Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Afungua Hoteli ya Madinat Al Bahr Mbweni Nyeye Hadhi ya Nyota Tano.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Hoteli ya Kitalii ya Madinat Al Bahr Mbweni Zanzibar Nyeye hadhi ya Nyota Tano.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa kujengwa kwa hoteli ya kisasa ya Madinat El Bahr ni hatua kubwa ya mafanikio katika mipango ya maendeleo kwenye sekta ya utalii ambayo inachangia asilimia 27 ya pato la taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa hoteli ya Madinat El Bahr iliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar, hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama na serikali pamoja na wawekezaji na wafanya biashara kadhaa kutoka katika sekta ya utalii.

Katika hotuba yake Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania, sekta ya utalii inachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazoingia Zanzibar ambapo taarifa za Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar zinaeleza kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, utalii umechangia kiasi kikubwa katika upatikanaji wa ajira.

Alieleza kuwa katika medani ya biashara ya Kimataifa inaeleweka kwamba utalii ndio sekta kuu miongoni mwa sekta zinazotoa huduma na ina mchango mkubwa katika uchumi wa dunia.

“Nina furaha kuona kwamba, sera na mipango yetu ya kukuza utalii inatufanya na sisi tuwe wenye kunufaika na neema za utalii kwa kadri sekta hii inavyokua duniani”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa katika mwaka 2017 sekta ya utalii ilitoa ajira takriban 28,000 za moja kwa moja ambazo ni zile ajira zinazohusu shughuli halisi za utalii na zaidi ya ajira 60,000 zisizo za moja kwa moja ambazo zinazinufaisha sekta nyengine za kiuchumi kutokana na shughuli za utalii.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa ufanisi wa mipango na sera katika kuendeleza utalii unadhihirika wazi wazi katika matokeo ya utafiti juu ya sekta ya utalii uliofanywa na UNICEF kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii Zanzibar mwaka 2018.

Alieleza kuwa utafiti huo umeonesha kwamba utalii umekuwa na mchango mkubwa kwa uchumi wa Zanzibar katika kukuza ajira, hali za maisha ya watu na utekelezaji wa mipango na mikakati ya kupunguza umasikini.

“Imeelezwa kwamba pato linalopatikana kutoka sekta ya utalii limekuwa likiongezeka kwa kiasi kikubwa kila mwaka kwa mfano pato hilo liliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 157.1 mwaka 2011 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 269.3 katika mwaka 2014 na katika mwaka 2017 tayari lilikuwa limeshafika Dola za Kimarekani milioni 489”,alisema Dk. Shein.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa idadi ya watalii wa kimataifa waliofika Zanzibar tangu mwaka 2008 hadi mwaka huu imekuwa ikiongezeka kwa kiwango kizuri ambapo hadi mwaka 1985 idadi ya watalii waliofika Zanzibar ilikuwa chini ya 20,000 ambapo hadi Disemba mwaka 2018 idadi ya watalii ilifikia 520,809.

Rais Dk. Shein alisema kuwa hayo ni matunda ya juhudi zilizochukuliwa ambayo yametokana na mipango bora na Sera sahihi ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mikakati mbali mbali, mpango wa Utalii kwa Wote na kuimarisha utawala bora ambayo inahakikisha mazingira ya amani, utulivu na usalama kwa wageni na wawekezaji.

Hata hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuongezwa kwa  kasi na mipango bora zaidi katika kuwatembeza watalii kwenye makumbusho yaliopo na baadhi ya maeneo muhimu ya historia wkani bado idadi ya wageni wanaotembelea makumbusho ni ndogo.

Hivyo, Dk. Shein alitoa agizo kwa Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar na Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale, ziandae mkutano maalumu na makundi mbali mbali katika sekta ya utalii kwa ajili ya kupanga na kushauriana juu ya namna bora itakayowezesha kuwavutia wageni wanaokuja Zanzibar kutembelea makumbusho ili waifahamu historia ya Zanzibar.

