Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Kigwangalla akiwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro (Uhuru Peak) katika kampeni ya kutangaza utalii mlima Kilimanjaro.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Kigwangalla akipanda mlima Kilimanjaro akiwa ameambatana na kunndi la wasanii na wadau mbalimbbali kwa lengo la kuutangaza mlima Kilimanjaro hivi karibuni.
Na.Aron Msigwa – WMU.
Waziri wa Malisili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema ataongoza kampeni ya kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika ukanda wa kusini na ukanda wa Kaskazini magharibi kwenye hifadhi mpya za Taifa zilizotangazwa hivi karibuni.
Amesema kampeni hiyo itawahusisha wasanii na watu maarufu wenye ushawishi katika jamii na inalenga kuhamasisha utalii wa ndani na kutangaza vivutio vya utalii vilivyo katika hifadhi za Taifa za Ruaha,Mikumi, Nyerere na Burigi – Chato.
Dkt.Kigwangalla ameyasema hayo alipokuwa akizugumza na Menejimenti ya Shirika la hifadhi za Taifa nchini (TANAPA) na wakuu wa Kanda wa shirika hilo jijini Arusha.
Amesema hatua hiyo ya kuwatumia wasanii na watu maarufu wenye ushawishi katika jamii inalenga kuogeza hamasa kwa watanzania wavijue na kuvitembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi hizo hivyo kuogeza idadi ya watalii wa ndani.
Dkt.Kigwangalla amesema wasanii hao na watu maarufu wana wafuasi wengi wanaofuatilia kazi zao na matukio wanayofanya katika jamii kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii hivyo ni vyema wakatumika kutangaza utalii katika maeneo hayo.
Amesema hatua kazi hii ya kuhamasisha utalii wa ndani ni vyema wadau na watumishi walio kweye sekta husika wakawa wa kwanza kuvijua vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo mbalimbali ili iwe rahisi kuvielezea na kuvitagaza.
“Tukitaka kutagaza soko la utalii wa ndani lazima sisi wenyewe tuanze kwanza kuyajua maeneo ya vivutio tuliyonayo ili iwe rahisi kuwafikia watu wengine, tuna marafiki zetu ndani na nje ya Tanzania inakua rahisi kwetu kuwaalika na kuwakaribisha kwenye vivutio hivyo kwa kuwa sisi wenyewe tunavijua” Amesisitiza Dkt.Kigwangalla.
Amesema mkakati wa sasa ni wa kusambaza uelewa kuhusu vivutio vilivyopo ndani ya nchi ili kuwahamasisha watanzania wengi zaidi kutembelea vivutio hivyo akibainisha kwamba mkakati huo utakuwa na matokeo ya haraka na gharama nafuu ya kuhamasisha utalii wa ndani katika maeneo mengine ya nchi tofauti na ilivyo sasa ambapo watu wengi wanayafahamu maeneo machache na hasa yaliyo mikoa ya Kaskazini.
“Nilipoamua kuutangaza mlima Kilimanjaro na mimi mwenyewe kushiriki kupanda mlima kila mtu alishuhudia nini kilichotokea, kila mtu alikua akiuzungumzia mlima na hii inaongeza umaarufu wa mlima ndani ya nchi huu ni mkakati tunaotakiwa kuutumia katika maeneo mengine” Amesema.
Dkt. Kigwangalla ameiagiza TANAPA iendelee kukusanya takwimu za makundi mbalimbali ya watalii wa ndani wanafanya utalii katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo watazania wanaoshiriki mbio za marathon.
Katika hatua nyingine Waziri wa Maliasili na Utalii ameiagiza TANAPA kuifanyia kazi na kuikamilisha miradi ya ujenzi wa magati na ununuzi wa vivuko na Boti zitakazokuwa zikitumika kusafirisha watalii katika ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi kwenye eneo la Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Amesema gati hizo zitajengwa Dar es salaam, Saadani, Pangani, Pangani na Tanga ili kuwezesha boti hizo kusimama katika maeneo hayo yenye vivutio vya utalii na kushusha watalii wanaotaka kutembelea maeneo hayo.
“Hili ni eneo muhimu sana kwetu na rahisi kuuza huduma zetu za utalii wa ndani ya maji kutokana na uwepo wa visiwa na idadi ya watu wanaokwenda kuvitembelea, Ni lazima tujipange kuzitumia fursa hizi kwa kuwa na boti nzuri zitakazowawezesha watu kufanya utalii, mikutano, harusi na sherehe mbalimbali ndai ya maji na hii itakua ni Biashara kubwa kwetu na njia moja nzuri ya kulitumia vizuri eneo la bahari tulilo nalo” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Amesema ili kuitangaza hifadhi ya Taifa ya Saadani ni lazima kuiunganisha na utalii wa fukwe ili kuwavutia watalii wengi zaidi na kuongeza kuwa hifadhi hiyo kutokana na maeneo mazuri yaliyopo,sehemu za kulala na ukaribu wake na Bagamoyo na Dar es salaam.
Dkt. Kigwangalla amefafanua kuwa uanzishaji safari za boti za siku kutokea Dar es Salaam kwenda Bagamoyo na kurudi Dar es salaam utawawezesha watalii kwenda kati katika maeneo hayo kwa haraka na ni rahisi kuuza huduma hiyo kwa wageni watakaokuwa wanakwenda kufanya utalii mwisho wa wiki na kuiwezesha Serikali kupata faida ya kiuchumi kutokana na uwepo wa huduma hizo.
No comments:
Post a Comment