Habari za Punde

Rais Magufuli: Tuimarishe umoja na mshikamano kuijenga SADC kuleta maendeleo kwa wananchi




STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
 Dar es Salaam                                                         18.08.2019
---
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amefunga mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kutoa pongezi zake kwa heshima iliyopewa Tanzania kufuatia lugha ya Kiswahili kuteuliwa kuwa lugha ya nne itakayotumiwa rasmi katika Jumuiya hiyo.

Hafla hiyo imefanyika leo katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi hizo za (SADC) uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar-es-Salaam uliohudhuriwa na viongozi  mbali mbali wa nchi za Jumuiya hiyo ya (SADC) akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Magufuli alieleza kuwa kukifanya Kiwashili kuwa ni lugha rasmi ya Jumuiya hiyo ni heshima kubwa hasa kwa muasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kusisitiza kuwa kiongozi huyo alikuwa na upendo kwa watu na alijitolea kutoa upendo wake sio tu kwa Watanzania bali hata   wananchi wa nchi jirani na Afrika kwa jumla.

Alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika kuhakikisha amani na utulivu inapatikana kwa nchi za Bara la Afrika. Juhudi hizi ni kuendeleza historia kubwa ambayo iliyoanza wakati wa harakati za ukombozi ambapo katika harakati hizo
 lugha ya  Kiswahili ilitumika na ilikwa na mchango mkubwa katika kuwaunganisha  wanaharakati  wa nchi mbali mbali

Akitolea mfano, Rais Magufuli alisema kuwa mnamo mwaka 1975 Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) lilikwenda nchini Shelisheli kuzima Mapinduzi pamoja na nchi nyengine kadhaa za Bara la Afrika.

Alieleza kuwa kutumika kwa lugha ya Kiswahili katika Jumuiya hiyo imepelekea Watanzania kufurahishwa na hatua hiyo na kuwapongeza wakuu wa nchi za (SADC) kwa kukuza na kuendelea historia hiyo ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya nne katika Jumuiya hiyo.

Alisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza ushirikiano na utengamano wa wananchi “Kiswahili ni lugha ya Afrika na sisi ni wananchi wa Bara hilo hivyo tunapaswa kuitumia lugha ya Kiswahili”, aliongeza Dk. Magufuli.

Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa nchi za (SADC) kuiga mfano wa nchi ya Afrika ya Kusini ambayo kuanzia mwakani itaanza kufundisha Kiswahili katika Skuli zake na kuongeza kuwa Tanzania iko tayari kusaidia kufanikisha malengo ya Taifa hilo la kufundisha na kutumia Kiswahili katika shughuli mbali mbali.

Aidha, Rais Magufuli alieleza kuwa mkutano huo wa siku mbili umekuwa wa mafanikio makubwa sana na kuweza kufanyika kwa upendo mkubwa huku akieleza kuwa viongozi wakuu wa nchi za (SADC) walijadiliana kwa umakini mkubwa na hatimae kufikia makubaliano ambapo ajenda nyingi zilijadiliwa na kufikia maamuzi.

Akieleza jinsi nchi za Jumuiya hiyo zilivyoshindwa kufikia kukua kiuchumi kwa asilimia saba na badala yake zilikuwa kwa asilimia tatu hivyo Rais Magufuli alisisitiza haja ya kuimarisha Sera za uchumi na fedha kwa nchi hizo.

Pamoja na hayo, alieleza kuwa ombi la Burundi la kujiunga na Jumuiya hiyo pamoja na suala la Zimbwabwe yalizungumzwa na kufikiwa muwafaka mzuri ambapo nchi zote wanachama zimeunga mkono nchi ya Zimbabwe kuondolewa vikwazo huku kwa upande wa Burundi imepewa muda zaidi kukamilisha baadhi ya mambo.

Rais Magufuli pia, alitumia fursa hiyo kueleza jinsi Itifaki zilizosainiwa katika mkutano huo wa leo na kusema kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa mikakati ya kuhakikisha maamuzi yanatekelezwa kwa haraka zaidi.

Aliipongeza ripoti ya Mwenyekiti anaemaliza muda wake pamoja na ripoti ya Sektarieti kwa kuwa zimebainisha wazi kazi nzuri iliyofanywa na viongozi hao katika kipindi chote cha uongozi wao. Aidha, alitoa pongezi kwa washirika wa maendeleo  na taasisi mbali mbali za Kimataifa  zinauna mkono na kufanya kazi kwa karibu na Jumuiya ya (SADC).

Nae Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi alitoa nene la shukurani katika mkutano huo,  ambapo alitoa a pogezi kwa mashirikiano yaliopo katika Jumuiya hiyo na kutoa pongezi maalum kwa Rais Magufuli kwa Tanzania na wananchi wa Tanzania kwa kufanikisha mkutano huu na ukarimu mkubwa walionyesha kwa wageni waliofika nchini.

Sambamba na hayo, alitumia fursa hiyo  kutoa shukurani kwa  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  Wananchi  kwa misaada mbali mbali waliyotoa kwa
ndugu zao wa Msumbiji wakati walipopata janga la kimbunga na mafuriko nchini humo.

Vile vile,  alitumia fursa hiyo kuwakaribisha viongozi wote wa (SADC) katika Mkutano wa 40 utakaofanyika nchini Msumbiji mwaka 2020 ambapo Rais wa  nchi hiyo atakabidhiwa kijiti cha Uwenyekiti wa (SADC).

Mapema zoezi la kutiwa saini  kwa Itifaki na viongozi wan chi za Jumuiya hiyo lilifanyika.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.