Habari za Punde

HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA MTANDAO WA VIONGOZI WANAWAKE AFRIKA TAWI LA TANZANIA KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO ST. GASPAR HOTEL - DODOMA TAREHE 26 FEBRUARI, 2020

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizindua Mtandao wa Viongozi wanawake Afrika Tawi la Tanzania katika Ukumbi wa St. Gaspar Jijini Dodoma leo Febuari 26,2020 ambapo kauli mbiu ya Mtandao huo ni Wananwake na Uongozi Twende Pamoja Wakati ni huu.

Madam Bineta Diop, Mjumbe Maalum wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika inayoshughulikia Wanawake, Amani na Usalama;

Mheshimiwa Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;

Bi. Hodan Addou, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Mwanamke (UN Women) Tanzania;

Mheshimiwa Anders Sjöberg, Balozi wa Norway nchini Tanzania;

Mheshimiwa Elisabeth Jacobsen, Balozi wa Sweden nchini Tanzania;

Bi. Raatikainen Riikka, Mkuu wa Idara ya Ushirikiano, Ubalozi wa Finland;

Bi. Norzin Grigoleit-Dagyab, Mkuu wa Idara ya Ushirikiano, Ubalozi wa Ujerumani;

Bi. Mary Rusimbi na Bi. Rebecca Gyumi, Wenyeviti wa Kamati Mkakati ya Uendeshaji wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika Tawi la Tanzania;

Wanachama wote wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika Tawi la Tanzania waliopo hapa;

Waheshimiwa Mawaziri and Manaibu Waziri mliopo;

Waheshimiwa Wabunge;

Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu;

Maofisa wa Kibalozi;

Wadau wa Maendeleo;

Wawakilishi kutoka Asasi za Kiraia;

Waandishi wa Habari;

Mabibi na Mabwana;

Habari za Asubuhi!


Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutuwezesha kukutana katika siku hii muhimu kwa wanawake na wasichana hapa Tanzania. Pili, ninayo furaha kubwa na shukrani kwa heshima mliyonipa kuwa Mgeni Rasmi katika siku ambayo, viongozi wanawake wenye uzoefu tofauti, wanawake waliofikia mafanikio makubwa, na wanawake ambao wameonesha umahiri katika maeneo mbalimbali ya uongozi, na katika kuendeleza haki za wanawake na usawa wa kijinsia, wamejumuika pamoja kwa ajili ya kujadili maendeleo ya taifa letu. 

Binafsi nafarijika sana kuwa nanyi hapa leo kwa ajili ya uzinduzi wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika, tawi la Tanzania. Tukio hili, ni kielelezo cha jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kumuwezesha mwanamke wa Kitanzania kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda wa Taifa letu. Kwa namna ya pekee naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru kamati ya maandalizi na kamati mkakati ya uendeshaji wa mtandao huu, kwa kunialika kwenye tukio hili muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Viongozi wa Mtandao,
Natambua kwamba Mtandao huu wa Viongozi Wanawake Afrika, unawezeshwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika inayoshugulikia masuala ya Wanawake, Amani na Usalama, Madam Bineta Diop, ambaye tumebahatika kuwa naye hapa leo, pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mtendaji Mkuu wa UN Women, Dk. Phumzile Mlambo-Ngcuka. Hivyo naomba kumshukuru sana Madam Diop, kwa kujumuika nasi kwa ajili ya tukio hili muhimu (Bineta We are pleased and gratified to have you here with us), lakini tunamshukuru pia kwa uongozi wake mahiri na thabiti, na kwa kushirikiana na Dkt. Phumzile katika kuhakikisha kwamba Mtandao unaunda matawi ya kitaifa. Aidha, katika jambo hili napenda pia kuzitambua na kuzishukuru kwa dhati kabisa Serikali za Finland, Sweden, na Ujerumani ambazo zimeunga mkono mpango huu hadi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ndugu Wageni Waalikwa,
Kama tulivyokwisha sikia awali, mnamo mwaka 2017, mkusanyiko wa wanawake kama sisi ulikutana jijini New York nchini Marekani, ambapo uamuzi wa kuunda mtandao wa viongozi wanawake wa Afrika ulifanyika, sambamba na uamuzi wa kuunda matawi ya kitaifa. Maamuzi hayo yaliyofanyika miaka mitatu iliyopita, yaani 2017 ndiyo yametufikisha katika tukio letu la leo la kuzindua tawi hili la taifa hapa Tanzania ambalo ni tawi la 13 la Mtandao katika Bara la Afrika.

