Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Akihutubia na Kuahirisha Mkutano wa Kumi na Saba wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali akiahirisha Mkutano wa Kumi na Saba wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar  hapo Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar uliojadili Miswada pamoja na Ripoti za Kamati za Kudumu za Baraza hilo.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuifanyia marekebisho Sheria ya Dawa za Kulevya kwa kuzidisha adhabu kwa waingizaji, wasafirishaji na wasambazaji wa Dawa hizo zenye madhara yanayoeleweka kwa kina na wana Jamii.
Alisema hatua mbali mbali za kupambana, kukemea pamoja na kuchukia shughuli zote zinazoshajiisha matumizi  ya Dawa za Kulevya zitapaswa kuchukuliwa kutokana na janga hili linaloikumba Dunia kwa kuathiri  nguvu kubwa ya Vijana, Wazee na Watoto wa Jinsia na Rika zote .
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiahirisha Mkutano wa Kumi na Saba wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar  uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar uliojadili Miswada pamoja na Ripoti za Kamati za Kudumu za Baraza hilo.
Alisema programu Maalum ya uchunguzi wa Makontena Bandarini pamoja na Mizigo katika Viwanja vya Ndege imeanzishwa  kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye Ibara ya 119 A – D lengo likiwa kuzuia bidhaa haramu ikiwemo Dawa za Kulevya zisiingizwe Nchini.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali Kuu kupitia Mradi wa Zanzibar Salama imeweka Vifaa vya ukaguzi {X-Ray Mashine} wa Abiria na Mizigo inayoingia na kutoka Nchini katika maeneo ya Bandari na Viwanja vya Ndege.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alibainisha kwamba Elimu inaendelea kutolewa kupitia vyombo vya Habari, Majarida na Vipeperushi juu ya athari za Dawa za Kulevya katika maeneo tofauti ikiwemo Skuli ili kuitanabahisha Jamii kutojiingiza katika janga la Dawa hizo Thakili.
“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Taasisi za Kitaifa na Kimataifa na za Kikanda kuendeleza mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya”. Alisisitiza Balozi Seif.
Amewashukuru Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Viongozi wa Taasisi za Umma na zile Binafsi kwa kutumia nafasi zao za Kidemokrasia katika kuishauri Serikali kuwajibika ipasavyo kwa Wananchi wake juu ya njia sahihi za mapambano dhidi ya janga hilo.
Akizungumzia uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae Mwaka huu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi  kujitayarisha kwa kujihakiki pamoja na kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakalomuwezesha yule aliyefikia Umri  na sifa sahihi anapiga Kura.
Balozi Seif alitoa wito kwa Wananchi Mijini na Vijijini kufuatilia kwa karibu maelekezo yote yanayotolewa na Tume zote za Uchaguzi Nchini kuhusiana na mchakato huo uliokwisha kuanza katika maeneo mbali mbali Nchini ili kutumia haki yao ya Kidemokrasia.
Alisema ni jukumu la kila Mwananchi wa Taifa hili wakati wa kipindi chote cha mchakato wa Uchaguzi kuanzia Daftari hadi Uchaguzi Mkuu kuhakikisha kwamba anasimama imara katika kudumisha hali ya Amani na utulivu ambayo ndio lulu ya Taifa hili.
Aliwakumbusha Wananchi kuendelea kupendana, kuvumiliana pamoja na kushirikiana kwa vile mshikamano na Umoja miongoni mwa Wananchi wa Imani za Dini na Itikadi tofauti ndio utakaoivusha Tanzania hii kuelekea kwenye Maendeleo ya kudumu.
Balozi Seif  aliwakumbusha Wazee kuwasihi Vijana wao kukataa kurubuniwa na Wanasiasa wachache ili washiriki katika vitendo vya uvunjifu wa Amani na kuonya kwamba  Serikali haitamvumilia Mtu au Kikundi chochote kitakachoashiria kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa Amani ya Nchi.
Kuhusu Utekelezaji wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Awamu ya Tatu sehemu ya kwanza kipidi cha Miaka Mitato ya Awali, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Jamii imekuwa shahidi kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya mpango huo.
Alisema ni vyema kwa Wananchi waendelee kushirikiana na Viongozi katika kuyatunza mafanikio hayo  hatua kwa hatua yanayotokana na Mradi huo uliojitokeza bayana  kuwa ni Mkombozi wa Wananchi Wanyonge.
Balozi Seif aliwanasihi Wananchi pamoja na Viongozi wa ngazi zote kuanzia Shehia kuendelea kujenga uaminifu, ukweli na uadilifu katika hatua zote za Mradi kuanzia ukusanyaji wa Taarifa za Walengwa watakaotimiza vigezo wapate fursa hiyo katika ngazi zao.
“ Nafuraha kueleza kwamba Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini { Tasaf 111 – 11} inayotegemewa kutekelezwa kwa Miaka Minne tayari imeshazinduliwa Rasmi na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli Mnamo Tarehe 17 Febuari 2020”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Watumishi wote watakaoshiriki katika ngazi tofauti za Mradi huo waonyeshe Uzalendo wao na Serikali kamwe haitamfumbia macho Mtumishi atakayebainika ameshiriki kwa njia yoyote katika kuchangia upotevu au ubadhirifu wa Fedha za Mradi huo.
Kuhusu utabiri wa kuwepo kwa Mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha Wiki ya Pili ya Mwezi wa Tatu ndani ya Msimu wa Masika  uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar, Balozi Seif  aliwanasihi Wananchi kuendelea kukumbushana umuhimu wa kuzitumia vizuri Mvua hizo.
Alisema licha ya Taifa kuendelea kupata mvua katika kipindi hichi kwa baadhi ya wakati lakini bado Jamii hasa Wakulima ni vyema wakazitumia Mvua hizo kwa shughuli za Maendeleo zikiwemo Kilimo cha mazao ya Chakula na Miti ya Kudumu.
Balozi Seif aliendelea kuwakumbusha Wananchi kuchukuwa tahadhari za kujiepusha na Maafa kwa kuhama mapema kwenye maeneo hatarishi, kufuatilia mienendo ya Watoto wao, kufuata maelekezo ya Wataalamu wa Mazingira, Afya na kuendelea kufuatilia Taarifa za Kitaalamu na Elimu zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepata nafasi ya kupokea, kuchangia na hatimae kupitisha Miswaada Miwili ya Sheria, Ripoti Tisa za Kamati za Wajumbe wa Baraza hilo, Taarifa ya Dawa za Kulevya pamoja na Marekebisho ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi.
Baraza la Wawakilishi lililopokea Maswahi 112 ya Wajumbe wa Baraza hilo na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa Wizara mbali mbali  limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 1 Aprili Mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.