Habari za Punde

Uwekaji wa Jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi wa Jengo Kipya la Mahakama Kuu Zanzibar Tunguu Mkoa wa Kusini Wilaya ya Kati Unguja.


 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akiweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Mahakama Kuu ya Zanzibar, linalojengwa katika eneo la Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja hafla hiyo imefanyika leo 10-2-2020

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikishughulikia sana suala la kuwandalia wafanyakazi wake mazingira mazuri na yaliyo salama ya kufanya kazi ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi na bila ya usumbufu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mahkama Kuu mpya, inayojengwa huko Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja ambapo hafla hiyo ni miongoni mwa shamra shamra za wiki ya Sheria hapa nchini.

Katika hotuba yake Rais Dk. Shein alisema kuwa ndio maana majengo kadhaa ya baadhi ya Taasisi za Serikali yaliyokuwa na ufinyu wa nafasi au uchakavu mkubwa yamefanyiwa matengenezo na mengine kujengwa upya katika uongozi wa Awamu zilizopita na Awamu hii ya Saba.

Aliongeza kuwa uwamuzi uliochukuliwa wa kujenga jengo jipya la Mahkama Kuu huko Tunguu umezingatia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuimarisha mazingira bora na salama ya  kufanyia kazi kutokana na ukweli kwamba jengo la Mahkama Kuu ya Vuga halikidhi haja.

Alisema kuwa hapo siku za nyuma lilikuwa linatosha kwa kutoa huduma kwa wakati huo wa karne iliyopita kulingana na mahitaji, mazingira na teknolojia iliyopo ambapo hivi sasa shughuli zimekua zikiongezeka.

Rais Dk. Shein  alisema kuwa jengo la Mahkama Kuu ya Vuga lililojengwa miaka mia moja iliyopita lilikidhi haja ya shughuli zake zilizokusudiwa kwa siku za nyuma kwa sababu wakati huo idadi ya watu wote wa Zanzibar ilikuwa ndogo na kwa mujibu wa Sensa zilizofanyika katika miaka tofauti hapa Zanzibar zinaonesha kwamba idadi ya watu imekuwa ikiongezeka.

“Kwa upande wa Sekta ya Sheria, Serikali imefanyia matengenezo makubwa majengo yetu ya mahkama, pamoja na kuimarisha miundombinu ya Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, ili pawe na mazingira mazuri ya kutolea huduma kwa wananchi” alisema Dk. Shein.Rais Dk. Shein alieleza kwamba katika eneo hilo la Tunguu, mbali ya kujenga jengo jipya la Mahkama Kuu vile vile, Serikali itajenga Skuli ya Sheria (Law School)  na kuitaka Wizara husika kuhakikisha ujenzi huo unafanywa hatua kwa hatua katika Bajeti ijayo ya mwaka 2020-2021.

Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kurejea kauli yake ya kuwataka maofisa wa ununuzi na uwagizishaji katika taasisi za Serikali kuwa wakweli, weledi, wawazi na waaminifu na wasifanye mizengwe katika shughuli zao za kazi sambamba na  kufuata sheria za manunuzi.

Aliwataka watendaji hao kutofanya yale ambayo yaliwahi kusikika ambayo yamepelekea kuzorotesha miradi kadhaa na kuwaeleza kuwa Serikali haitosita kuwachukulia hatua za kisheria pale watakapogundulika kufanya hivyo.

Hivyo, Rais Dk. Shein aliwataka watendaji hao kuwa waadilifu kwani Serikali imewapa dhamana hivyo ni vyema wakazitumikia dhamana walizopewa ipasavyo.

Sambamba na hayo, rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imelazimika kuimarisha sekta ya sheria na imeunda Wizara Maalum ya Katiba na Sheria kwa lengo la kuimarisha sekta ya sheria na muhimili wa Mahkama.