Ndugu Viongozi,
Ni ukweli kwamba katika nchi nyingi duniani bado usawa wa kijinsia haujaweza kufikiwa katika nyanja nyingi ikiwemo uongozi. Hali hii inaigusa pia nchi yetu ya Tanzania, ingawa kwa kiasi kikubwa tunafanya vizuri tulinganishwa na nchi nyingi Barani Afrika. Kwa mfano, katika mihimili yetu mitatu ya Dola, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya uwiano wa kijinsia. Kwa upande wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kati ya wabunge 393, wabunge wanawake ni 126 ambao ni sawa na asilimia 36.7, na Baraza la Wawakilishi la   Zanzibar wanawake ni asilimia 38. Kiwango hiki ni juu ya uwiano uliowekwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) cha angalau asilimia 30. Pamoja na hayo, tulishakuwa na Maspika wa Mabunge Wanamke hapa nchini na pia katika Bunge la Afrika. Aidha tuna Manaibu Spika Wanawake katika Bunge na Baraza la Wawakilishi.

Vivyo hivyo, kwa upande wa Mahakama, idadi ya Majaji wanawake kwa Mahakama Kuu ni asilimia 30 na Mahakama ya Rufani ni asilimia 38. Aidha, katika Baraza la Mawaziri la wanawake ni asilimia 18 wakati Naibu Mawaziri ni asilimia 33.  Kubwa zaidi na la kihistoria kwa nchi yetu ni kuwa katika Serikali ya Awamu ya Tano, kwa mara ya kwanza nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Imeshikwa na Mwanamke.  Kwa ujumla, Taifa letu lina fakhari ya kuwa na viongozi wanawake na wanawake mashujaa. Historia yetu kabla na baada ya uhuru, Mapinduzi na Muungano wa Tanzania, na hata sasa, imesheheni michango ya wanawake wengi.

Ndugu Viongozi,
Kwa takwimu hizo utaona kwamba bado hatujaweza kufikia usawa wa kijinsia kwa kiwango kikubwa sana, lakini hii ni ishara kwamba uwiano wa kijinsia katika nchi yetu umefikia mahali pazuri, na kwamba, dalili za kufikia usawa wa jinsia angalau kwenye nafasi za kisiasa zinaonekana na zinatia moyo (Attemp ya Urais).  Jukumu letu ni kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika kugombea nafazi za uongozi katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa, biashara, huduma za umma au asasi za kiraia. Kwa kuwa takwimu za idadi ya watu nchini kwetu zinaonesha sisi ni wengi zaidi ya wanaume, naamini kama wanawake, tukiamua na tukishirikiana vizuri na kuaminiana basi tunaweza kupunguza wigo wa uwiano wa kijinsia kwa kiasi kikubwa.Ndugu Viongozi, Wageni Waalikwa,
Sote tunafahamu kuwa Wanawake kote ulimwenguni na hususan Barani Afrika, wanakabiliwa na changamoto nyingi, baadhi zikiwa za muda mrefu na nyingine zinaendelea kujitokeza siku baada ya siku. Hivyo, ni dhahiri kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuongeza uwiano wa usawa wa kijinsia katika ngazi za maamuzi, ili kupanua jukwaa litakaloweza kuzisemea changamoto zinazowakabili wanawake na hatimae ziweze kutambuliwa na kushughulikiwa kwa ufanisi zaidi. Ni ukweli kwamba wanawake wakiongezeka katika nafasi za uongozi, zipo faida nyingi zitakazopatikana, sio tu kwa wanawake wenyewe, lakini kwa familia, jamii, biashara binafsi, mashirika na nchi kwa ujumla.

Tafiti zimeonesha kwamba ongezeko la idadi ya viongozi wanawake wa kisiasa limesababisha kuboreshwa kwa sera, sheria pamoja na bajeti, kwa mtazamo wa kijinsia. Mfano mzuri ni majirani zetu Rwanda ambao wabunge wanawake ni asilimia 61.25 na hii imesaidia maamuzi mengi bungeni kuwa na mtazamo wa kijinsia. Hivyo, ni dhahiri kwamba uwepo wa uwiano sawa kwenye nafasi za uongozi na maamuzi katika utumishi wa umma unasaidia kuhimiza kutenga rasilimali zaidi kwa huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara, umeme na mambo yanayoleta ustawi wa jamii (Matunzo kwa makundi maalum).

Utafiti wa Shirika la Delloitte wa mwaka 2017 kwa nchi 64 duniani, Mashirika 500, umebaini kuwa ni asilimia 15 tu ya Mashirika ndio yanaongozwa na Wanawake na hiyo ni ongezeko la asilimia 3 zaidi ya mwaka 2015.

Hapa kwetu Tanzania taarifa iliyochapishwa na jalada la “Women Advancement Deeply” la tarehe 26 Juni, 2018 imeonesha kuwa Wanawake walioshika khatamu za kuongoza mashirika walikuwa ni asilimia 8 tu ambayo ilikuwa kubwa ikilinganishwa na kiwango cha Dunia kwa wakati huo, ambacho kilikuwa asilimia 3.  Bila shaka viwango hivi vitakuwa vimeongezeka tunapozungumza leo.

