Habari za Punde

Balozi Seif Afanya Ziara Wilaya ya Kaskazini "B" Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwatembelea Watoto Yatima na Walezi wao kwenye zoezi la usajili wa Watoto hao katika Wilaya ya Kaskazini B linalofanyika katika Tawi la CCM Kitope B.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif akishiriki Kazi za Ujenzi wa Taifa katika katika Tawi la Chama cha Mapinduzi Kipandoni Jimbo la Kiwengwa Mkoa Kaskazini Unguja
Balozi Seif akiukabidhi Uongozi wa Tawi la CCM Kipandoni mchango wa Saruji iliyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Kiwengwa Mh. Asha Abdullah. 
Balozi Seif akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa Kaskazini Unguja, Viongozi wa Serikali na Wakuu wa Kamati za Ulinzi za Wilaya za Mkoa huo katika Mkutano wa Majumuisho kufutia aliyoifanya Mkoani humo hapo Ukumbi wa Mikutano wa CCM Mkoa Mahonda.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa Kaskazini Unguja, Viongozi wa Serikali na Wakuu wa Kamati ya Ulinzi ya Wilaya za Mkoa huo wakiwa katika Mkutano wa Majumuisho kufutia Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyoifanya Mkoani humo.
Na.Othman Khamis OMPR.                                                                                              
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema nguvu ya Chama cha Mapinduzi itaimarika mara dufu iwapo Wanachama wake watabeba juk
umu la kushawishi Vijana wenye nia na Uzalendo wajiunge na Chama hicho ili kiendelee kushika Dola muda wote.
Alisema Viongozi wa Ngazi mbali mbali wa Chama hicho kuanzia Shina, Tawi, Jimbo, Wilaya hadi Mkoa wanapaswa kusimamia kazi hiyo inayohitaji muda mwingi wa kujitolea lakini faida yake huweza kunufaisha jamii nzima ya Watanzania.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wanachama, Viongozi na Wananchi wa Kijiji cha Kipandoni mara baada ya kushiriki Kazi ya Ujenzi wa Taifa wa Tawi la Kijiji hicho akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za Chama pamoja na kuelewa changamoto zinazowakabili ili kuzitafutia mbinu za utatuzi.
Alisema Chama cha Mapinduzi kinaendelea kukubalika na Watanzania walio wengi Mjini na Vijijini kutokana na jitihada kubwa zinazochukuliwa na Viongozi wake katika kuwaletea Maendeleo na Ustawi wao kupitia Utekeleza wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020.
Balozi Seif  aliwapongeza Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Kipandoni kwa uzalendo wao uliopelekea kujenga Jengo la Kudumu la Ofisi yao inayotarajiwa kulingana na hadhi ya Chama chenyewe.
Alisema lengo la Ujenzi wa Majengo ya Kisasa ya Chama hicho kama ilivyosisitizwa katika Kanuni za Chama hicho utawapa fursa Wanachama hao kukutana au wakati mwengine kuendesha Vikao vyao katika mazingira safi na salama.
Balozi Seif alifahamisha kwamba wakati wa kuendesha Vikao na Mikutano ya Wanachama chini ya Miti au Majengo Mabovu umepitwa na muda kutokana na mabadilio makubwa yaliyopo ya mfumo wa Sayansi na Teknolojia ambao CCM yenyewe imejikita kwenda nao.
Katika kuunga mkono jitihada za Viongozi na Wanachama hao wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Kipandoni Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif aliahidi kuchangia Saruji Paketi 25 pamoja na Rangi kwa ajili ya kukamilisha Ujenzi wa Jengo hilo la Chama.
Akitoa Taarifa ya Ujenzi huo Katibu wa Tawi la Kipandoni Nd. Jadi Mtumwa Jadi alisema Tawi hilo likiwa niongoni mwa Matawi 14 yaliyomo ndani ya Jimbo la Kiwengwa limeanza Ujenzi wake Mnamo Tarehe 28 Juni Mwaka 2009.
Nd. Jadi alisema Tawi hilo lenye Wanachama 150 kukamilika kwake linatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Milioni 9.3 ambapo hadi sasa zimeshatumika gharama zaidi ya shilingi Milioni 7.7 zikiwemo nguvu za Wanachama wenyewe.
Akitoa salamu za Chama cha Mapinduzi Mkoa wa KaskaziniUnguja kwenye Kikao cha majumuisho ya ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Nd. Iddi Ali Ame ameiomba Serikali itoe adhabu kali kulingana na uzito wa makosa ya udhalilishaji yanayoonekana kuongezeka kila kukicha.
Nd. Iddi alisema katika kupunguza makosa hayo umefika wakati sasa kuundwa kwa Mahakama Maalum itakayosikiliza kesi zinazowahusu Wadhalilishaji wote   wa vitendo vinavyowakosesha raha Wananchi hasa wale wanaofanyiwa vitendo hivyo.
Naye kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kaskazini “B” ambae pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Nd. Rajab Ali Rajab alisema Halmashauri ya Wilaya kamwe haitasita kuzitumia Fedha za Mfuko wa Jimbo zinazotolewa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano kwa ajili ya Maendeleo ya Wananchi.
Nd. Rajab alisema wapo baadhi ya Wabunge ambao ndio Wenyeviti wa kuratibu matumizi ya Fedha hizo lakini hushindwa kuhudhuria Vikao vya kupanga mikakati ya Miradi ya Wananchi jambo ambalo Serikali ya Wilaya haitakuwa tayari kulivumilia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.