Na
Faidha Jumanne-Maelezo.
Serikali kupitia
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na
wadau wa masuala ya mazingira imefanikiwa kuboresha upatikanaji wa mifuko bora
mbadala kwa wananchi.
Hii imetokama na
jitihada za serikali za kupiga marufuku mifuko hiyo, kuanzia tarehe 01 Juni
2019 na kupelekea kupatikana kwa mifuko mbadala, kwa wananchi inayoimarisha afya zao kuongeza
ajira na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Akihojiwa na Idara ya
Habari - MAELEZO, Afisa Habari Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Lulu Musa,
alianza kusifia juhudi zilizopatikana kwa muda mfupi, huku akirejea Siku ya Maazimisho
ya Usafi Kitaifa Jijini Dodoma, yaliyofanyika Juni 5, 2019.
"Tumetoa katazo la
matumizi ya mifuko ya plastiki kwa wananchi, kazi hii inafanywa na Halmashauri
za Serikali za Mitaa- TAMISEMI kwa kusimamia maeneo yao kwa kutotumia mifuko ya
plastiki hakika wanastahili pongezi, nasema hongereni sana”.
Uamuzi wa Serikali
kuhusu kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki lengo lake ni kuboresha usafi wa
mazingira na kuwaweka wananchi katika hali ya kuepuka magonjwa ya milipuko kama
kipindupindu na kuhara damu.
“Lengo ni kuimarisha
afya. Kadhalika, mazingira salama ambapo,
sote tunatambua umuhimu wa mtu kuwa na mazingira mazuri na yenye usalama kiafya
kwa kushiriki katika shughuli za kijamii na za kitaifa”. Amesisitiza Lulu.
Ameongeza serikali itaendelea kuwa macho kufuatilia
mwitikio mzuri wa wananchi kutoendelea kutumia mifuko ya plastiki, na
kutotegemea watu wengine kusimamia mazingira ya Watanzania, kadhalika akasema bali
iwe ni zoezi la kawaida kwa wananchi.
Lulu akazidi
kufafanua kuwa, serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kutunza
mazingira kwa lengo la kuboresha afya
zao na kufahamu kwa kina mifuko ya plastiki kwa kiasi gani imeleta madhara na
kusababisha magonjwa ya aina mbalimbali yakiwemo nyemelezi, kuteketeza uhai wa viumbe kama vile samaki na
mifugo.
Aidha, Tanzania ni
nchi miongoni mwa nchi zilizoonekana katika orodha ya matumii makubwa ya mifuko
uya plastiki. Hii ilitokana na kuongezeka kwa kasi kwa matumizi hayo kadiri
siku zilivyozidi kwenda, amesema Lulu.
Imeelezwa pia,
Serikali kwa kushilikiana na wadau kama Shirika la Viwango Tanzania -TBS
limeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwenye sekta ya afya na
mazingira yenye lengo la kuboresha matumizi ya mifuko mbadala na kuimalisha
afya za wananchi.
Mfano, TBS imeweka
viwango vya ujazo kwenye mifuko ya plastiki ambayo bado inatumika kama vifungashio
kuepusha kuzagaa kwa mifuko ya plastiki na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Pia, imebainisha viwango vya mifuko
ambayo imeruhusiwa kwa kutumika kwa kufungashia chakula pamoja na madawa ya
kilimo kwa kuangalia uzito/ujazo wa bidhaa, aina za bidhaa ambazo zitatumia
mifuko hiyo ili kuweza kusaidia katika utunzaji wa mazingira.
Vilevile, Lulu aliongezea kuwa shirika la viwango, TBS
litakua na uwezo wa kuwasiliana na wananchi kwa njia yoyote ile hata ikiwa
kimtandao kwa kuwapa taarifa ya matumizi ya mifuko iliyo bora na yenye
viwango ili kuweza kusaidia kutoa huduma
bora kwa wanainchi.
Akielezea mfumo wa
matumizi ya kidigitali Lulu amesema kuwa, Tanzania ilishaingia mfumo wa
matumizi ya kidigitali katika utoaji huduma kwenye maeneo mengi, na imekuwa
msaada mkubwa katika shirika la viwango TBS.
Hata hivyo Tanzania
imekua na matumizi mazuri ya mfumo wa kidigitali kwa kutoa mawasiliano kwa
wananchi katika mambo mbalimbali ya kijamii na kuleta mafanikio chanya katika
mwitikio wa jambo kama hili la katazo ya mifuko ya pllastiki, Lulu akasema, “Kupitia
mfumo huu wa kutoa mawasiliano katika mitandao ya kijamii utasaidia kuongeza
uwingi wa watu katika kupata taarifa kwa uharaka na sisi kutupelekea ufanyaji
kazi wetu kutoa taarifa haraka kwa umma”.
"tutaendelea kuwa
na utaalamu wa hali ya juu kwa kuhakikisha taarifa tutakazo zitoa zitakuwa
taarifa sahihi zenye viwango sahihi kwa kutoa msaada mkubwa sana kwa kuwa hizi
taarifa ni za muhimu sana kwa wananchi’’.
Akiongea mmoja wa
wananchi waliohojiwa, Hashim Chikwaya
ambaye ni mkulima amesema, “ Kutokana na
kusitishwa kwa mifuko ya plasiki, hakika hili ni jambo jema sana kwa wananchi
kwa kuwa wananchi walikuwa wakitumia mifuko hiyo kwa kuhifadhia chakula ambacho
chakula hicho ni chenye joto” alisema Chikwaya.
Akaendelea Chikwaya
ambaye anaonekana kuwa na uzoefu wa kujua athari za mifuko, kuwa Kutokana na
joto la kwenye mfuko linasababisha kutoa mvuke wenye majimaji ya tindikali ambayo
imetumika kutengenezea mfuko huo na kuingia kwenye chakula, iwapo chakula hicho
kikiliwa na mtu, hupata athari kubwa za kiafya.
Vilevile, akielezea zaidi
adhari za kiafya Chikwaya alisema “Kulikuwa na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima
pale mtu anapochukua mfuko wa plastiki kwa matumizi ya kuwashia moto, hususani
jiko la mkaa, kitendo hicho kinapofanyika mtu huyo anavuta hewa ya mfuko unaoyeyuka
na kumsababishia madhara ya kupata ugonjwa wa kansa”.
Akimalizia, Chikwaya alisema,
mbali na uchafuzi wa mazingira mara nyingi, mfano hospitali madaktari walikuwa
wakishauri kuepukana na matumizi ya vifaa vya plastiki kuhifadhia chakula
chenye joto na kusema kuwa plastiki hizo huchubuka zipatapo joto na kusababisha
athari ya upatikanaji wa magojwa pinde ulapo chakula hicho, akaongeza, “hata
hivyo si rahisi kuona michubuko hiyo kwa macho”.
Zoezi la katazo la
Mifuko ya Plastiki limeanza Juni mosi, 2019 ambapo mpaka sasa kwa tafiti imeonyesha
mafanikio, mfano katika Jiji la Dar-es-salaam wengi waliohojiwa mitaa ya
Kariakoo wamesema mitaa yao inaonekana safi kwa kuondolewa mifuko hiyo na hivyo
wanaishukulu serikali.
No comments:
Post a Comment