Habari za Punde

MAKAMU WA RAIS AHUTUBIA MKUTANO WA KIMATAIFA WA UFADHILI WA MAENDELEO NCHINI HISPANIA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) unaofanyika Jijini Sevilla nchini Hispania tarehe 30 Juni 2025. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito wa kufanyika maboresho ya mfumo wa fedha na ufadhili wa maendeleo duniani ili kutoa nafuu ya riba, kuwa endelevu, unaotabirika na unaozingatia  usawa na vipaumbele vya mataifa yanayoendelea.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) unaofanyika Jijini Sevilla nchini Hispania. Amesisitiza umuhimu wa mbinu za kibunifu katika ufadhili ikiwemo kubadili madeni ya kifedha kwenda katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kama vile uhifadhi wa mazingira.

Vilevile Makamu wa Rais amesema taratibu za upimaji wa uwezo wa serikali kifedha katika ulipaji madeni unapaswa kupitiwa upya ili kuongeza uwazi na kuwa wa haki. Ameongeza kwamba Mkutano huo unapaswa kutoa ufumbuzi wa namna ya kupunguza gharama za ukopaji na kuongeza fursa za mikopo nafuu na ya muda mrefu.

Makamu wa Rais amesema kutokana na biashara kuwa nguzo ya kiuchumi ni vema mataifa kuwezeshwa katika uzalishaji na uongezawaji thamani wa bidhaa ili kufikia viwango vya kimataifa. Amesisitiza uwepo wa usawa na haki katika taratibu na sheria za kibiashara za kimataifa ikiwemo masuala ya ushuru wa forodha na ukomo wa mauzo kwa mataifa yanayoendelea.

Aidha Makamu wa Rais amesema unahitajika ushirikiano baina ya Mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea katika kuharakisha maendeleo ya sayansi, teknolojia na takwimu ili kuweza kusaidia katika utungaji sera na utekelezaji kwa kuzingatia tafiti na takwimu sahihi.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Mataifa tajiri kushirikiana na nchi zinazoendelea katika kupunguza viatarishi kwenye uwekezaji na ufadhili wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.

Kuhusu Mazingira, Makamu wa Rais ametoa wito wa kutoa kipaumbele katika ufadhili wa usimamizi na urejerezaji wa bioanuai pamoja na kuongeza wigo wa ufadhili katika miradi ya kujenga uhimilivu na miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amesisitiza umuhimu wa kuanza kazi kwa mfuko wa mazingira wa kukabiliana na hasara na uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi (Loss and Demage Fund).

Makamu wa Rais amesema kufikia mwaka 2024, Tanzania imefikia asilimia 60 ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa kupiga hatua zaidi katika lengo namba 2 hadi namba 7 hususani katika maeneo ya afya, utoshelevu wa chakula, elimu, usawa wa kijinsia, upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na upatikanaji wa nishati.

Ameongeza kwamba ili kuendeleza mafanikio hayo unahitajika ushirikiano na ufadhili wa gharama nafuu katika kuongezea mapato ya ndani ya nchi.

Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo unalenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili dunia katika kugharamia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), kujadili njia za kurekebisha mfumo wa fedha wa kimataifa ili kuwa jumuishi, wenye usawa na unaozingatia mahitaji ya nchi zinazoendelea.

Malengo mengine ya Mkutano huo ni pamoja na kupendekeza mbinu bora za kupunguza na kushughulikia mzigo wa madeni kwa nchi maskini na zenye kipato cha kati pamoja na kujenga mifumo madhubuti ya kifedha inayoweza kukabili athari za majanga ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Mkutano kuhusu Ufadhili wa Maendeleo ulianzishwa rasmi mwaka 2002 kupitia Mkutano wa kwanza uliofanyika Monterrey, Mexico na kupelekea kuundwa kwa msingi wa ushirikiano wa kimataifa katika kufadhili maendeleo. Mkutano wa Pili ulifanyika mjini Doha, Qatar mwaka 2008 ambao ulianzisha  Azimio la Doha kusisitiza haja ya kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kukabiliana na athari za mtikisiko wa kifedha duniani.

Mkutano wa Tatu ulifanyika Addis Ababa, Ethiopia, mwaka 2015, na matokeo yake yalikuwa ni Addis Ababa Action Agenda (AAAA), ambayo ilijikita katika uhamasishaji wa vyanzo vya ndani vya mapato, ushirikiano wa kimataifa, uwekezaji wa sekta binafsi, pamoja na kushughulikia changamoto za madeni na usawa wa kijinsia.

Mkutano  huu wa Nne ambao umepitisha Azimio la Sevilla unalenga kuchambua maendeleo yaliyopatikana tangu Addis Ababa na kujadili njia bora za kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu katika muktadha wa changamoto mpya kama vile mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kimataifa na athari za kiuchumi za janga la Uviko -19.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

30 Juni 2025

Sevilla - Hispania.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.