Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Alifunga Rasmin Tamasha la JAMAFEST.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif  akihutubia wakati wa ufungaji wa Tamasha la Pili la Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki lililokuwa likifanyika kwa siku Nne katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam.
Na.Othman Khamis.OMPR.                                                                                            
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa rai kwa washirika wa Utamaduni kuongeza jitihada katika kuthamini, kubuni na kuzalisha bidhaa za Kiutamaduni zenye ubora na  viwango vinavyokubalika ili ziweze kushindaniwa katika Masoko ya Kitaifa na Kimataifa.
Alisema Tasnia ya Kazi za ubunifu na Utamaduni kwa ujumla zina mchango mkubwa katika kuchochea kasi ya kuviendeleza Viwanda vidogo vidogo ambavyo mali ghafi hutumika kutengenezea bidhaa mbali mbali zinazotokana na Utamaduni.
Akilifunga Tamasha la Nne la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki {JAMAFEST} lililodumu kwa siku Nane katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam Balozi Seif Ali Iddi alisema Sekta yaUbunifu imekuwa ikitoa mchango mkubwa  wa fursa za Ajira kwa baadhi ya Watu na Makundi tofauti ya Jamii.
Balozi Seif  alisema Kazi za Ubunifu ambazo hufanywa zaidi na  Wajasiri Amali , Vikundi vya Sanaa, Maonyesho na michezo ya Jadi kupitia Viwanda mbali mbali zimeendelea kuinua Uchumi wa Watu Binafsi pamoja na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aliupongeza Uamuzi mzuri uliozaa Busara wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wa kutambua nafasi ya Sekta ya Utamaduni na Sanaa za Ubunifu kuwa miongoni mwa nyenzo zinazoweza kutumika katika kukuza Uchumi na kuimarisha Utengamano wa Kikanda.
Balozi Seif  alisema uamuzi huo ndio uliosababisha kuzaliwa kwa Tamasha la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwafanya Wanajumuia kukusanyika pamoja kuonyesha Utajiri wao wa Urithi mkubwa wa Utamaduni wao.
“Tuwapongeze sana Viongozi wetu Wakuu wa Jumuiya kwa uamuzi wao mzuri na muhimu kwa manufaa ya Kizazi cha sasa na kile cha baadae ndani ya Jumuiya yetu” Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Tamasha hilo limefanikiwa kupanua soko la Bidhaa na Kiutamaduni  sambamba na Wigo wa mawasiliano katika kutekeleza shughuli za kila siku za Wanachama wa Jumuiya hii.
Balozi Seif alisema wengi walioshiriki Tamasha hilo wamefanikiwa kuuza na kununua Bidhaa kutoka kwa Wadau na Wafanyabiashara mbali mbali jambo ambalo linakuza kuongeza vipato vya Uchumi wa Nchi Wanachama.
Alisema inapendeza kuona Tamasha hili la Kihistoria la Utamaduni linalogusa Nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki ambalo Mwaka huu  limeshirikisha Visiwa vya Mayotte vilivyo  nje ya Jumuiya ikionyesha ushahidi wa wazi kwamba kinachofanyika katika Jumuiya kinavutia na Mataifa mengine.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa mdau mkubwa wa Utamaduni na masuala ya Sanaa amekiri na kufurahishwa na Ujumbe wa Mwaka huu wa Tamasha la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki usemao uanuwai wa Utamaduni:- kichocheo cha Utangamano wa Kikanda, Ukuaji wa Uchumi na kuendelezwa kwa Utalii.
Balozi Seif Alisema Ujumbe huu unasisitiza kwamba Utamaduni umekuwa ni kichocheo cha Ukuaji wa Sekta ya Utalii kupitia Vivutio vya Asili na vya Utalii na Kiutamaduni vinavyopatikana miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema baadhi ya Washiriki wa Tamasha hilo wamejionea wenyewe Utajiri mkubwa wa vivutio vya Asili na Utamaduni wakati walipopata fursa adhimu ya kutembelea vivutio vilivyopo Nchini Tanzania ikiwa ni moja ya Nchi Mwanachama.
Hata hivyo Balozi Seif  aliwaomba Washiriki hao wakipata fursa yoyote wasisite kufika katika Visiwa vya Zanzibar vya marashi ya Karafuu ili waone maeneo ya Kihistoria na Kiutamaduni ukiwemo Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni Moja kati ya Urithi wa Utamaduni Duniani pamoja na Bagamoyo na Kilwa.
Alielezea matumaini yake kwamba Tamasha hili litaendelea kuwa chachu kwa Matamasha  mengine yajayo katika kuenzi, kulinda, kudumisha na kuendeleza uanuwai wa Urithi wa Utamaduni miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Balozi Seif alisisitiza kwamba jambo kubwa zaidi ni kwamba kuendelea kufanyika kwa Matamasha ni hatua muhimu sana katika kukuza na kuimarisha Umoja, Upendo wa Udugu na Ushirikiano wa Kidiplomasia uliopo baina ya Nchi za Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mapema akitoa Taarifa ya Tamasha hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania  Bibi Suzan Mlawi alisema Tamasha hilo lilitanguliwa na Maandamano ya Wasanii kutoka Nchi Tano Wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Katibu Suzan alisema jumla ya Vikundi 61 kutoka Nchi hizo vilishiriki vikiwa na idadi ya Washiriki 2,893, michezo ya Watoto wadogo ambapo Tamasha hilo lilitoa fursa kwa Wananchi zaidi ya 100,000 walitembelea Maonyesho hayo kwa siku Tofauti.
Alisema inapendeza kuona kwamba Takwimu za Kiteknolojia  ya Habari na Mawasiliano zimebaini kwamba Maonyesho hayo ya Pili yamefuatiliwa takriban na Watu zaidi ya Milioni 3,000,000 kupitia Mitandao ya Kijamii Duniani.
Bibi Suzan Mlawi alifahamisha kwamba Tamasha hilo pia lilishuhudiwa na uwepo wa ushindani wa Filam, Michezo ya jadi kama Bao kukuna Nazi pamoja na sarakasi likiwepo pia soko la Maonyesho ya vyakula vya asili pamoja na kuhitimishwa na Washiriki Wanne kupanda Mlima Kilimanjaro hadi Kileleni.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania  amewashukuru Washirika wa Tamasha hilo waliojitolea kudhamini Tamasha la Utamaduni zikiwemo Taasisi na  Mashirika ya Umma pamoja na Vyombo mbali mbali vya Habari.
Akitoa salamu za Jumuiya ya Afrika Mashariki Kaimu Katibu Mkuu wa Sekreterieti ya Jumuiya hiyo Bwana Christopher Babizabi  alisema Ushiriki wa Wanajumuiya katika Tamasha la JAMAFEST ni ishara na muendelezo wa pamoja wa Wananchi wa Mataifa hayo.
Bw. Christopher alisema kinachostahiki katika muelekeo wa sasa  ni kuongeza mahusiano yatakayozifanya Nchi za Jumuiya kuwa Moja na kutoa shukrani maalum kwa Watoto waliojitokeza kushiriki Tamasha  hilo ikiwa ni njia sahihi ya kujifunza Utamaduni ambao ndio watakaokuwa na dhima  na dhamana ya kuulinda katika maisha yao ya Utumishi hapo baadaye.
Akimkaribisha mgeni Rasmi kuzungumza katika hadhara hiyo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Dr. Harrison Mwakyembe Waziri Mwenyeji wa Tamasha hilo alisema Viwango vya Tamasha la Mwaka huu vimetia fora ikilinganishwa na vile vya awali.
Dr. Mwakyembe alisema muelekeo mkubwa wa maingiliano ya Washiriki wa Tamasha hilo umeonyesha kufungua ukurasa mpya  kwa Wasanii kuendelea kushikamana chini ya mwamvuli wa  Utamaduni na Sanaa.
Katika ufungaji huo wa Tamasha la Pili la Utamaduni wa Jumuiya ya Afrika Mashariki {JAMAFEST} Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa Tuzo na zawadi mbali mbali kwa washindi wa Mashindano ya Sanaa, Filam,  Insha, na Mwanahabari bora kwa kwa kutangaza Utalii na Utamaduni.
Tamasha la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki hufanyika kila baada ya Miaka Miwili kwa Nchi Wanachama kwa mzunguuko  ambapo lile lililopita lilifanyika Nchini  Uganda Mnamo Mwaka 2017 na la Mwaka huu Tanzania imekuwa Nchi mwenyeji wa Tamasha la Nne.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.