Na Ismail Ngayonga. MAELEZO DAR ES SALAAM 23.9.2019
SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inatekeleza Mkakati maalum unaolenga kuziwezesha Halmashauri kujitegemea kimapato ili kutoa huduma bora zaidi na zenye uhakika kwa wananchi.
Katika kutekeleza Mkakati huu, Wizara ya Fedha na Mipango imetoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatumia kwa ukamilifu fursa za kimapato zilizopo katika maeneo yao na hivyo kuongeza uwezo wa kujitegemea kimapato.
Takwimu zinaonesha kuwa bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa hutegemea ruzuku kwa zaidi ya asilimia 88 kutoka Serikali Kuu katika kuchangia utekelezaji wa bajeti pamoja na kugharamia utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Kwa kuzingatia sababu hizo, Wizara ya Fedha na Mipango imeanzisha utaratibu kwa Halmashauri mbalimbali nchini kufanya mawasilisho ya miradi yao ya kimkakati katika eneo la kujijenga kimapato kwa madhumuni ya kujitegemea na kuboresha utoaji wa huduma.
Msingi wa utaratibu huu unatokana na ukweli kwamba upatikanaji wa mapato ya kutosha na yenye uhakika katika Halmashauri ni nguzo imara katika kuboresha utoaji huduma nzuri na zenye uhakika kwa wananchi.
Akiwasilisha Makadirio ya Hatuba ya Bajeti kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo anasema Ofisi ya Rais TAMISEMI ilianza utaratibu wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika Mwaka wa Fedha 2017/18.
Anasema miradi hiyo inapaswa kuwa na sifa ya kuiwezesha Halmashauri kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuziwezesha kujitegemea kimapato na kupunguza utegemezi wa Ruzuku ya Serikali Kuu.
Anaongeza kuwa hadi Februari, 2019 jumla ya Halmashauri 29 zenye miradi 37 zimekidhi vigezo vya kupatiwa jumla ya Tsh Bilioni 268.84 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati ambapo katika awamu ya kwanza Halmashauri 18 zenye miradi 23 zilikidhi vigezo vya kupatiwa jumla ya Tsh Bilioni 131.46.
“Kati ya Fedha hizo Tsh Bilioni 31.36 zimepokelewa kwenye Halmashauri hizo ambazo zimesaini mikataba ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati zitakazotumika kutekeleza miradi ya ujenzi wa masoko, viwanda, machinjio, vituo vya mabasi na maghala ya kuhifadhia mazao” alisema Jafo.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo anasema katika Awamu ya Pili, Halmashauri nyingine 12 zenye miradi 15 zimekidhi vigezo vya kupatiwa jumla ya Tsh Bilioni 137.37 mwezi Januari, 2019 na kusaini mikataba ya utekelezaji wa miradi hiyo itakayohusisha ujenzi wa masoko ya kisasa, machinjio ya kisasa, vituo vya mabasi, uendelezaji wa ufukwe wa Oysterbay.
Waziri Jafo anasema Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango inaendelea kujenga uwezo kwa Halmashauri kuziwezesha kuibua miradi, kufanya upembuzi yakinifu ili miradi hiyo iweze kukidhi vigezo na kupata fedha na kuitekeleza kwa ufanisi.
Upatikanaji wa mapato ya kutosha na yenye uhakika katika Halmashauri ni nguzo imara katika kutatua changamoto za mapato katika ngazi ya halmashauri ni pamoja na uwezo mdogo wa kubaini na kutumia fursa zilizopo pamoja na usimamizi hafifu katika ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya mapato ambazo zina athari katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Matumizi mazuri na yenye tija ya fursa hizi katika vyanzo vya mapato yataziwezesha Halmashauri kuwa na vyanzo vya uhakika ili kujijengea uwezo wa kujitegemea na hivyo kuiwezesha Serikali Kuu kuongeza nguvu na msukumo katika Halmashauri zenye uhitaji zaidi.
No comments:
Post a Comment