Habari za Punde

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Amewata Walezi Wazazi na Walimu Kuwa na Mashirikiano Kuwajengea Uwezo Wanafunzi Kufanya Vizuri Masomo Yao.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud akizungumza na Wanafunzi wa Kidatu cha nne wa Serikali na Binafsi kuhusu kujiandaa kufanya Mitihani yao huko katika Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Dkt Shein Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Na Mwashungi Tahir       Maelezo   16-10-2019.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud amewataka wazazi, walezi na walimu kuwa na mashirikiano  kuwajengea uwezo wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika kufaulu mitihani yao ya kidato cha nne  ambayo inatarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Rai hiyo imetolewa leo huko katika ukumbi wa Dkt  Ali Mohamed Shein ulioko Tunguu wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa skuli za Serikali na Binafsi kuhusu upatikanaji wa ufaulu katika mitihani yao.
Amesema lengo la mkutano huu ni kuhamasisha wanafunzi wanaojiandaa katika kufanya mitihani ya Taifa ya kidato cha nne inayotarajiwa kufanyika nchini kote ifikapo tarehe 4-11-2019 kupata ufaulu kwa kiwango cha juu katika Mkoa huo.
“Tumeweka kukaa kwa pamoja na wazazi walimu na wazee  kwa kuweza kuwahamasisha wanafunzi washughulikie masomo yao ili upatikane ufaulu mzuri katika Mkoa huu tukitarajia kupatikana division one kwa wingi.”alisema Mkuu wa Mkoa huo.
Aidha  alieleza kwamba Serikali  ya  Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dkt Ali Mohamed Shein imekuwa mstari wa mbele katika  sekta ya elimu ili ufaulu uwe mzuri ikiwa ni ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Pia amesema ili kukuza kiwango cha elimu nchini Serikali imejitahidi kujenga skuli na kuongeza madarasa, kuweka madeski na kutoa vitabu na mabuku  kwa dhamira ya watoto kusoma kwa bidii ili waweze kupata mstakbali mzuri wa maisha yao ya hapo baadae na kupata wataalamu kwalio bora nchini.
Ayoub ameahidi kwa kila mwanafunzi ataepata division one katika Mkoa wa Kusini Unguja atamzawadia zawadi ya vifaa vyote vya kusomea pamoja na uniform ikiwa ni kuwahamasisha wanafunzi kujitahidi kupata ufaulu kwa kiwango cha juu.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kati Hamida Mussa Khamis amewataka wanafunzi kuzidisha bidii katika masomo masomo yao ili upatikane ufaulu mkubwa mwaka huu katika Mkoa huo .
Amesema kamati za skuli zimejipanga vizuri katika kuwasaidia kutoa michango  ili kuhakikisha wanafunzi wanaweza kufaulu vizuri katika masomo yao.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Kusini Unguja  Suleiman Mzee Suleiman akizungumza kwa niaba ya  Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa huo amesema ili wapatikane viongozi walio bora  lazima wapatikane viongozi wenye elimu ili Taifa liwe na maendeleo.
Hivyo amewataka wanafunzi hao kujikurubisha kwenye kutafuta elimu zaidi na mambo mengine yatakuja hapo baadae.
Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja Hamida Mussa Khamis akielezea kuhusu Wilaya yake ilivojipanga kuwasaidia wanafunzi wa Kidatu cha nne wanaotarajiwa kufanya Mitihani yao huko katika Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Dkt.Shein Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.  
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu Mkoa wa Kusini Unguja Hassan Makame Haji akielezea kuhusu kuzidisha mashirikiano ya elimu  katika Mkutano wa Wanafunzi wa Kidatu cha nne wa Serikali na Binafsi huko Ukumbi wa Dkt.Shein Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja. 
 Baadhi ya Wanafunzi wa Kidatu cha nne wa Serikali na Binafsi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa nasaha katika Mkutano uliofanyika huko Ukumbi wa Dkt Shein Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.