Habari za Punde

HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI ALIYOITOA WAKATI WA KUAKHIRISHA MKUTANO WA KUMI NA SABA WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI TAREHE 26 FEBRUARI, 2020



Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote tumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehma kwa kutujaalia uhai, akatupa afya njema na akatuwezesha kufanikisha Mkutano huu wa Kumi na Saba wa Baraza la Tisa ulioanza tarehe 05 Februari, 2020 hadi leo tarehe 26 Februari, 2020 tunapouakhirisha.
Mheshimiwa Spika,
Nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa  Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa Uongozi wao mahiri na makini katika kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Serikali zetu, ikiwemo kufanya mabadiliko ya Uongozi katika ngazi mbali mbali ndani ya Chama na Serikali kwa lengo la kuendeleza ufanisi katika utendaji na usimamizi wa Demokrasia na Utawala bora.
Mheshimiwa Spika,
Vile vile, nachukua nafasi hii kukupongeza wewe binafsi Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza letu Tukufu, Naibu Spika Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma, pamoja na Wenyeviti wote wa Baraza kwa kuviendesha vyema vikao vyetu kwa hekima, busara na weledi mkubwa na kukifanya kikao hiki kumalizika kwa amani, salama na mafanikio.

Mheshimiwa Spika,
Katika Mkutano huu, Baraza lako tukufu limepokea na limejadili miswada pamoja na Ripoti za Kamati za Kudumu zifuatazo:-
  • Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya mawakili Sura ya 28 na Sheria ya wakuu wa viapo sura ya 29 na kutunga Sheria ya Mawakili na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
  • Mswada wa Sheria ya Wazee Zanzibar na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
  • Ripoti ya Kamati ya Utawala Bora na Idara Maalum ya Mwaka 2019/2020.
Ripoti ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Mwaka 2019/2020.
  • Ripoti ya Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Mwaka 2019/2020.
  • Ripoti ya Kamati Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya mwaka 2019/2020.
  • Ripoti ya Kamati Ardhi na Mawasiliano ya mwaka 2019/2020.
  • Ripoti ya Kamati ya Kuchunguza na              Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika PAC ya Mwaka 2019/2020.
  • Ripoti ya Kamati ya Bajeti ya mwaka 2019/2020.

  • Ripoti ya Kamati ya Kanuni na Sheria ndogo ndogo.
  • Marekebisho ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi.
  • Taarifa ya dawa za kulevya.
  • Taarifa ya Rushwa na Uhujumu uchumi.
  • Ripoti ya Mapendekezo ya Muelekeo wa Uchumi, Mpango wa Maendeleo na Bajeti kwa mwaka 2020/2021.
 Mheshimiwa Spika,  
Pia Baraza lako tukufu lilipokea Kauli za Serikali zifuatazo:-
  • Kauli ya Serikali kuhusu Sukari ya Kiwanda cha Sukari cha Mahonda.
  • Kauli ya Serikali kuhusu Ugonjwa wa Ngozi uliogundulikana katika Wilaya ya Micheweni.
Mheshimiwa Spika,            
Katika Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Mawakili Sura ya 28 na Sheria ya Wakuu wa Viapo sura ya 29 na kutunga Sheria ya Mawakili na mambo mengine yanayohusiana na hayo, umepelekea kuundwa kwa Sheria hii mpya itayowasaidia zaidi Mawakili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa na kupunguza changamoto zilizokuwepo hapo awali. Aidha Sheria hii itawawezesha mawakili kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini na ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Spika,
Kupitishwa kwa Mswada wa Sheria ya Wazee Zanzibar na mambo mengine yanayohusiana na hayo kutaisaidia sana Serikali kuwa na Sheria madhubuti ya kuweza kuongeza huduma stahiki kwa Wazee ambazo zitaendelea kuwapatia faraja.

Aidha Serikali inatoa shukurani kwa taasisi na watu binafsi kwa namna wanavyochangia na kutoa misaada kwa wazee hao. Vile vile tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kutekeleza majukumu ya msingi katika kuwahudumia na kuwatunza wazee ambayo ni silka na utamaduni wetu. Kila mwananchi wa Zanzibar mwenye mzee anao wajibu wa kumtunza mzee wake.
Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu pia walipata fursa ya kuchangia kwa kina Marekebisho ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi ambayo yatasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Baraza kwa kufuata na kuimarisha misingi ya Utawala Bora.

Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wajumbe pia wamepokea na wamechangia ripoti za Kamati za Kudumu za Baraza hili. Nachukua nafasi hii kuzipongeza kamati zote kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao na hatimae wakawasilisha ripoti zilizofanyiwa utafiti wa kutosha. Aidha nazipongeza Wizara na taasisi kwa mashirikiano yao na Kamati hizo. Kwa upande wa Serikali nachukua nafasi hii kuliahidi Baraza lako tukufu kwamba maoni, maelekezo na mashauri yaliyotolewa na Kamati pamoja na michango ya Waheshimiwa Wajumbe yatafanyiwa kazi na Serikali ili kuongeza ufanisi.

