Habari za Punde

Mama Mwanamwema Shein Amewataka Wajasiriamaliu Wanawake Kutumia Taalum Katika Kazi Yao ya Ujasiriamali


Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein akihutubia wakati akilifungua Kongamano la Wajasiriamali Wanawake Zanzibar linalofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu (SUZA) kulia Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Zanzibar.Mhe. Maudline Castico na kushoto Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa.Bi.Thuwaiba Editon Kisasi, ufunguzi huo umefanyika leo.19-10-2019.  

MKE  wa Rais wa Zanzibar, mama Mwanamwema Shein amesema shughuli za ujasiriamali zinahitaji taaluma ili ziweze kufanyika kwa ufanisi na kuleta tija pamoja na kuondokana na changamoto.

Mama Mwanamwema amesema hayo katika ufunguzi wa Kongamano la  Wajasiriamali wanawake wa Mikoa ya Unguja, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein, SUZA - Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema shughuli za ujasiriamali kama ilivyo shughuli nyengine zinahitaji elimu ya nadharia na vitendo ili kumwezesha mjasiriamali kupata tija na kuongeza kipato katika familia,

Alisema kwa kuelewa umuhimu wa shughuli za ujasiriamali kwa wananchi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya saba inayoongozwa na Rais Dk. Shein imeunda Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, wanawake na watoto, pamoja na kaunzisha Mfuko wa Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ili kufanikisha azma hiyo.

Alieleza kuwa Serikali imeandaa mipango mbali mbali ya kuwasaidia wananchi ili kuongeza kipato, hivyo akawataka wananchi kuzitumia ipasavyo fursa zilizopo ili kuongeza kipato cha familia.

Aidha, Mama Mwanamwema alipongeza Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), kw uamuzi wa kuandaa kongamano hilo, ambapo pamoja na mambo mengine linazungumzia umuhimu wa kuimarisha Daftari la wapiga kura.

Alisema wakati huu wananchama wa CCM wakiajiandaa kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao mwakani, kuna umuhimu wa kukumbushana haja ya kuimarisha daftari la kudumu la wapiga kura, hivyo akatowa wito kwa kila mmoja kushiriki na kutekeleza wajibu wake wakati utakapofika.

Alisema ili kufanikisha azma ya kuipatia ushindi CCM, ni muhimu kila mmoja kushiriki katika uimarishaji wa daftari hilo, kwa msingi kuwa bila ya kujiandikisha hakutakuwa na fursa ya mtu kupiga kura.

Aliwakumbusha washiriki wa kongamano hilo kuwa CCM ndio chama kinachotegemewa na Watanzania katika kuwaletea maendeleo, kudumisha amani na umoja, kulinda Mapinduzi pamoja na kudumisha Muungano, hivyo kuna kila sababu ya kukiandalia mazingira bora  ya ushindi.

“Tusisahau kuwa sisi akinamama na vijana ndio tulio wengi na tegemeo la Chama chetu kukipatia ushindi wa kishindo, nasaha zangu nyote utakapofika wakati mtekeleze wajibu wenu”, alisema.

Aidha, Mama Mwanamwema aliwataka washiriki na wananchi wote kushrikiana an Serikali katika kuwafichua watu wote wanaojihusisha na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.

Alisema udhalilishaji wa kijinsia pamoja na matumizi ya dawa za kulevya  ni mambo yanayohitaji mikakati mizuri ya  haraka katika kupambana navyo.

Alisema kuna umuhimu wa kuangalia na kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ambapo chanzo chake kinatokana na mmong’onyoko wa maadili katika jamii.

“Naamini mada ya mmong’onyoko wa maadili itakapowasilishwa mtapata kuzungumza kwa kina, na kwa mifano na hatimae kupendekeza mbinu za kuihami jamii yetu”, alisema.

Aidha, alitowa wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa, vyombo vya habari, viongozi wa taasisi za kiraia na Jumuiya zisizo za Kiserikali kuzidi kuwaelimisha wananchi ju ya athari na ubaya wa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Alieleza matumaini yake kuwa kutokana na mafunzo hayo, vita dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukiukwaji wa maadili, vitapata kasi mpya, hivyo akaiomba jamii kushirikiana na Serikali.

Katika hatua nyengine, Mama Mwanamwema aliipongeza UWT kwa maandalizi ya Kongamano hilo, ikiwa ni utekelezaji wa majukumu yake ya msingi.

Aliwapongeza wajasiriamali walioshiriki katika kongamano hilo, kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha azma yake ya kuinua kipato na hali za  wananchi wake.

Aidha, alitoa pongezi za dhati kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa hatua mbali mbali anazozichukuwa katika kuhimiza na kuwasidia wajasiriamali, ikiwa pamoja na kuanzisha mfuko wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi ambao hutoa mikopo nafuu kwao.

“Ni vyema mkautumia mfuko huo kikamilifu katika kujiongezea mitaji kwenye biashara zenu na kukuza maendeleo kwa ujumla”, alisema.

Mama Mwanamwema aliwataka washirki wa kongamano hilo kuwa makini na watulivu katika kipindi chote cha mafunzo ili kufikia malengo yaliokusudiwa, sambamba an kuwapongeza wafadhali mbali mbali waliowezesha kufanyika kongamano hilo.

Nae, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, wanawake na watoto Moudline Castico, alimpongeza Mama Mwanamwema kwa mchango mkubwa anautowa katika kusaidia harakati za ujasiriamali kwa akinamama.

Aidha, Makamo Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thuwayba Edington Kisasi, alisema ni lengo la Jumuiya hiyo kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu ya ujasiriamali nchi nzima.

Aliwataka washirkki wa mkongamano hilo kuitafutia ufumbuzi changamoto ya udhalilishaji wa kijinsia, akibainisha chanzo chake kinatokana na jamii kuondokana na utamaduni, mila na silka za Wazanzibari.

Alitumia furs ahiyo kuwapongeza wafadhali mbali mbali, ikiwemo ZRB, NMB, ZSSF, ZURA, Bima, Chuo Kiku cha Taifa SUZA na wengineo kwa michango yao iliyofanikisha kufanyika kongamano hilo.

Mapema, katika hafla hiyo Mama Mwanamwema aliangalia bidhaa mbali mbali zinazozalishwa na vikundi vya ujasiriamali kutoka Mikoa hiyo ya Unguja.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.