Habari za Punde

ZURA Yakifunga Kituo Cha Mafuta Kwa Muda

Kituo cha kuuzia Mafuta cha Kijangwani Wilaya ya Mjini Unguja kilichofungwa kwa muda na Mamlaka ya Udhibiti,  Huduma za Maji na Nishati  Zanzibar (ZURA)   kwa  kutokufuata agizo lilotolewa na mamlaka hiyo

(Picha na Mwashungi Tahir Maelezo)
Na. Mwashungi Tahir - Maelezo Zanzibar 15/08/2019
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imewataka wamilki wa vituo vya kuuzia mafuta kufuata bei elekezi zinazoelekezwa na Mamlaka hiyo ili kuweza kuondoa usumbufu unaweza kujitokeza.
Wito huo ameutoa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mamwasiliano (ZURA) khuzaimat Bakar Kheir mara baada Mamlaka hiyo kufanya ukaguzi katika vituo vya kuuzia mafuta kwa ajili ya kuangalia bei ya uuzaji wa mafuta kwa wananchi.
Amefahamisha kuwa ZURA inahakikisha kwamba kabla ya kutangaza bei mpya ya mafuta katika vyombo vya habari hupeleka taarifa katika vituo vya kuuzia mafuta.
Amefahamisha kuchelewesha kufanya mabadiliko katika vituo ni kosa hivyo mamlaka  hulazimika kuchukua hatua zinazostahiki mara  baada ya wakaguzi kutoka katika Mamlaka kuthibitisha kuwepo hali hiyo.
“ZURA inahakikisha kwamba kabla ya kutangaza bei mpya ya mafuta katika vyombo vya habari tunapeleka taarifa katika vituo vya kuuzia mafuta ili kupata taarifa mapema ili kutochelewesha na kwenda sambamba na mabadiliko yaliwekwa na Mamlaka”, alifahamisha Mkuu wa Kitengo.
Amesema Mamlaka imefanya ukaguzi huo katika vituo vyote vya Unguja na Pemba ambapo  vituo vinne kutoka Unguja vilibainika kutofuata bei elekezi na kupelekea kusimamishwa huduma ya uuzaji wa mafuta katika vituo hivyo.
Amevitaja vituo vilivyofungiwa ni pamoja na Kituo cha Kijangwani, Mwanakwerekwe, Dunga na Kikungwi ambavyo vilikiuka kufuata utaratibu wa kuuza bei halali.
Hata hivyo vituo hivyo viliweza kulipa faini ya dola 500 iliyoelekezwa na sheria za Mamlaka hiyo na huduma zilirejea kama kawaida baada ya kufungiwa.
Akizungumzia uboreshaji wa vituo khuzaimat amesema Mamlaka ZURA inaendelea kutoa maelekezo ya kuviboresha vituo vya kuuzia mafuta ili viweze kuendana na ubora unaotakiwa katika kutoa huduma hiyo.
Aidha amewataka wananchi kutoa mashirikiano kwa kutoa taarifa za vituo ambavyo vinakwenda kinyume na maelekezo ya Mamlaka hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.