Habari za Punde

Wamiliki wa Skuli binafsi zilizofanya vibaya mtihani wa majaribio wa kidatu cha nne watakiwa kujieleza

Na Mwashungi Tahir     Maelezo     

MKOA WA MJINI MAGHARIBI
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed amewaagiza walimu wakuu pamoja na wamiliki wa skuli binafsi wa skuli 20 zilizopata nafasi za mwisho katika mitihani ya majaribio ya kidatu cha 4 iliyofanyika mwaka huu kuandika barua ya kueleza sababu za kufanya vibaya skuli zao ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi kabla ya mitihani ya mwisho. 

Ayoub ametoa agizo hilo mara baada ya kupokea taarifa ya matokeo ya mitihani ya majaribio  (Mock) ya kidatu cha nne iliyofanyika juni mwaka huu kutoka kwa kamati ya mitihani ya mock ya mkoa wa mjini magharibi huko ofisini kwake vuga mjini Zanzibar. 

Amesema lengo la mkoa ni kuona skuli zote zinafanya vizuri katika mitihani yao hivyo ameitaka kamati hiyo kuandaa mikakati maalumu ya kuinua ufaulu katika skuli zilizokuwa hazijafanya vizuri katika mitihani ya majaribio ili kuongeza ufaulu katika
mitihani ya mwisho .

Akizungumzia suala la utoro Ayoub amefahamisha kuwa serikali ya mkoa itaanza kutangaza vita kwa wazazi wasiosimamia vizuri watoto wao katika masuala ya elimu ili kuona kila mtu anawajibika katika kuimarisha maendeleo ya elimu katika Mkoa.

“Hali ya utoro imekuwa imekuwa kubwa hivyo Serikali ya Mkoa haitovumilia suala hili hivyo tunaanza kutangaza vita kwa kupambana na wazazi wasiowajibika kwa watoto wao wasiowasimamia vizuri”, alisema Mkuu wa Mkoa huyo.

Akiwasilisha taarifa ya matokeo hayo Mwenyekiti wa mitihani ya majaribio mock
mkoa wa mjini magharibi Mussa Hassan Mussa amesema licha ya changamoto mbalimbali kujitokeza katika mitihani hiyo lakini ufaulu kwa mwaka huu umeongeza kwa asilimia 65.42 ambapo kwa mwaka jana kulikuwa na ufaulu wa asilimia 63.20.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya elimu mkoa wa mjini magharibi Mabrok Jabu Makame amewataka wafunafunzi waliyofanya vizuri kwenye mitihani hii ya majaribio kuwa na jitihada zaidi na waliofeli kutumia muda huu kufanya bidii ya kusoma ili kuongeza ufaulu katika mitihani ya taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.