RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein,
akiondoa kipazia kuashiria kulizindua Mradi wa Maji Safi na Salama na Usafi wa
Mazingira Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja
katika eneo la Saateni Jijini Zanzibar ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 56 ya
Mapinduzi ya Zanzibar, (kulia kwa Rais) Waziri wa Ardhi Nyumba Maji na Nishati.Mhe.Salama Aboud Talib na (kushoto kwa
Rais) Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyuma Maji na Nishati.Ndg. Ali Halil na
Mkurugenzi Mkuu (ZAWA) Ndg. Mussa Ramadhan Haji.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya juhudi kubwa katika
kuendeleza miradi ya maji safi na salama na si muda mrefu changamoto ya
upatikanaji huduma hiyo itakuwa ni historia.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo
katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa
Mkoa wa Mjini Magharibi (ZUWSP)-ADF 12 huko Saateni Wilaya ya Mjini Unguja ikiwa
ni shamrashamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa Awamu ya Saba imeanza mikakati kabambe ya kuimarisha miradi ya maji na
kueleza kuwa Awamu zijazo zitaendeleza mikakati hiyo kwa azma ya kuwapatia
wananchi huduma hiyo muhimu hapa nchini.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa huduma za maji safi na salama kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 zilikuwa
zikitolewa kwa ubaguzi licha ya kuwa ni neema aliyoileta MwenyeziMungu kwa waja
wake.
Alisema kuwa kwa
Zanzibar wakati huo huduma zote muhimu zilianza katika nyumba za mawe
zilizokuwepo katika eneo la MjiMkongwe pekee yake.
Rais Dk. Shein alieleza
umuhimu wa maji kwa wanaadamu, wanyama na miti na kueleza kuwa ndio maana
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikafanya juhudi za makusudi kuhakikisha
huduma hiyo inaimarika hasa ikizingatiwa kuwa maji hayana mbadala.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza jinsi ya Washirika wa Maendeleo wakiwemo nchi rafiki ikiwemo Ras al Khaimah,
Sharja, Japan, China, India na wengineo
walivyoiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maji safi na salama hapa
nchini.
Alisema kuwa Zanzibar
ina historia kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama kwani historia hiyo
inaonesha kuwa zilikuwa zikija meli maalum kuchukua maji kutoka nje ya nchi kutokana na sifa za
maji ya Zanzibar.
Alieleza jinsi ya
ongozeko la watu lilivyochangia uhaba wa maji hapa Zanzibar na kueleza jitihada za Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya
kuimarisha miradi ya maji katika eneo la mji wa Zanzibar na hatimae kupatikana
kwa kiasi cha USD Milioni 268 kwa ajili ya miradi hiyo.
Alieleza kuwa azma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha kiwango cha maji kinaongezeka
kwa kiasi kikubwa ili wananchi wapate huduma hiyo ipasavyo na kusisitiza kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imetekeleza malengo ya
Mapinduzi sambamba na Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Wizara hiyo kwa kuiongoza Wizara hiyo
pamoja na watendaji wengine wote wa Wizara hiyo kwa kushirikiana, “Namie kidogo
nimeubwaga moyo katika kufanikisha mradi huu wa maji”alisema Rais Dk. Shein
katika hotuba yake hiyo.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kueleza historia ya Mapinduzi hapa Zanzibar na jisni
jitihada za akusudi zilivyochukuliwa katika kuhakikisha ukoloni unaondoshwa na
wananchi wa Zanzibar wanaishi maisha bora na wanaodokana na dhulma iliyokuwepo.
Alieleza kuwa Mapinduzi
yaliyofanyika Januari 12, 1964 ni Mapinduzi halali na lengo lake ni kuhakikisha
wananchi wanaishi maisha bora ya amani sambamba na furaha na kushirikiana hatua
ambayo iliwapelekea nchi kadhaa duniani kuyatambua.
Aliwanasihi wananchi
na kueleza kuwa si busara na wala si vizuri wakaunganisha maji katika nyumba
zao bila ya kufuata sheria na utaratibu uliowekwa.
Alisisitiza kuwa
Zanzibar maji hayalipiwi bali yanachangiwa katika kupatikana kwa huduma hiyo
na kuwataka wananchi pale Serikali inapoelekeza kuchagia huduma hiyo basi
wananchi wasirudi nyuma kwani hatua hiyo itaisaidia (ZAWA) kufikisha na
kutengeneza miundombinu ya maji kwani ina lengo na nia nzuri huku akisisitiza
haja ya kutunzwa kwa miundombinu hiyo ya maji.
Aliendelea kusisitiza
haja ya kuzihifadhi na kuvitunza vyanzo vya maji kwani hivi sasa vimekuwa
vikivamiwa kwa kujengwa nyumba katika maeneo hayo likiwemo eneo la Mwanyanya huku
akisisitiza umuhimu wa kupandwa miti na kukemea kukatwa miti ovyo.
Pia, Dk. Shein aliitaka
(ZAWA) kuwa na wataalamu wa maji
kutokana na kuwepo kwa miundombinu mipya ya maji hivi sasa hivyo, ni lazima
wajiandae kuwapa elimu na mafunzo watendaji wake katika vyuo kadhaa vikiwemo
vya nje ya nchi vinavyosomesha kada hiyo.
Aliwataka wafanyakazi
wa (ZAWA) kutofanya kazi kwa mazoea na kusistiza kuwa ni vyema wakawepo watu
wenye utaalamu wa kutosha katika kada hiyo ili kupelekea ufanikishaji wa utoaji wa uhakika wa maji safi
na salama.
Rais Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuwepo kwa hakiba ya vifaa katika Mamlaka ya (ZAWA) ili
kuepuka uhaba wa vifaa pamoja na kuwepo timu kabambe ya kufuatilia matatizo ama
uvujaji wa ovyo na si kutegemea taarifa kutoka kwa wananchi.
Alisisitiza haja ya kuwaajiri
vijana ili wafanye kazi kwani wako wengi hawana kazi ili lengo la kufanikisha
utoaji wa huduma hiyo lifikiwe.
Alitumia fursa hiyo
kumpongeza Mkurugenzi wa (ZAWA) na timu yake kwa hatua inazozichukua hasa
wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuwapelekea maji wananchi katika mwezi
huo mtukufu na kuwataka waendelee na utaratibu huo.
Aliipongeza Serikali
ya Japan kwa kusaidia hatua ya mwanzo ya mradi wa maji katika Mkoa wa Mjini,
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuendelea kutoa msaada wake ikiwemo
pale Serikali inapotaka kukopa, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambao wameanza
kusaidia tokea mwaka 1964 pamoja na Serikali ya India.
Mara baada ya kuwasili
katika eneo la Saateni, Rais Dk. Shein alipata maelezo juu ya mradi wa
maji kwa tangi la Saateni na tangi la
Mnarawambao kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Mussa
Ramadhan Haji.
Nae Waziri wa Wizara
ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Salama Aboud Talib alieleza kuwa hatua hiyo ni
lengo na madhumuni ya Rais Dk. Shein katika kuhakikisha anawaletea maendeleo
wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuwapelekea huduma ya maji safi na salama.
Alisema kuwa jitihada
hiyo ni matokeo ya pamoja kwani kumekuwa na mashirikiano mazuri kati ya Wizara
na Idara zake husika kwa mashirikiano ya Washauri na Waelekezi wa Ujenzi wa
Miradi hiyo pamoja na Mwenyekiti wa Badi ya Wakurugenzi kwa mashirikiano inayotoa
katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika.
Alisema kuwa katika
majaribio yaliofanyika, imeonesha kwamba tatizo la maji lime kupungua na
kupongeza ahadi ya Rais Dk. Shein aliyoitoa kwa wananchi wake juu ya mradi huo
na kusifu dhamira na miongozo yake ambayo ndio imekuwa dira.
Alieleza kuwa kwa
Afrika Mashariki ni nchi ya mwanzo kujenga matangi ya maji ya aina hiyo na
kupongeza jitihada za Rais Dk. Shein kwa kazi hiyo kubwa ya mradi huo iliyofanyika ya kuhakiisha huduma ya maji
inaimarika katika mjiwa Zanzibar.
Aliwapogeza viongozi waliokuwa wakitoa mashirikiano katika
uhakikisha mradi huo unafanikiwa wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi
Hassan Khatib, Masheha wa Mkoa huo ambao wamefanya kazi kubwa kwa kusimamia
miradi hiyo na kupelekea kufanya kazi bila ya bughudha katika kufanikisha mradi
huo.
Sambamba na hayo,
Waziri huyo alikipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kusimamia Ilani ya
chama hicho kwa kuweza kusaidia kufanikisha mradi huo ikiwa ni pamoja na ziara
mbali mbali walizozifanya wakati wa ujenzi wa mradi huo.
Akisoma taarifa ya
kitaalamu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Ali Halil
Mirza aliipongeza Seruiiklai ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais
Dk. Shein kwa uongozi wake mahiri kwa kuamua kutekeleza Mradi wa Maji na Usafi
wa Maziringira wa Mkoa wa Mjaini Magharibi.
Alisema kuwa uwamuzi
huo ulikuwa ni wa busara na wa msingi katika kuodosha kero zinazowakabili
wananchi, unaokwenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM
2015-2020, Mkatkati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA
III), Dira ya Maendeleo ya 2020 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), katika
kuimarisha huduma za maji safi na salama Zanzibar.
Aidha, alisema kuwa
mradi huo utawanufaisha wananchi wapatao 283,198 wa Mjini zikiwemo Shehia
27 za Mji Mkongwe na Ngambo ya zamani ambao umetekelezwa
kwa pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) ulioanza rasmi mwezi Julai 2013 na kukamilika mwezi Disemba 2019.
Shehia hizo ni
Shangani, Mkunazini, Kiponda, Malindi, Mchangani, Vikokotoni, Mwembetanga,
Kisiwandui, Kikwajuni Bondeni, Kikwajuni Juu, Kisima Majongoo, Mlandege,
Mwembeladu, Rahaleo, Mikunguni, Mkele, Mwembeshauri, Shaurimoyo, Mwembe Makumbi,
Kwaalamsha, Gulioni, Miembeni, Kilimani, Kwahani, kwaalinato, Makadara na
Migombani.
Kwa maelezo ya Katibu
Mkuu huyo Mradi huo umesimamiwa na Mshauri Mwelekezi kutoka Kampuni ya Don
Consult Ltd na ujenzi wa matangi na ulazaji wa mabomba umefanywa na Mkandarasi
kutoka Kampuni ya Stcol Corporation ambapo uchimbaji na ukarabarti wa visima
umefanywa na Kampuni ya NSPT Ltd.
Alisema kuwa mradi huo
umejumuisha uchimbaji wa visima 6 vipya vyenye uwezo wa kuzalisha wastani wa
lita 150,000 kwa saa kwakila kisima, ukarabati wa visima vikongwe 23, ujenzi wa
matangi 2 yenye ujazo wa lita milioni 2 Saateni na milioni 1 Mnarawambao.
Pia, unajumuisha
ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 75.7 ambapo kilomita 20.6 ni mabomba
ya usafirishaji maji yenye kipenyo kuanzia inchi 12 hadi 24 yaliyolazwa kutoka
visimani Bubwisudi hadi Welezo matangini na kutoka visimani Karurikikombe hadi
tangi la Mnarawambao.
Mradi huo hadi
kukamilika kwake umegharimu jumla ya TZS Bilioni 37.142 ambapo kwa upande wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa TZS Bilioni 3.809 na Benki ya Maendeleo ya Afrika imetoa TZS Bilioni
33.332 ambapo tangi la Saateni limegharimu jumla ya TZS Bilioni 2.937 na kwa
upande wa tangi la Mnarawambao limegharimu TZS Milioni 908.536.
Katibu Mkuu huyo alisema
kuwa baada ya kukamilika kwa mradi
uzalishaji wa visima 23 vilivyofanyiwa marekebisho umeongezeka kutoka lita
Milioni 32.789 hadi kufikia lita milioni 36.755 sawa na ongezeko la asilimia
12.
Alisema kuwa visima
vipya 6 kwa sasa vinazalisha lita milioni 22.550 hivyo kufanya jumla ya lita
zote hizo kwa siku kuwa ni milioni 59.305 sawa na ongezeko la asilimia 36,
uzalishaji ambao unatarajiwa kuwanufaisha wakaazi wapatao 283,000 ambapo kazi
hiyo ni endelevu.
Alieleza kuwa Serikali
kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba,Maji na Nishati inatarajia kwamba Mradi huo utaendeshwa na kutunzwa
vizuri kwa mshirikiano kati ya Mamlaka ya Maji Zanzibar,Wananchi, Uongozi wa
Majimbo na Ofisi za Wakuu wa Wilaya.
Aliitaja Miradi
mengine iliyobuniwa na inayotegemewa kutekelezwa katika kipindi cha karibuni
ukiwemo Mradi wa Uhuishaji wa Mfumo wa
Usambazaji maji Zanzibar, Mradi wa Uhuishaji wa Huduma za Usambaji Maji Safi wa
Mazingira Miji 26 ya Tanzania ikiwemo Zanzibar na Mradi wa Uimarishaji wa
Miundombinu ya Maji Mkoa wa Mjini Magharibi yenye gharama za Dola za Kimarekani
247.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment