MUONEKANO
wa Jengo la Skuli mpya ya Sekondari ya
Rahaleo Wilaya ya Mjini Unguja iliofunguliwa leo na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, kwa niaba ya Skuli
Tisa za Unguja na Pemba, ikiwax ni shamrashamra za Kusherehekea Miaka 56 ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar imepata mafanikio
makubwa katika sekta ya elimu, kutokana na misingi bora iliyowekwa na muasisi
wa Taifa hili, marehemu Abeid Amani Karume.
Dk. Shein amesema hayo katika hafla ya Ufunguzi wa Skuli ya
Sekondari ya Mwembeshauri, ikiwa ni shamra shamra za maadhimiisho ya miaka 56
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema ukombozi uliofanywa na Chama cha ASP chini ya Uongozi
thabiti wa marehemu mzee Abeid Amani Karume mwaka 1964, umeweka misingi bora ya
upatikanaji wa elimu nchini, na kubainisha kuwa itaondelea kutolewa bure katika
awamu zijazo.
Alisema kabla ya Mapinduzi ya 1964, elimu ilitolewa kwa
malipo, hivyo watoto wa wazalendo wa Zanzibar, hususan wanyonge
walishindwa kupata fursa ya kusoma, sambamba na kutolewa kwa misingi
ya ubaguzi kutegemea na kabila la mtu alikotoka.
Alisema kupitia Ilani ya uchaguzi wa ASP, marehemu Abeid Amani
Karume alitangaza elimu kutolewa bure nchini
kote, pale chama hicho kitakaposhinda na kukamata hatamu, jambo ambalo
limeeendelea kutekelezwa hadi leo.
Dk. Shein alisema katika awamu tofauti za Uongozi, Serikali
imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuendeleza sekta ya elimu kwa kuimarisha miundombinu
ya elimu, ikiwemo ujenzi wa skuli hadi kufikia 381 hivi sasa kati yake skuli
284 zikiwa za Sekondari.
Alisema Zanzibar inasifika kwa kuwa na mfumo bora wa utoaji wa
elimu katika ukanda wa Mashariki ya Afrika na Bara lote kwa ujumla.
Alisema ujenzi wa Skuli tisa mpya, utaondoa kabisa tatizo la
mlundikano la wanafunzi katika skuli mbali mbali, akitowa mfano wa baadhi ya
skuli, walimu watatu kufundisha darasa moja
kwa wakati mmoja, kutokana na wingi wa
wanafunzi.
Aidha, alisema Serikali
inaendelea kufanya juhudi kubwa kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali
mbali zinazokwaza maendeleo ya elimu nchini, ikiwemo upatikanaji wa vitabu na
madawati, akibainisha awamu ya pili ya uagizaji madawati 42,135 kutoka nchini
China kwa ajili ya skuli za msingi.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea kukimarisha Chuo Kikuu cha
Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kuongeza vitivo na program mbali mbali za masomo ili
kuhakikisha Taifa linapata wataalamu wengi kupitia nyanja tofauti.
Alisema Serikali imelipa kipaumbele suala la elimu na
kubainisha katika Bajeti ya mwaka huu wa
fedha 2019/2020 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 178.9 kwa ajili ya sekta ya
elimu nchini.
Aidha, alisema changamoto ya upungufu wa walimu wa Sayansi
inafanyiwa kazi ambapo tayari limeanza kupatiwa ufumbuzi kwa msaada wa wahisani
mbali mbali.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein alipingana na mitazamao ya
baadhi ya watu wanaodai elimu imeshuka nchini, akisema haijulikani kipimo gani
kilichotumika kuhusisha ya dhana hiyo,
kwa kuzingatia kuwa hivi sasa Zanzibar imekuwa na Vyuo vikuu kadhaa, wakati ambapo
zamani havikuwepo.
Alisema weledi wa kuzungumza lugha ya Kiingereza sio kigezo
cha kupimwa kiwango cha elimu akibainisha kuwepo nchi kadhaa duniani zilizopiga
hatua kubwa za maendeleo ambapo hutumia lugha zao za Taifa katika kufundishia hadi vyuo vikuu.
Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma
alisema ujenzi wa skuli hiyo ya ghorofa mbili una lengo la kuondokana na ufinyu
wa nafasi, na kubainisha kuwa zitatumika
na wanafunzi wa skuli mbili na kuondokana na kadhia ya mazingira mabaya yaliopo
katika skuli za Darajani na Vikokotoni, ambazo zimezungukwa na shughuli za
kibiashara.
Aisema majengo hayo yatawasaidia sana walimu kufundisha katika
mazingira mazuri na wanafunzi kupokea vyema kile wanachofundishwa, na hivyo
kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufaulu masomo yao.
Alieleza kuwa Wizara imeweka mikakati kabambe ili kuhakikisha
wanafunzi wanaendelea kufanya vyema katika mitihani yao na kueleza kuwa hatua
hiyo imeilanza kuleta mafanikio kwa kupunguza kiwango kikubwa cha wanafunzi
wanaofeli (Divisheni zero).
Waziri Pembe alitoa ombi rasmi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Skuli hiyo ya Mwembeshauri iitwe kwa jina la Dk. Ali Mohamed Shein, lengo
likiwa ni kumuenzi kiongozi huyo kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha
sekta ya elimu nchini.
Mapema, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dk.
Idriss Muslih Hijja alisema Skuli mpya ya Mwembeshauri ni miongoni mwa skuli
tisa zilizokamilika ujenzi wake Unguja na Pemba.
Alisema ujenzi huo umetekelezwa kwa mashirikiano kati ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wahisani Opec Fund for International
Developement (OFID), kupitia mradi wa Zanzibar Third Education Project (ZATEP).
Alieleza kuwa ujenzi wa skuli hizo unaendana na utekelezaji wa
Ilani ya CCM, ukiwa umegharimu jumla ya shilingi Bilioni 26.3, kati ya hizo
shilingi Bilioni 23.4 ni mkopo kutoka OPEC Fund na shilingi Bilioni 2.9 ni
mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha,
alisema ujenzi wa skuli ya Mwembeshauri pekee imegharimu zaidi ya shilingi
Bilioni 3.5, kati ya hizo shilingi Bilioni 3.2 zimetumika kwa shughuli za
ujenzi na zaidi ya shilingi Milioni 361.1 ni gharama za ununuzi wa vifaa
mbalimbali, zikiwemo komputa na vifaa vya maabara.
Alisema skuli hiyo ya ghorofa mbili iliyojengwa na Kampuni ya ‘Group Six International Limited’ kutoka China ina uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 2,560 kupitia mikondo miwili kwa wastani wa wanafunzi 40 kwa darasa.
Katibu Mkuu alisema mradi wa ujenzi wa skuli tisa unalengo la kukuza ubora wa elimu nchini kupitia uimarishaji wa miundombinu na samani na kubainisha hatua hiyo itaongeza nafasi za masomo na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Alisema kwa ujumla skuli hizo (tisa) zina uwezo wa kuandikisha wanafunzi 11,520, watakaopata fursa ya kusoma kupitia mikondo miwili ya masomo.
Alizitaja skuli nyengine zinzohusika na mradi huo, kuwa ni pamoja na Kinuni, Chumbuni , Bububu na Fuoni kwa Unguja na Wara, Mwambe, Kizimbani na Micheweni za Kisiwani Pemba, ambazo nazo zimepewa majina mbali mbali ya Viongozi wa Kitaifa.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment