Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapiunduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Awasili Nchi leo Akitokea Ziarani Ras Al Khaimah.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapiunduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar, katika ukumbi wa VIP Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, baada ya kuwasili akitokea Ras Al Khaimah, baada ya kumaliza ziara yake ya wiki moja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amerejea nchini leo akitokea Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambapo alifanya ziara nchini Ras Al Khaimah pamoja na Abudhabi ikiwa ni muwaliko wa kiongozi wa Ras Al Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi kwa ziara ya wiki moja.

Ziara hiyo ya Rais Dk. Shein ilianza tarehe 23 na kumaliza jana tarehe 28 Septemba mwaka huu 2019 ambapo katika ziara hiyo, alipata fursa ya kuzungumza na mwenyeji wake Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi pamoja na kuzungumza na Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)

Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Rais Dk. Shein alipokewa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali pamaaoja na  viongozi wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

Mara baada kuwasili kiwanjani hapo, Rais Dk. Shein alifanya mazungumzo na Waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali vikiwemo vya Serikali na binafsi ambapo katika maelezo yake alieleza mafanikio makubwa ya ziara hiyo ikiwa ni pamoja na mapokezi mazuri aliyoyapata yeye na ujumbe wake aliofuatana nao.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza hatua zilizofikiwa na Kampuni ya Mafuta ya “RAK GAS” inayojishughulisha na utafiti wa mafuta na gesi asilia hapa Zanzibar na kusisitiza kuwa kazi iliyofikiwa ni nzuri na kila hatua itakayofikia wananchi wataelezwa.

Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wasihadaiwe na wale wanaopenda kusema kuwa Rais amefunja sharia na katiba  na kusisitiza kuwa suala la mafuta na gesi liko vizuri wala hakuna Sheria wala Katiba iliyovunjwa.

Rais Dk. Shein pia, alieleza namna ya Kiongozi wa Abudhabi Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan alivyomuhakikishia kuwa yuko tayari kuiunga mkono Zanzibar katika kutafuta nishati mbadala ambayo kwa upande wa Zanzibar nishati hiyo inatazamiwa kuwa itakuwa nishati ya jua.

Alieleza kuwa tayari Zanzibar kazi imeshaanza kufanywa katika kuhakikisha nishati mbadala ya jua ndio kipaumbele ambapo kwa mashirikiano ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na Umoja wa Ulaya (EU).

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa tayari kuna wawekezaji ambao wako tayari kuja kuekeza katika umeme wa jua ambapo kwa upande wa Serikali imo katika kuandaa mipango madhubuti.

Rais Dk. Shein alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa fedha zake wenyewe kwa ajili ya uendeleza wa ujenzi wa jengo jipya la abiria la uwanja wa ndege huku akieleza hatua za ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri ambayo alieleza azma ya Serikali kuanza ujenzi japo wa awali kabda hajamaliza muda wake.

Alieleza kuwa tayari fedha za Mkopo kutoka Benki ya Exim ya Indonesia umepatikana sambamba na ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi huko Mangapwani ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kwa upande wa msaada wa fedha Bilioni 23 zilizotolewa na Mfuko wa Khalifa Fund, Rais Dk. Shein alisema kuwa mbali ya fedha hizo pia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itatoa fedha kama hizo na kufikia Bilioni 46 kwa ajili ya kuwawezesha vijana wakiwemo wajisiriamali na wanawake

Alisisitiza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano na ushsirikiano kati ya wafanyabiashara wa Zanzibar na wale wa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Akiwa UAE, Rais Dk. Shein alikutana na viongozi mbali mbali wakiwemo wa Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na gesi asilia ya Ras Al Khaimah “Rak Gas”, Kampuni ya RAKEZ, Kampuni ya Mji wa Bahari wa Ras Al Khaiman, Mamlaka ya Uendelezaji Utalii ya Ras Al Khaimah, uongozi wa Taasisi ya Sera na Utafiti ya Kiongozi wa Ras Al Khaiman.
Kiongozi wa Ras Al Khaimah Sheikh Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi alimuandalia Rais Dk. Shein dhifa maalum ya kitaifa ya chakula cha mchana mara baada ya mazungumzo yao huko nyumbani kwake mnamo Septemba 23 pamoja na kumuandalia dhifa maaluma ya kitaifa ya chakula la usiku huko  katika hoteli ya Kimataifa ya “The ritz Carlton” katika jangwa la Wadi ya hifadhi ya asili iliyopo nje kidogo ya mji wa Ras Al Khaimah
Rais Dk. Shein akiwa Ras Al Khaimah atatembelea   maeneo ya mji wa Ras Al Khaiman ikiwa ni pamoja na maeneo mengine ya kitalii katika mji huo na eneo la kiwanda cha Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na gesi asilia ya Ras Al Khaimah.
Aidha, Dk. Shein atakwenda Abu Dhabi kwa ajili ya kushuhudia utiaji wa saini Mkataba wa Mashirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya UAE kupitia Mfuko wa ‘Khalifa Fund’ kwa ajili ya kwuasaidia vijana.
Katika ziara hiyo, Dk. Shein amefuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu, Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib.
Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Said Hassan Said, Balozi Mohamed Haji Hamza Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa upande wa Zanzibar pamoja na watendaji wengine wa Serikali. 
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.