Mheshimiwa Spika,
Katika kikao hiki jumla ya maswali ya msingi 112 na maswali ya nyongeza ........yaliulizwa na yalijibiwa kwa ufasaha na ufafanuzi wa kina na Waheshimiwa Mawaziri. Nawapongeza wajumbe wote waliouliza maswali ambayo naamini nia yao ilikuwa kujenga hasa katika maeneo yenye mapungufu ya hapa na pale.  Nawapongeza Mawaziri kwa kuielimisha jamii kutokana na kujibu maswali hayo kwa usahihi.

Mheshimiwa Spika,
Nachukua nafasi hii kuwakumbusha wananchi wote kwamba mwaka huu wa 2020 ni mwaka wa uchaguzi mkuu katika nchi yetu. Uchaguzi wowote una matayarisho yake ikiwemo kujiandikisha kwa wapiga kura wapya na kwa wale wapiga kura wa zamani kuhakiki taarifa zao.
Naomba kuchukuwa fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar kufuata kwa karibu maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na Tume yetu ya Uchaguzi ili tuendelee kufanya uchaguzi uliokuwa huru na haki.
Aidha ni jukumu la kila mmoja wetu wakati wa kipindi chote cha uchaguzi kuhakikisha amani inadumishwa. Tuendelee kupendana, kuvumiliana na kushirikiana kwani mshikamano na umoja wetu ndio utakaoivusha nchi yetu kuelekea kwenye maendeleo endelevu. Nawataka wazee kuwasihi vijana wao kukataa kurubuniwa na baadhi ya vyama vya siasa kwa lengo la kushiriki katika vitendo vya uvunjifu wa amani. Serikali haitamvumilia mtu au kikundi cha watu kitakachoashiria vitendo vya uvunjifu wa amani. AMANI YA NCHI YETU NDIO RASILIMALI YETU.
Mheshimiwa Spika,
Natoa shukurani za dhati kwa Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako tukufu kwa kufanya marejesho ya matumizi ya Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, HONGERENI SANA. Nachukua nafasi hii kuwasisitiza Waheshimiwa Wawakilishi kuendelea kuzitumia fedha za mfuko huu kwa kufuata matakwa ya Sheria Nam. 4/2012 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo mengine ni kufuata maamuzi ya kamati husika.  Narudia tena kusema kwamba Mhe. Mwakilishi ambaye hatofanya mrejesho wa matumizi ya fedha za Jimbo hazitotolewa fedha nyengine mpaka mrejesho uwe umefanyika.
Mheshimiwa Spika,
Ninaomba niwakumbushe Waheshimiwa Wajumbe na wananchi kwa ujumla kwamba katika hotuba yangu ya kuuakhirisha Mkutano wa Kumi na Tano wa Baraza la Tisa nilielezea mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) awamu ya tatu sehemu ya kwanza kwa kipindi cha miaka mitano ya awali. Sote ni mashahidi wa mafanikio hayo, vile vile nilielezea maamuzi ya Serikali zetu mbili ya kuendeleza mradi huu ambao unajitokeza bayana kuwa ni mkombozi wa wanyonge.
Kwa furaha nachukua nafasi hii kuwaeleza Waheshimiwa Wajumbe na wananchi wote kwamba kama mlivyoona na kusikia katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, tarehe 17 Februari, 2020 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezindua rasmi Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ( TASAF III-II) unaotegemewa kutekelezwa kwa miaka minne.
Mheshimiwa Spika,
Ninawaomba viongozi na wananchi tuendelee kushirikiana katika kuyatunza mafanikio yaliyopatikana pia kuiendeleza awamu hii mpya hatua kwa hatua, na wale wote watakaotimiza vigezo wapate fursa hiyo. Aidha nawasihi wananchi na viongozi wa ngazi zote kuanzia Shehia tuwe waaminifu, wakweli na waadilifu katika hatua zote za mradi kwa kuanzia  ukusanyaji wa taarifa za walengwa katika ngazi ya Shehia.
Natoa wito kwa watumishi wote watakaoshiriki katika ngazi tofauti za mradi huo waoneshe uzalendo wao kwa lengo la kuufanikisha. Serikali haitamfumbia macho mtumishi yeyote atakayebainika ameshiriki kwa njia moja au nyengine katika kuchangia upotevu na ubadhirifu wa fedha za mradi huu.
Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu bado inaendelea kukumbwa na matukio ya udhalilishaji yakiwemo kupigwa, kubakwa kwa wanawake na watoto wadogo, kutelekezwa kwa watoto wachanga, talaka zisizofuata utaratibu, ushirikishwaji wa watoto na vijana wenye umri mdogo katika biashara zikiwemo biashara haramu za madawa ya kulevya.
Kwa mara nyengine tena nachukuwa nafasi hii kuwakumbusha wananchi wote kurudisha imani zetu kuanzia za kibinaadamu, kiutu, kijamii, kidini na kujenga umoja na mashirikiano kwa viongozi wa ngazi zote katika kupinga suala hili baya.  Aidha Serikali kupitia vyombo vyake vya dola itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za kukabiliana na janga hili.
Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu inaendelea kupata mvua katika kipindi hiki, Vile vile Mamlaka ya Hali ya Hewa imetabiri kuwepo kwa mvua kubwa katika kipindi cha Masika kuanzia wiki ya pili ya mwezi wa Machi. Nawashauri wananchi tuendelee kukumbushana umuhimu wa kuzitumia vizuri mvua hizo kwa shughuli zetu za kimaendeleo zikiwemo kilimo cha mazao ya chakula na miti ya kudumu.

