ya kila abiria na mtazamo wao wa baadae kufikiria kuzitumia Bajaji na Boda boda katika azma ya kurahisisha Usafiri Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.