Habari za Punde

Makamu wa Rais TFF ashukuru michango ya wadau kwa Timu ya Taifa kwa Watu wenye ulemavu wa Amputee Zanzibar

Na Othman Khamis/Rashida Abdi

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Hassan Haji Silima alisema msaada wa uwezeshaji uliokwenda sambamba na Ushirikiano wa Karibu iliyoupata Timu ya Taifa kwa Watu wenye ulemavu wa Amputee Zanzibar imeuwezesha kushiriki Mashindano ya Afrika ya Mashariki yaliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es salaam.
Alisema mchango wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na mawazo ya Viongozi wa Taasisi zinazosimamia Sekta ya Michezo Zanzibar yamewatia ari wachezaji wa Timu hiyo na hatimae walitolewa na Kenya baada ya kufikia hatua ya nusu Fainali ya Mashindano hayo.
Hassan Haji Silima akiuongoza ujumbe wa Viongozi wa Chama cha Michezo kwa Watu wenye Ulemavu wa Viungo Zanzibar alisema hayo wakati wakitoa shukrani zao  kwa wale wote waliochangia kufanikisha safari yao mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema kwenye  mashindano hayo ya CECAAF yaliyoshirikisha Timu za Taifa za Kenya, Uganda, Rwanda, Zanzibar na wenyeji Tanzania BaraWachezaji wa Zanzibar walionyesha uwezo mkubwa ikilinganishwa na baadhi ya Timu nyengine licha ya maandalizi hafifu na ukosefu wa vifaa.
Hassan Haji Silima alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba katika kukabiliana na changamoto tofauti baada ya Timu hiyo kupata Barua ya kushiriki kwenye mashindano hayo katika kipindi kifupi Uongozi wa Chama hicho ulilazimika kukopa baadhi ya Vifaa deni ambalo bado linawasumbua ili kufanikisha malengo ya ushiriki wao.
“ Wewe shahidi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Kamishna wa Michezo Zanzibar, Katibu wa Baraza la Taifa la michezo pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu walijitahidi kuichangia Tumu yetu, jambo ambalo lilileta faraja kwetu sote”. Alisema Hassan Haji Silima.
Makamu wa Rais huyo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kupitia Balozi Seif  aliwaomba Washirika wa Sekta ya Michezo ndani na nje ya Nchi kuendelea kusaidia Vifaa vya Michezo pamoja na vile vya Ofisi kwa Timu za Watu wenye Ulemavu Nchini.
Alisema ni vyema msaada huo ukaenda sambamba na Kundi hilo kupatiwa usafiri wa uhakika kwa kila mwisho wa Mwezi ili kuhamasisha mchezo huo katika ilaya zote za Unguja na Pemba pamoja na kuwasfirisha wachezaji waliopo Tanzania Bara kujumuika pamoja katika uhamasishaji huo.
Akitoa shukrani zake na kukubali kuwa Mlezi wa Chama cha Michezo kwa Watu wenye Ulemavu wa Viungo Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliuhakikishia Uongozi wa Chama hicho kwamba Serikalipamoja na Taasisi zinazosimamia Michezo zitandelea kuunga mkono Watu wenye Maalum Maalum wakati wote.
Balozi Seif alisema Serikali pamoja na Jamii imeshuhudia uwezo mkubwa ulionalo Kundi hilo katika ushiriki wa Mashindano ya Kitaifa na Kimataifa yanayowawezesha kupata ushindi na nishani mbali mbali zinazobakia kuwa Historia hapa Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.