Habari za Punde

Waziri Mwakyembe: Maafisa Michezo lindeni viwanja vya Michezo


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na Maafisa Michezo wa Mikoa na Halmashauri za Tanzania Bara wakati akifungua kikao kazi cha maafisa hao cha siku mbili (tarehe 12-13, Desemba 2019) leo Jijini Dodoma. Kauli mbiu ya kikao kazi hicho ni “Michezo kwa Afya, Ajira na Maendeleo ya Viwanda”
Na. Anitha Jonas – WHUSM, Dodoma.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka Maafisa Michezo kote nchini  kulinda viwanja vya michezo na kutoa taarifa ya viwanja vya michezo vinavyobadilishwa matumizi hata kwa siri.

Waziri Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Michezo kinachofanyiki kwa siku mbili chenye lengo la kutathimini, kujadili na kuelekezana namna bora ya kuimarisha michezo na kutumia sekta hiyo kutangaza vivutio vya utalii nchini.

"Wapo baadhi ya Wakuu wa shule na walimu wanaozuia michezo shuleni na mnawajua, mnakaa kimya sasa wajibu wenu ni nini? Tambueni michezo sasa ni ajira ambayo ni mgodi na taifa lina vijana wengi simamieni vyema michezo,'' Dkt. Mwakyembe.

Akiendelea kuzungumza katika ufunguzi wa kikao kazi hicho Dkt. Mwakyembe amekiagiza Chuo cha Michezo cha Malya kufanya utafiti wa kodi inayotokana na michezo mbalimbali inayofanyika nchini.

Naye Kaimu Katibu Mkuu Dkt. Ally Possi amemwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo kukakikisha kikao kazi hicho kinakuwa endelevu na kufanyika kila mwaka. Aidha, aandae utaratibu wa kuwa na vikao hivyo kikanda vikiwa na lengo la kuwaandaa vijana waweze kushiriki michezo mbalimbali kitaifa na kimataifa.

"Kikao Kazi hiki kitatoa tathimini ya wapi tulipo, nini kifanyike pamoja na kutoa mwongozo wa kusimamia michezo mbalimbali na kutoa maelekezo kwa kuweka maazimio yatakayosaidia kupeleka michezo kuwanufaisha vijana maana michezo ni ajira," alisema Dkt. Possi.

Aidha, Dkt. Possi aliwataka maafisa michezo hao kuzingatia mada ya uandishi wa maandiko ya udhamini katika michezo ambayo ni kichocheo cha kufanikisha michezo nchini kwani maandiko mradi hufanyika ni miongoni mwa kazi inayofanyika kila siku katika sekta ya michezo, hivyo ni  vyema kuwa na ujuzi huo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini Yusuph Singo alitoa pongezi na shukrani kwa Makatibu Tawala Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri kwa kuwawezesha maafisa michezo hao kushiriki kikao hicho kwa mikoa yote nchini imeshiriki.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho Afisa Michezo kutoka Wilaya ya Mbarali Bw. Gerald Chiwaya aliishukuru wizara kwa kuandaa kikao hicho ambacho kimefanyika kwa mara ya kwanza nchini ambacho kina washiriki 265 kutoka mikoa yote Tanzania Bara.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi akitoa maelezo mafupi kuhusu Kikao kazi cha  Maafisa Michezo wa Mikoa na Halmashauri za Tanzania Bara kinachofanyika  kwa  siku mbili (tarehe 12-13,Desemba 2019) leo Jijini Dodoma. Kauli mbiu ya kikao kazi hicho ni “Michezo kwa Afya, Ajira na Maendeleo ya Viwanda”
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph Singo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akitambulisha washiriki wa Kikao kazi cha Maafisa Michezo wa Mikoa na Halmashauri za Tanzania Bara wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho cha siku mbili (tarehe 12-13,Desemba 2019) leo Jijini Dodoma. Kauli mbiu ya kikao kazi hicho ni “Michezo kwa Afya, Ajira na Maendeleo ya Viwanda”
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na  Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Wizara mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Maafisa Michezo  wa Mikoa na Halmashauri za Tanzania Bara cha siku mbili (tarehe 12-13,Desemba 2019) leo Jijini Dodoma. Kauli mbiu ya kikao kazi hicho ni “Michezo kwa Afya, Ajira na Maendeleo ya Viwanda”

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na  baadhi ya Maafisa Michezo  mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Maafisa Michezo wa Mikoa na Halmashauri za Tanzania Bara cha siku mbili (tarehe 12-13 Desemba 2019) leo Jijini Dodoma. Kauli mbiu ya kikao kazi hicho ni “Michezo kwa Afya, Ajira na Maendeleo ya Viwanda”
(Picha na Shamimu Nyaki, WHUSM, Dodoma)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.