Nawakumbusha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujiepusha na maafa kwa kuhama katika maeneo hatarishi, kufuatilia mienendo ya watoto wetu, kufuata maelekezo ya wataalamu wa Mazingira, wataalamu wa afya, kuendelea kufuatilia taarifa za kitaalamu na elimu zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Kanda ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Kama inavyoeleweka kwamba suala la Dawa za Kulevya ni janga kubwa duniani kote, Wazee, vijana na watoto wa jinsia na rika zote wameathirika na janga hili. Ingawaje madhara yake kwa jamii yetu tunayaelewa sote.
Kutokana na hali hiyo Serikali inaendelea kuchukuwa hatua mbali mbali za  kupambana, kukemea, kuchukia shughuli yoyote inayoshajihisha matumizi yake na   inachukua hatua kali sana kuhakikisha inatokomeza na kudhibiti uingizwaji, usambazaji na utumiaji Dawa za kulevya  nchini kama ilivyoelekezwa  Ilani ya CCM 2015 katika Ibara 119 A – D. 

Miongoni mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali yetu ni pamoja na kuandaa mazingira bora kwa kuifanyia mabadiliko Sheria ya Dawa za Kulevya kwa kuzidisha adhabu kwa waingizaji, wasafirishaji, wasambazaji wa Dawa za Kulevya. Aidha, Serikali imetoa mafunzo ya kina ya utambuzi pamoja na uchunguzi wa Dawa za Kulevya. Mafunzo haya yamelenga maeneo yote ya viwanja vya ndege pamoja na Bandari.

Pia, Program maalum ya uchunguzi wa Makontena Bandarini pamoja na mizigo (cargo) uwanja wa ndege imeanzishwa kwa lengo la kuzuia bidhaa haramu zisiingie nchini. Mafunzo haya yanaambatana na vifaa maalum vya ukaguzi wa abiria pamoja na mizigo inayoingia na kutoka nchini. Aidha Serikali kupitia Mradi wa Zanzibar Salama imeweka vifaa vya ukaguzi x-ray mashine katika maeneo ya bandari na viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, majarida na vipeperushi juu ya athari za Dawa za Kulevya katika skuli mbali mbali za Serikali na binafsi Unguja na Pemba, maeneo ya kazi, katika shehia kwa ngazi za Wilaya, pamoja  na Mabaraza ya vijana. Taaluma hiyo inawatanabahisha kutojiingiza na matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha, taaluma hiyo imeifikia jamii. Vile vile, Serikali imejenga kituo  maalum cha Tiba na Marekebisho ya Tabia kwa waathirika wa Dawa za Kulevya (Rehabilitation Center)               kilichopo Kidimini Wilaya ya Kati Unguja. Kituo hiki kitatoa huduma kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya. Aidha Serkali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania pamoja na asasi za kitaifa kimataifa na za kikanda zinazoendesha mapambano dhidi ya dawa za Kulevya.

Mheshimiwa Spika,
Tunawashukuru Waheshimiwa Wawakilishi kwa kutumia nafasi yao ya Kidemokrasia ya kuisimamia, kuishauri na kuihoji Serikali, jambo ambalo limeonesha nia thabiti mliyonayo ya kuitaka Serikali kuwajibika ipasavyo kwa wananchi wake. 

Kadhalika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kujibu maswali yote mliyoulizwa, mliweza kuyatolea ufafanuzi ambao uliwanufaisha Waheshimiwa Wajumbe pamoja na wananchi kwa ujumla. Aidha, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ufafanuzi wake alioutoa katika mambo mbali mbali yaliyohitaji ufafanuzi wa kisheria.

Mheshimiwa Spika,
Napenda kuwashukuru wale wote waliotuwezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu wa Kumi na Saba wa Baraza la Tisa la Wawakilishi kwa ufanisi.  Pongezi hizo zaidi ziwafikie Watendaji wote wa Baraza hili la Wawakilishi wakiongozwa na Katibu wa Baraza. Ni ukweli usiofichika kwamba tumeanza vizuri na ninaamini tutaendelea vizuri. 

Mungu libariki Baraza hili, Mungu ibariki Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Pia nawapongeza Wakalimani wa lugha ya alama ambao wamewawezesha wale wenye ulemavu wa  kusikia kuweza kufuatilia yote yaliyokuwa yakiendelea ndani ya Baraza hili Tukufu.  Vile vile, nawashukuru Wanahabari kwa kufanya kazi nzuri ya kuwapatia habari wananchi wetu kwa shughuli zote ambazo zilikuwa zikiendelea kufanyika.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo hayo, naomba sasa kwa heshima na taadhima kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liakhirishwe hadi siku ya Jumatano tarehe 1 Aprili, 2020, saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.