Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Awataka Mawaziri wa SADC Kuyapa Uzito Maazimio ya Mkutano.

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd akipata maelekezo kuhusu mfumo wa matumizi ya simu za mezani kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wakati wa kutembelea mabanda mbalimbali kabla ya kufunga mkutano wa Mawaziri wa sekta za Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wa pili (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Sekta za Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewakutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mara baada ya kufunga mkutano huo leo Ijumaa Septemba 20, 2019.
(Picha na Maelezo Dar.)

Na. Mwandishi Wetu, Maelezo Dar es Salaam. 
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewataka Mawaziri wa Sekta za TEHAMA, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuyapa uzito maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wao kuleta ustawi wa Maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Ukanda huo.
Akifunga Mkutano wa Mawaziri wa SADC wa sekta za TEHAMA, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa leo Ijumaa (Septemba 20, 2019) Jijini Dar es Salaam, Balozi Seif alisema ajenda na maazimio ya mkutano mkutano huo ni maeneo muhimu yatakayoweza kuharakisha kasi ya ukuaji wa uchumi na biashara kiuchumi katika ukanda wa SADC.
Balozi Idd alisema miongoni mwa maeneo muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambayo kwa sasa ukuaji wake umekuwa ni sehemu muhimu katika maendeleo ya kiuchumi ndani ya Jumuiya hiyo ikienda sambamba Mpango Mkakati Wa Maendeleo wa ya Miundombinu ya Kikanda jumuiya hiyo wa mwaka 2019-2023.
Aidha Balozi alisema malengo ya Tanzania ni kuhakikisha Jumuiya hiyo inakuwa na mshikamano na nguvu ya pamoja katika kuondoa na kukabiliana na vikwazo mbalimbali vinavyosababisha ukuaji hafifu wa maendeleo ya kiuchumi katika SADC vikwazo vya biashara ya mipakani vilivyopo baina ya Nchi na Nchi ndani ya Jumuiya hiyo.
“Mkutano huu umekuwa muhimu kwa ustawi wa Jumuiya ya SADC, wananchi wa mataifa yetu wanatarajia kupata unafuu na kutengeneza fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo masoko, biashara na ajira na kwa kufanya hivi tutatekeleza Mipango Mikakati tuliyojiwekea katika kuinua uchumi wa mataifa yetu ndani ya Jumuiya” alisema Balozi Idd.
Kwa mujibu wa Balozi Seif alisema sekta za TEHAMA, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hali pia zina mchango mkubwa katika kuleta mageuzi ya uzalishaji mali na ufanyaji biashara ndani ya Jumuiya ya SADC na hivyo kuzitaka Nchi wanachama kuweka mkazo katika kubuni mipango madhubuti itakayowahakikishia inakuza na kuimarisha miundombinu iliyopo.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alisema katika Mkutani huo, Mawaziri wa sekta hizo wamekuwa na majadiliano mapana yaliyoweza kujadili kwa kina changamoto mbalimbali zilizopo katika Nchi wananchama wa Jumuiya hiyo na kuweka mipango madhubuti kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Aliitaja moja ya changamoto hiyo kuwa ni pamoja na vikwazo vya ufanyaji biashara katika mipaka baina ya Nchi hizo na kueleza kuwa kwa pamoja wamejipanga kuhakikisha kuwa wananachi wa Mataifa hayo wanakuwa na fursa ya kutembeleana na kuweza kufanya biashara baina yao bila vikwazo vya kisheria na kisera.
“Mkutano huu umekuwa muhimu sana kwa manufaa ya wananchi wetu kwani umeweza kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia wananachi wetu kupata unafuu wa gharama katika mfumo mzima wa ufanyaji biashara uliopo katika jumuiya yetu” alisema Waziri Kamwelwe.
Kamwelwe alisema mkutano huo pia ni sehemu muhimu iliyowapa fursa wajumbe wa kuweka mikakati ya pamoja ya njia bora zitakazowezesha kuzinufaisha Nchi wanachama kuweza kutumia fursa za ukuaji wa teknolojia katika kutengeneza fursa ya ukuaji wa sekta za kijamii na kiuchumi ndani ya jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.