Habari za Punde

TAASISI YA MOI YAOKOA TSH 38.4 ZA KUTIBIA WAGONJWA WAGONJWA NJE YA NCHI


Na Mwandishi Wetu,MAELEZO DAR ES SALAAM 22.11.2019
TAASISI ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano imeokoa kiasi cha Tsh. Bilioni 38.4 zilizotakiwa kutumika kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa 43,200 nje ya nchi kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya upasuaji wa kibingwa.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa (Novemba 22, 2019) Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Dkt Respicious Boniface na kuongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, Taasisi hiyo imeendelea kuimarisha na kuboresha huduma mbalimbali za afya kwa wananchi.
Dkt. Respicious anasema kutokana na maboresho na kuimarika kwa huduma ya afya, Taasisi ya MOI ndani ya kipindi cha miaka minne imeweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 43,200  waliofanyiwa upasuaji wa kibingwa na hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi na pesa za Serikali ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu.
‘Gharama za matibabu za wagonjwa hao kwa ndani ya nchi zilikuwa Tsh Bilioni 16.5 na kama wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu, jumla ya Tsh Bilioni 54.9 zingetumika, na hivyo kuifanya taasisi kuokoa kiasi cha Tsh Bilioni 38.4 ambazo zitatumika kwa shughuli nyingine za maendeleo’’.
Aliongeza kuwa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne iliyopita imeweza kupokea kiasi cha Tsh. Bilioni 16.5 kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo jengo jipya la MOI pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa ambavyo vimeweza kuleta mageuzi na maboresho ya huduma za afya katika Taasisi hiyo.
Akitolea mfano, Dkt. Respicious anasema  katika fedha hizo zilizotolewa na Serikali, taasisi hiyo iliweza kuongeza idadi ya vitanda kutoka 150 hadi 350 kwa wagonjwa wa kawaida, na kufanya kutowepo na mgongjwa anayelala chini kwa sasa, sambamba na kuongeza idadi ya vitanda kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum kutoka vitanda 8 hadi 18.
Aidha Dkt. Respicious anasema kuwa pia katika fedha hizo, Taasisi hiyo imeweza kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka vyumba 6 hadi 9, kuongeza vyumba 32 vya wagonjwa binafsi vya daraja la juu pamoja na kuongeza chumba cha upasuaji kwa mgonjwa bila kulazimika kulala hospitali.
Kuhusu vifaa Dkt. Respicious anasema, katika fedha hizo, pia Taasisi ya MOI iliweza kununua mashine mpya za kutolea dawa za usingizi, mashine za kisasa za Radiolagia zikiwemo MRI, CT-Scan, Digital X-Ray, CR X-ray, Portable X-ray, Ultra Sound 2, ECHO na ECG, ununuzi wa mashine mbili mpya za kisasa za vipimo vya maabara.
Akifafanua zaidi, Dkt. Respicious anasema kutokana na maboresho hayo, Taasisi hiyo ndani ya kipindi cha miaka mine imeweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 43,200 waliofanyiwa upasuaji wa kibingwa na hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi na pesa za Serikali ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu.
‘Mbinu hii imesaidia kuongeza idadi ya wagonjwa wa upasuaji kutoka 400-500 kwa mwezi hadi kufikia 700-900 kwa mwezi, na idadi ya wagonjwa hao waliofanyiwa upasuaji wa kibingwa ni pamoja na kubadilisha nyonga (900), kubadilisha magoti (870), upasuaji wa mfupa wa kiuno (618), watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi (2,070)’’ alisema Dkt. Respicious.
Aidha Dkt. Respicious anasema Taasisi ya MOI pia imeanzisha huduma mpya ikiwemo huduma ya upasuaji wa magoti/mabega kwa njia ya matundu ambapo hadi sasa wagonjwa 800 wamefanyiwa upasuaji pamoja na huduma ya upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo ambapo wagonjwa watano pia wamefanyiwa upasuaji huo.
Anaitaja huduma nyingine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa wodi maalum ya kulazwa na kufanyiwa upasuaji siku hiyo hiyo, ambapo wagonjwa 355 wamefanyiwa upasuaji na kufanya upasuaji wa uti wa mgongo kwa kupitia tundu dogo, ambapo hadi sasa wagonjwa 120 wamefanyiwa upasuaji.
‘Huduma hizi mpya, zimeiwezesha Taasisi kupunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa nje ya nchi, ambapo kwa sasa kwa magonjwa ya Neurosurgies asilimia 95 tunafanya hapa na upasuaji wa mifupa asilimia 98 tunafanya hapa pia’’ alisema Dkt. Respicious
Kuhusu huduma ya tiba mtandao, Taasisi hiyo kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imejenga chumba maalum ambapo madaktari katika sehemu mbalimbali za nchi watatuma picha za X-ray/CT-Scan zitakazosomwa na madaktari bingwa wa radiolojia na majibu yatarudishwa kwa daktari aliyeomba kwa muda mfupi.
Aidha katika katika eneo la mafunzo, Dkt. Respicious anasema katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli, jumla ya madaktari bingwa 50 wa mifupa wamehitimu mafunzo, ukilinganisha na madaktari 7 waliohimtimu katika kipindi cha miaka mine iliyotangulia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.