Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ katika mkutano wa utekelezaji  wa  mpango kazi wa Mwaka wa Fedha kwa kipindi cha Julai  2018-Juni 2019 na mpango kazi wa mwaka 2019-2020 uliofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar,[Picha na Ikulu.] 04/09/2019. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed  Shein ameutaka uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kuongoza kwa kufuata sheria, kanuni na Katiba ya nchi ili watekeleze vyema majukumu yao.    

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ ulipowasilisha Taarifa za Utekelezaji wa Mpango Kazi wa mwaka 2018/2019.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kwamba  uteuzi alioufanya kwa viongozi wa Ofisi hiyo hakuangalia uzuri wa mtu ukiwemo wa sura bali ni kwa uaminifu wao, uwezo wao walionao wa kufanya kazi, nidhamu pamoja na taaluma walizonazo.

“Bado nina imani na uongozi huu hivyo nakuhimizeni mtekeleze wajibu wenu kwa kutumia Sheria za Zanzibar, kanuni zilizopo pamoja na Katiba kwani hata mimi natumia nyenzo hizi hizi kutekeleza majukumu yangu”, alisema Dk. Shein.

Aliwaeleza viongozi hao kuwa matatizo yote watakayopambana nayo yatatatuka kirahisi iwapo watafuata sheria zikiwemo sheria za ardhi na kusisitiza kuwa iwapo watafuata sheria hizo hawatopata ugumu katika kutekeleza majukumu yao.

Kuhusu suala zima la ugatuzi, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeamua kuanza na sekta tatu za afya, elimu na kilimo lakini hata hivyo umeanza vizuri na fedha nyingi zimepelekwa katika Halmashauri hivyo, aliutaka uongozi huo kuzisimamia vyema kwani hizo ni fedha za wananchi kwa ajili ya huduma zao.

Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Ofisi hiyo Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kukusanya mapato ya TZS Bilioni 12.032 sawa na asilimia 93.55 ya makadirio jambo ambalo ni mafanikio makubwa.

Aidha, Dk. Shein aliwataka viongozi wa Ofisi hiyo kukiri na kutambua kwamba mwaka huu fedha walizoingiziwa katika Bajeti yao ni za kutosha jambo ambalo limewapelekea kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa jambo ambalo halijawahi kutokea hapo siku za nyuma.  

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza hatua za makusudi zitakazochukuliwa katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika katika hospitali zilizopo visiwani ikiwa ni pamoja na kuwapeleka madaktari wakiwemo wakunga.

Rais Dk. Shein aliupongeza uongozi huo huku akisisitiza haja ya kufanya utafiti juu ya zao la korosho Kusini mwa kisiwa cha Pemba kwani zao hilo linaweza kukubali hasa ikizingatiwa mazingira ya eneo hilo.

Dk. Shein alieleza haja ya kuimarisha mafunzo na kuzitaka Wilaya na Mikoa kuzingatia haja ya kuwafundisha wafanyakazi wao ili waweze kufanya kazi vizuri kwani Ofisi  haiwezi kufanya kazi vizuri iwapo wafanyakazi wake hawana ujuzi.

Rais Dk. Shein alisisitiza faida za kufanya utafiti kwani kuna umuhimu katika kutekeleza majukumu ya kila siku ya Ofisi hiyo na Ofisi nyengine za Serikali.

Aliongeza kuwa Serikali imeanzisha Jiji na yeye kumteua Mkurugenzi wa Jiji la Zanzibar kutokana na vigezo vinavyohitajika kufikiwa hivyo, matumaini yake kuwa kazi ya kuliendeleza na kuliimarisha jiji hilo itafanywa kwa mashirikiano ya pamoja katika kuhakikisha azma hiyo inatekelezeka.

Nae Kaimu Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Salum Maulid Salum alieleza haja ya mashirikiano na kukaa pamoja kati ya taasisi za Serikali katika kutekeleza miradi inayokusudiwa ili kuepuka hasara zisizo za lazima.

Mshauri wa Rais wa Zanzibar Pemba Dk. Maua Abeid Daftari kwa upande wake alitoa pongezi na shukutani kwa Rais kwa kujenga majengo ya Ofisi za Wizara za Serikali Gombani Pemba pamoja na kumpongeza kwa kujengwa kwa makaazi ya Madaktari katika hospitali ya Mkoani jambo ambalo litaimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir akisoma muhtasari wa utekelezaji wa Mpago Kazi wa Ofisi hiyo alisema hali ya usalama katika Wilaya na Shehia imeimarishwa na wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo kwa amani na utulivu.

Alieleza kuwa ahadi alizotoa Rais Dk. Shein za kujenga barabara ya Kinuni kutokea Makondeko zzimetekelezwa na Mkandarasi kwa sasa yupo katika hatua ya uwekaji wa lami wa barabara hiyo ya Kinuni yenye urefu wa kilomita 0.95 na kwamba kazi hiyo itakamilika ndani ya mwezi wa Septemba, 2019.

Alisema barabara ya Mwera Wilayani hadi Fuoni Mambosasa yenye urefu wa kilomita 3.4 Ofisi hiyo imekamilisha hatua za kumpata Mkandarasi na Mkataba wa ujenzi wa barabara hio umeshatumwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa hatua za Kisheria.

Aidha, alieleza kuwa Ofisi hiyo imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Daladala Kijangwani kwa uwekaji wa lami ili kuhamisha Kituo cha Daladala cha Michenzani pia, ujenzi wa barabara ya kuelekea Tume ya Uchaguzi Zanzibar yenye urefu wa kilimoita 1.8 ipo hatua ya uwekaji wa kifusi na itakamilika katika hatua ya lami ifikapo Novemba 2019.

Alieleza kuwa Ofisi imesimamia na kuutekeleza ugatuzi kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wananchi ambapo kwa mwaka 2018/2019 imefanikiwa kukamilisha muundo wa Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Sheria na miongozo kutoka  Serikalini.

Waziri huyo alieleza kuwa Ofisi hiyo ilipokea na kutiliana saini hati za makabidhiano ya ugatuzi kwa majukumu yaliogatuliwa kutoka Wizara ya Elimu, Afya na Kilimo jambo lililoondosha mgongano wa utekelezaji wa shuguli zilizogatuliwa.

Katika kuimarisha taarifa za usajili wa matukio ya Kijamii, Waziri huyo alisema kuwa Ofisi imesimamia zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vipya vya Mzanzibari Mkaazi ambalo lilifanyika katika Shehia zote 388 za Zanzibar.

Alisema kuwa Ofisi hiyo tayari imeshaanza kazi ya kuzisimamia Jumuiya zisizo za Kiserikali (NGOs) kwa kuzisajili zile tu ambazo zina sifa ya kusajiliwa.

Nae Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Radhia Rashid Haroub akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa mwaka 2018/2019 alieleza mafanikio yaliopatikana sambamba na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Ofisi hiyo.

Nao uongozi wa Ofisi hiyo walieleza kuwa tayari wamefanya kazi ya kuwaelimisha na kuwaeleza wananchi umuhimu wa utalii wa ndani na tayari wananchi hao wameanza kuuelewa hasa katika maeneo ya Kaskazini Pemba ikiwemo Wilaya ya Micheweni.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alikutana na uongozi wa Idara Maalum za SMZ ambapo katika maelezo yake aliupongeza uongozi huo kwa kuendelea kuwajenga vijana pamoja na Maofisa kuwa na nidhamu, uadilifu na uzalendo mkubwa zaidi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.