Pia, Rais Dk. Shein alitoa agiza kwa kuwataka wamiliki wa hoteli na wawekezaji kuendelea kushirikiana na Kamisheni ya Utalii katika utekelezaji wa mipango ya kujitangaza katika masoko mapya.

Alisisitiza kwamba Serikali itaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha utalii kama ilivyoelezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na 2020, MKUZA III pamoja na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi wa Kamisheni ya Utalii kwa kusimamia vizuri hatua zilizowezesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuingia katika makubaliano na Kampunni ya Touchroad ya China ambayo ilitiwa saini tarehe 21 Julai, 2019.

Alieleza kuwa makubaliano hayo ni kwa ajili ya kuleta wageni hapa Zanzibar kutoka China ambapo kupitia makubaliano hayo Zanzibar inatarajiwa kupokea ndege za moja kwa moja zitakazoleta watalii kutoka China hatua ambayo itaongeza watalii kutoka 8,127 ya mwaka 2018 hadi kugfikia 18127 mwaka 2020.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alisema kuwa Serikali imefarajika sana na uwekezaji huo na kusisitiza kuwa Serikali inajali na imekuwa ikilipa umhimu suala la utalii kwa kutambua umuhimu wake katika mapato ya nchi.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM sambamba na mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Dira 2020 ambayo ilielekeza hadi 2020 watalii wanaofika Zanzibar wafikie laki 500,000 lakini kwa sasa  idadi hiyo imevukwa kabla ya muda na kufikia watalii 520,809 waliofika nchini mwaka jana 2018 huku watalii wengi wanaoingia sasa ni wa daraja la juu.

Nae Mmiliki wa Mradi huo wa Hoteli Rustamali Merali Shivji  alipongeza mashirikiano makubwa aliyoyapata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mamlaka ya (ZIPA), na kumshukuru Dk. Shein kwa kumshauri kuja kuekeza Zanzibar tokea walipokutana mwaka 2004 wakati alipokwenda kumzindulia hoteli yake  ya  “New Dodoma Hotel”, mjini Dodoma wakati Dk. Shein akiwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Alieleza kuwa mradi huo wa Hoteli ya hadhi ya nyota tano umechukua muda wa miaka minane kukamilika ambao una ukubwa wa mita za mraba 22000 ambao umegharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 38 huku akisisitiza kuwa mradi huo utasaidia kupanua soko la ajira na pato la Taifa.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Iddi Haji Makame akitoa maelezo mafupi ya Mradi huo alisema kuwa Mradi huo wa “ Pristine Investments” uliidhinishwa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) mwezi Disemba mwaka 2008 chini ya kiongozi wake Rustamali Merani Shivji na Bi Amina Chandoo wote ni raia wa Tanzania.

Aliongeza kuwa Pristine Investments ilipanga kuwekeza dola za kimarekani milioni 12 katika hoteli hiyo yenye hadhi ya nyota tano lakini hata hivyo kutokana  na matakwa ya soko la utalii na aina ya utalii mwekezaji wa mradi huo kwa vile amelenga kuvutia watalii wa nje na wa ndani ilipelekea kuongezeka mara dufu gharama ya hoteli hiyo.

Naibu Katibuhuyo alieleza kuwa  hoteli hiyo ya kifahari ina vyumba 129 vya aina tofauti pamoja na mikumbi mbali mbali yenye kuhudumia wageni wote .

Alisema kuwa mradi huo umetengeneza ajira 139 na tayari jumla ya wafanyakazi 125 wazalendo na wageni 14 wameajiriwa na kueleza kuwa kukamilika kwa mradi huu kumeifanya miradi iliyoidhinishwa na Mamlaka ya (ZIPA) kufikia 717 yenye mtaji wa makisio ya dola za Kimarekani Bilioni 6.4 ambapo jumla ya Miradi 409 inatoa huduma na 49 iko katika hatua za ujenzi.

Lakini hata hivyo, alisisitiza kuwa sekta ya utalii inaongoza kwa kuwa na miradi 432 ambayo ni sawa na asilimia 60.2.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali walihdhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume pamoja na wekezaji kadhaa akiwemo Sheikh Said Salim Baghressa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.