Habari za Punde

CCM Yapelekea Kuimarika Kwa Uchumi wa Taifa

Mama Asha Suleiman Iddi akizungumza na Wanachama wa CCM Mkoa Mjini hapo Viwanja vya Sheikh Thabit Kombo Aman kwenye maadhimisho ya Sherehe za CCM kutimia Miaka 43 Kimkoa.
Na.Othman Khamis.OMPR.                                                                                              Wanachama wa Chama cha Mapinduzi { CCM} lazima wajipongeze kwa kutimiza      Miaka 43 tokea Kuzaliwa kwa Chama hicho mnamo Mwezi Febuari Mwaka 1977    wakiwa na nia safi inayowawezesha kuendelea kuongoza Dola kwa pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.                                              
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema hayo wakati wa kuadhimisha Sherehe za kutimia Miaka 43 ya Chama cha Mapinduzi zilizofanyika katika Uwanja wa Sheikh Thabit Kombo Amani Mkoa Mjini.
Mama Asha alisema Uongozi huo wa Dola unaobeba Lulu ya Amani na Utulivu wa Nchi utadumu kipindi kirefu endapo Wanachama wenyewe pamoja na kuungwa mkono na Wananchi Wazalendo wataendelea kukiamini Chama hicho Kikongwe Barani Afrika.
Alisema yapo mambo mengi yaliyofanya na CCM yaliyopelekea kuimarika kwa Uchumi wa Taifa hasa katika Kipindi cha Miaka Mitano inayomalizika hivi sasa chini ya Usimamizi wa Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein anayetekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa umakini mkubwa.
Mama Asha alitanabahisha kwamba ili kuyaendeleza Maendeleo hayo Wana CCM wenyewe wanapaswa kuwa makini katika kupembua Wanachama sahihi watakaostahiki kubeba Bendera ya CCM kwenye mchakato wa kuwatafuta wagombea kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae Mwaka huu.
Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishauri na kupendekeza kwamba chaguzi hizo za ndani ya Chama lazima ziendelee kuzingatia Heshima, Maadili na uadilifu mambo ambayo yanawezekana ndani ya uwezo wa Wanachama wenyewe katika kumpata Kiongozi makini wa kuisafishia njia safi CCM kwenye ushindi wa ngazi zote.
Akijibu shutma zilizotolewa na baadhi ya Wanasiasa wa Vyama vya Upinzani ambazo alihusishwa nazo Mwakilishi wa Jimbo la Shaurimoyo Mheshimiwa Hamza Hassan Juma kuhusu Hoja Binafsi ya Mgombea kufika Miaka Miwili baada ya kujiunga na Chama Kipya alisema hiyo ni Haki ya Mjumbe ye yote anapoona inafaa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Hamza Hassan alisema akiwa Mjumbe Halali wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Shaurimoyo anajitayarisha kupeleka Hoja Mbili Binafsi kwenye Baraza la Wawakilishi ili zikapate Michango pamoja na Maoni ya Wajumbe wenzake.
Alizitaja Hoja hizo Mbili kuwa ni ile ya Mwanachama Mpya wa Chama lazima afikishe Miaka Miwili ndipo apewe fursa ya kugombea Uongozi ili kuondosha hilba na wababaishaji ndani ya Siasa pamoja na Hoja ya Kura ya Maoni ya kuendelea aukutokuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar {SUK}.
Alisema kufanya hivyo kamwe hajavunja Sheria zote Mbili ile Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar na hiyo itakuwa ni sawa na Hoja ile ile iliyowahi kuwasilishwa na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wa kuipendekeza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo ya sherehe za CCM kutimiza Miaka 43 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Nd. Talib Ali Talib alisema Watu au Chama kinachotaka kushindana na CCM kiko mlango wazi kufanya hivyo.
Nd. Talib alisema Chama cha Mapinduzi kinajiamini wakati wote kwenye ushindani huo kutokana na umamini wa Utekelezaji wa Ilani yake uliopelekea kupatikana kwa Maendeleo makubwa ya kustawisha Maisha ya Wananchi walio wengi hasa wale wanyonge wa Vijijini.
Aliwakumbusha Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM kwamba wao ndio wadhamini wa Chama hicho katika kuusimamia utendaji wa Serikali zote Mbili na lile lenye maslahi ya umma wasisite kulipeleka kwenye Vikao vyao.
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa Mjini aliwataka Wanachama na Wananchi wote wajitokeze kujihakiki na kwa wale Wapya kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakati utakapowadia.
Hata hivyo Nd. Talib alitanabahisha wazi kwamba yule asiyetimiza muda wa Miezi 36 kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi katika Jimbo Jipya analoishi asisogee kabisa kwenye uandikishi huo na kurejea alikotoka na Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi hautosita kulipigania hilo kwa nguvu zake zote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.