Habari za Punde

TRA: Atakayefichua Wakwepa Kodi Atalipwa Asilimia 3 ya Kodi Itakayokombolewa.


Na Veronica Kazimoto. Simiyu
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Diana 
Masalla amesema kuwa, mwananchi yeyote atakayefichua wakwepa kodi na TRA ikafuatilia 
na hatimaye kodi hiyo ikagundulika ni kweli ilikuwa imekwepwa na ikakusanywa, 
mwananchi aliyetoa taarifa hizo za ukwepaji kodi atalipwa asimilia 3 ya kodi iliyokusanywa 
lakini haitazidi shilingi milioni 20.
Masalla ameyasema hayo wakati wa Jukwaa la Biashara na Uchumi lililofanyika katika 
Wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambalo lengo lake ni kujadili fursa, changamoto na kero 
mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji wilayani humo na kuzitafutia 
ufumbuzi.
“Natoa wito kwa wananchi na washiriki wa jukwaa hili kuhakikisha mnawafichua wakwepa 
kodi wote kwa sababu watu hao wanaiibia Serikali yetu mapato na wanarudisha nyumba 
jitihada za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wake,” Amesema Masalla.
Aidha, Masalla amewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki jukwaa hilo 
kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa pindi wanapokuwa wamefunga biashara kutokana na 
sababu mbalimbali ili kuepuka kuendelea kutozwa kodi au kuonekana wamekaidi kulipa 
kodi.
“Ni muhimu kutoa taarifa TRA pale ambapo mfanyabiashara amefunga biashara yake lakini 
pale anapofungua ni muhimu pia kuitaarifu TRA ili kuepuka kuendelea kutozwa kodi 
unapofunga biashara na pia kuanza kutozwa kodi sahihi pale unapofungua biashara,” 
amesisitiza Masalla.
Naye, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Wilaya ya Busega David Mateko amempongeza 
Meneja wa TRA Mkoa wa Simuyu kwa kutoa elimu ya kodi kwa makundi mbalimbali ya 
wafanyabiashara mkoani humo pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuwahamasisha 
wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na hatimaye kuifanya Wilaya ya Busega kuwa wilaya 
ya pili kati ya wilaya 5 za mkoani Simiyu kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali 
yanayosimamiwa na TRA.
“Nampongeza Meneja wa TRA katika Mkoa wetu wa Simiyu kwa kuwatembelea 
wafanyabiashara na kuwapatia elimu ya kodi na pia nachukua fursa hii kumpongeza Mkuu 
wetu wa Wilaya Mheshimiwa Tano Mwera kwa kutuhamasisha kulipa kodi kwa wakati na 
sasa wilaya yetu imekuwa ya pili hapa mkoani kwa ukusanyaji Mapato yanayosimamiwa na 
TRA,” alibainisha Mateko.

Jukwaa hili la biashara na uchumi wilayani Busega limewakutanisha wafanyabiashara na 

wawekazaji zaidi ya 200 ambapo taasisi mbalimbali za Serikali zimealikwa kutoa mada 

ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.