Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Utawala Bora na Kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar leo.16-12-2019.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imefanya
bidii kubwa kuhakikisha misingi ya utawala bora inafuatwa ili kukuza uchumi na
kujenga jamii yenye imani, upendo na mshikamano baina yao, serikali na nchi yao
kwa jumla.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo
katika hotuba yake aliyoitoa huko katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakili,
Kikwajuni mjini Zanzibar katika maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za
Binaadamu.
Katika hotuba hiyo, Rais
Dk. Shein aliitaja misingi hiyo kuwa ni ushirikishwaji wa umma, utawala wa
sheria, haki na usawa kwa watu wote,uwazi katika kuendesha shughuli za
maendeleo pamoja na uwajibikaji katika utendaji na uadilifu.
Rais Dk. Shein alieleza
hatua mbali mbali zilizochukuliwa na Serikali kuona kwamba utawala bora
unaimarika ikiwa ni pamoja na kupitisha Sera ya Utawala bora ya mwaka 2011,
ambayo utekelezaji wake unasaidia katika kuyafikia malengo ya mkataba wa haki
za binaadamu na ule wa mapambano dhidi ya rushwa.
Alieleza kuwa Tanzania
ni nchi ya mwanzo kuanzisha Wizara ya Utawala Bora katika nchi za Bara la
Afrika hatua ambayo imeijengea sifa kubwa ndani na nje ya Afrika.
Alieleza kuwa katika
msingi wa ushirikishwaji wa umma, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia
Wizara ya Nchi,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ imeanisha
mfumo wa Ugatuzi kwa kuzingatia umuhimu wa utekelezaji wa Sheria Namba 7 ya
mwaka 2014 ili kukasimu baadhi ya
madaraka kwa wananchi.
Kwa madhumuni ya
kuzilinda haki za watoto, Rais Dk. Shein alisema kwamba Serikali imewajengea
watoto mazingira mazuri ya kutoa ushahidi kwa kuanzisha Mahakama za Watoto
katika Mikoa yote mitano ya Zanzibar.
Alisema kwamba kuweko
kwa utekelezaji wa haki sawa kwa kila binaadamu na utawala bora wa sheria ni
miongoni mwa misingi ya utawala bora kwani mambo matatu haya ambayo ni maadili,
haki za binaadamu na Utawala Bora yana uhusiano unaotegemeana.
Alisema kwamba
harakati za usimamizi na ulinzi wa haki za binaadamu hapa Zanzibar zilianza
zamani kabla ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambapom katika hatua
hiyo Rais wa Mwanzo wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume mara tu baada
ya Mapinduzi alipiga marufuku utaratibu wa mikopo ya fedha kwa njia ya kuweka
vitu rahani (pawn).
Aliongeza kuwa katika
kuhakikisha haki na usawa vinatekelezwa kwa wote, Serikali imeanzisha Tume ya
Utumishi Serikalini katika jitihada za kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa,
utendaji wa kazi unafanywa na vitendo vya unyanyasaji vinaondoka sehemu za
kazi.
Kadhalika alisema
Serikali imekuwa ikiongeza nafasi za uongozi kwa wanawake na kutolea mfano kuwa
katika Baraza la Wawakilishi la mwaka 2015-2020 la hivi sasa idadi ya wajumbe
wanawake imefika 32 ikilinganishwa na wajumbe 26 wa Baraza la wawakilishi la
mwaka 2010-2015 na lile la 2015-2010 ambalo lilikuwa na wajumbe 20.
Alisema kuwa miongoni
mwa wajumbe hao wanawake wapo watano wanaoongoza Wizara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar pamoja na kuwepo kwa nafasi za Makatibu Wakuu, Makatibu Watendaji na
Wakurugenzi.
Aidha, alisema kuwa
Serikali imeweka chombo chake kikuu ambacho kila mwaka huwa kinafanya uhakiki
wa fedha za umma zilizotumika ili kubaini jinsi zilivyotumika kufuatana na
sheria zilizowekwa pamoja na mipango ya maendeleo iliyopangwa.
Rais Dk. Shein
alieleza kuvutiwa kwake na kauli mbinu ya maadhimisho hayo isemayo “Maadili
katika Utumishi wa Umma ni msingi wa Utawala Bora, Haki za Binaadamu na
Mapambano dhidi ya Rushwa”, na kupongeza Kauli mbiu hiyo.
Rais Dk. Shein alisema
kwamba katika suala zima la uadilifu na uwazi katika kuendesha shughuli za
maendeleo na kuzilinda rasilimali za nchi ikiwemo rasilimali fedha na
kusisitiza haja kwa viongozi kuwatumikia watu.
Katika hotuba yake
hiyo, Rais Dk. Shein aliwasisitiza viongozi kuhakikisha wanawatumikia watu
kwani ndio waliowachagua viongozi hao na kuwataka kusimamia wajibu wao sambamba
na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. “Utawala Bora si nyimbo bali ni
kazi”,alisisitiza Dk. Shein.
Akieleza mafanikio ya
Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA), alisema kwamba Mamlaka hiyo
imefanikiwa kuokoa na kuzirejesha Serikalini jumla ya TZS Milioni 238 ambazo
zilitoweka kwa njia ya ubadhurifu kati ya Januari hadi Oktoba mwaka huu 2019.
Rais Dk. Shein
alieleza jinsi Serikali ilivyounda Tume
ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kwa sheria namba 4 ya mwaka 2015 ambayo ni
Taasisi inayojitegemea ambayo ina jukumu la kutekeleza na kusimamia maadili ya
viongozi wa umma hapa Zanzibar.
Hivyo, Rais Dk. Shein
alitoa wito kwa Taasisi zote za umma, za binafsi, asasi za kiraia na wananchi
wote kuziunga mkono jitihada za Serikali katika kushirikiana na Taasisi hiyo
ili hatimae mizizi ya rushwa ing’olewe hapa nchini.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita, Dk.
Amani Abeid Karume kwa kumuamini na kumteua kuwa Waziri wa Mwanzo wa Wizara
inayohusiana na Utawala Bora katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nae Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alitoa
pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa jitihada zake za kuimarisha Utawala Bora akiwa
ni muwasisi wa Wizara hiyo.
Katika hafla hiyo pia,
Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora walimtunuku Rais Dk. Shein, Tunzo
ya Heshima kwa kutambua na kuthamini mchango wake mkubwa katika kusimamia na
kuwa muanzilishi wa Taasisi ya Utawala Bora.
Akitoa neno la
shukurani Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na
Idara Maalum za SMZ, alieleza historia ya Taasisi ya Utawala Bora na kusisitiza
kwamba jamii yote ina jukumu la kusimamia Utawala Bora
Tumbuizo mbali mbali
zilitumbuiza katika maadhimisho hayo, ikiwemo Mchezo wa Kuigiza kutoka kikundi
cha JUFE Film Production kinachoongozwa na msanii maarufu Kachara kutoka
Kaskazini Pemba pamoja na utenzi maalum wenye mnasaba wa shughuli hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
No comments:
Post a Comment