Alieleza kuwa tangu mwaka 2010, Serikali imeuimarisha utendaji wa kazi wa mahkama katika Nyanja mbali mbali kama vile kuzipatia mahkama hizo vitendea kazi, kuongeza majaji, mahakimu, makadhi pamoja na kufanyia mapitio sheria mbali mbali ambapo pia, sheria 92 zimetungwa hadi Januari 2020.

Rais Dk. Shein pia, alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha vitendo vya udhalilishaji wa Wanawake na Watoto vinafanyiwa kazi ipasavyo.

Pamoja na hayo, rais Dk. Shein alieleza uwamuzi wa kuufanya mji mpya wa Tunguu kuwa ni Makao Makuu ya Muhimili wa Mahkama ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mipango Miji na kuuimarisha Mji huo.

Rais Dk. Shein alieleza matarajio yake juu ya ujenzi huo na kusema kuwa Serikali itatoa fedha za ujenzi huo kwa wakati ili jengo hilo likamilike kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano na Mkandarasi na kusema kuwa katika Bajeti ya mwaka huu Serikali imeweka kipaumbele katika majengo mawili likiwemo jengo hilo na lile la jengo jipya la abiria la uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume.

Nae Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kutekeleza ahadi yake pamoja na kuhakikisha Serikali anayoiongoza inaimarisha sekta ya sheria sambamba na kuzifanyia kazi changamoto kadhaa zilizokuwepo kwenye sekta hiyo.

Aliongeza kuwa Rais Dk. Shein katika uongozi wake amewacha alama kubwa kwa Mahkama, kwa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla kutokana na mambo mengi makubwa aliyoyafanya na kuahidi kua juhudi zitachukuliwa za ujenzi kuhakikisha Dk. Shein analifungua jengo hilo.

Alieleza juhudi zitakazochukuliwa katika kuhakikisha ujenzi wa skuli ya sheria unatekelezwa huku akieleza kuwa hatua ya ujenzi wa mahkama hiyo mpya inakwenda sambamba na utekelezaji wa ujenzi wa Mahkakama mpya katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Khamis Juma Maalim kwa upande wake  alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuhakikisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa asilimia mia moja ya ujenzi wa Mahkama hiyo mpya.

Waziri huyo alieleza kuwa ujenzi huo ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 huku akipongeza juhudi za Rais Dk. Shein katika kuongeza idadi ya Majaji ili kuimarisha haki na sheria kuweza kupatikana.

Mapema Mtendaji Mkuu wa Mahakama Zanzibar,Ndg.Kai Bashir Mbarouk akitoa maelezo ya kitaalamu alisema kuwa Mkataba wa ujenzi jengo hilo ulitiwa saini rasmi tarehe 21 Oktoba, 2019 baina ya Mahkama na Mjenzi ambaye ni Kampuni ya ‘Advent Construction Limited’ ya Dar es Salaam.

Alieleza kuwa Mshauri wa  Mwelekezi anayesimamia  ujenzi huo ni   kampuni  ya ‘Hab Consult’ ya Dar es Salaam ambayo pia, ndiyo iliyosanifu michoro ya jengo hilo ambapo mradi huo unaangaliwa  na Wakala wa Majengo ya Serikali pamoja na Mhandisi wa Mahakama.

Sambamba na hayo, Mradi huo unatarajiwa kugharimu jumla ya TZS Bilioni 14.3 fedha ambazo zote zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia mia moja pia, kuna Kamati Maalum ya Mradi yenye wataalamu waandamizi kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali ambapo mambo yote hayo yanafanywa ili kuhakikisha ujenzi huo unaendana na viwango na masharti yaliyokubaliwa katika Mkataba.

Mapema Rais Dk. Shein alijenga tofali katika jengo hilo ikiwa ni kiashiria cha kuweka jiwe la msingi na baadae kufungua kipazia maalum cha jiwe la msingi ambapo katika hafla hiyo viongozi mbali mbali wa Serikali, vyama vya siasa na wananchi walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mohammed Othman Chande na viongozi wengineo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.