Habari za Punde

Wanahabari watakiwa kutoa habari sahihi na kwa wakati - Wito

Na Mwashungi Tahir Maelezo
     
MKURUGENZI wa Habari Maelezo na msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Dkt. Hassan Abbas amewataka Wanahabari kutoa habari sahihi na kwa wakati ili jamii iweze kunufaika vyema na fursa zitokanazo na Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC utakaofanyika nchini.
Dkt. Abasi ametoa wito huo alipokuwa akifunga mafunzo kwa Waandishi wa Habari yanayohusiana na uandishi wa kina wa Mkutano wa SADC yaliyofanyika ukumbi wa Magadu Mkoani Morogoro.
Amesema kwa vile Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Dar es Salaam mwezi unaokuja hivyo ni vyema Watanzania wakafahamu umuhimu wa mkutano huo ili waweze kunufaika vyema na SADC.
Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuelimisha jamii juu ya matukio mbali mbali yanayotokea duniani hivyo ni wajibu kuhakikisha elimu waliyoipata inawafikia wanajamii wote kwa ujumla.
“Vyombo vyetu vya habari vina mchango mkubwa katika kuelimisha jamii, hivyo tutoe taarifa ziwafikie walengwa ili jamii iweze kuelewa SADC”, alisema Mkurugenzi huyo.
Dkt. Abas pia aliwataka Wanahabari kuwa Mabalozi wazuri kwa Watanzania wanaofikia Milioni 55 wenye kiu ya kufahamu SADC na mchango wake nchini.
Amewataka Wajasiriamali na Wafanyabiashara mbali mbali kujiandaa kikamilifu hasa kwa kuzingatia kuwa kabla ya Mkutano huo kutakuwa na maonesho ya Viwanda ya SADC yatakayofanyika Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Maelezo Zamaradi Kawawa alisema lengo la mafunzo hayo ni kuvishirikisha vyombo vya habari ili viweze kutangaza masuala muhimu za SADC na jamii iweze kupata taarifa za kina.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wameshukuru kwa kupatiwa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo na kuahidi kuyafanyia kazi ipasavyo.
Aidha waliiwaomba Watayarishaji wa Mafunzo hayo kuendelea kutoa mafunzo kila inapotokea Fursa ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa na kutimiza lengo lililokusudiwa.
Katika Mafunzo hayo Mada mbali mbali ziliwasilishwa ikiwemo Wiki ya Viwanda, maadili ya vyombo vya habari ,  na kujadiliwa kwa kina.
Mkutano huo wa SADC unaotarajiwa kufanyika mwezi unaokuja unatarajiwa kuhudhuriwa na Marais 16 wa nchi zinazounda SADC ambapo Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli anatarajiwa pia kupokea Kiti cha Uenyekiti wa SADC kutoka kwa Rais wa Namibia Hage Geingog.
Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika Magadu Morogoro  yameandaliwa Idara ya Maelezo Dar es Salaam na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.