Kadhalika, imebainika kuwa uwepo wa wanawake zaidi katika usimamizi wa Mashirika katika sekta binafsi umethibitika kusaidia kukuza faida za biashara kutokana na ujuzi, ufanisi, uaminifu na ustadi wa kipekee walionao wanawake, na kwamba Mashirika yanayoongozwa na Wanawake yanakuwa pia na idadi kubwa ya wanawake katika kuongoza vitengo vya Mashirika hayo na vile vile yanafanikiwa zaidi.

Tafiti zinaonesha pia kwamba wasichana wanaokua wakiwaona wanawake katika uongozi, wameweza kuboresha kuongeza jitihada katika masomo yao/utendaji wao na kuinua nia yao ya kujiendeleza zaidi kitaaluma. Kwa mantiki hiyo, Mtandao huu wa Viongozi Wanawake Tanzania tuna jukumu muhimu la kuwa mfano bora ili kuwawezesha wasichana kujifunza na kuhusudu kufanya kazi kwa bidii na kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao, ili hatimaye waweze kuwa viongozi na kufika tulikofika sisi au zaidi yetu. Kwa bahati nzuri, wanawake na wanaume tunazaliwa tukiwa sawa kabisa, tofauti zetu hutokana na malezi, mazingira tunayokulia, mila na desturi zetu na matakwa ya baadhi ya jamii zetu. Hivyo basi, Ili kuhakikisha usawa wa kijinsia katika kazi na uongozi, hatuna budi kusimamia ipasavyo makuzi ya watoto wetu ili usawa wanaozaliwa nao uendelee mpaka kwenye ngazi za uongozi. Jambo hili linawezekana endapo tutapambana na changamoto za mila na desturi potofu, lakini pia, kwa kutoa kipaumbele sawa cha elimu kwa watoto wa kike na kiume.

Ndugu Viongozi, Wageni Waalikwa,
Serikali yetu imeridhia mikataba ya kimataifa na kikanda inayo kuza haki za wanawake na usawa wa kijinsia. Aidha, lengo la 6 la agenda ya Afrika - 2063 (Afrika Tunayoitaka) linaitaka Afrika inayothamini watu wake, yenye usawa wa kijinsia, na ambapo wanawake wanawezeshwa kusimama katika nafasi zao kwenye nyanja zote za maisha. Vivyo hivyo, lengo namba 5.5 ya Ajenda ya Maendeleo Endelevu – 2030, linadhibitisha umuhimu wa wanawake kuwa na fursa sawa za uongozi katika ngazi zote za kufanya maamuzi, ikiwa ni pamoja na uongozi wa kisiasa, kiuchumi au uongozi wa umma.

Kwa kuwa asilimia 50 ya watu wa Tanzania ni wanawake, tunahitaji tuwe na uwiano sawa wa ushiriki katika kufanya maamuzi ambayo yanahusu maisha ya Watanzania, kike kwa kiume. ili tufanikiwe kuwa na ushiriki wa uwiano, hatuna budi kukabiliana na changamoto zilizotukabili, kama vile; umasikini, mfumo dume katika Maisha ya jamii, kwenye uongozi wa asasi mbalimbali, ujuzi dhaifu, wanawake kutokujiamini na ukatili/unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto. Hizi ni changamoto ambazo Serikali ya Tanzania inajitahidi kukabiliana nazo kwa mbinu mbalimbali na kwa kushirikiana na wadau wengine. Ni imani yangu kwamba mtandao huu, utashirikiana ili kuimarisha na kuhamasisha juhudi za kitaifa kukabiliana na changamoto hizo.

Ndugu Viongozi, Wageni Waalikwa,
Nimefarijika kuona kwamba Mtandao huu wa Wanawake Tanzania unaanza kwa kuainisha maeneo sita ya kipaumbele. Maeneo hayo ni uongozi wa wanawake na utawala; amani na usalama wa wanawake; wanawake vijijini; uhamasishaji wa jamii; viongozi wanawake vijana; pamoja na uwezeshaji wanawake kiuchumi. Maeneo haya yana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu. Kwa mfano, suala la uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Hii ni katika   kuhakikisha kwamba wanawake katika Halmashauri zote nchini wanatengewa asilimia 4 ya fedha za ndani za halmashauri kwa ajili ya mikopo itakayowasaidia kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Vile vile, kwamba wanawake wana haki sawa za umiliki wa ardhi na mali, na kwamba wanawake kila mahali waweze kufikiwa na huduma wanazozihitaji. Na ukimwezesha mwanamke kiuchumi ataboresha maisha yake katika ngazi tofauti ikiwemo maslahi yake, uwezo wake wa kufanya maamuzi na pia kupunguza matukio ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana. Ndugu Viongozi, Wageni Waalikwa,

Kama mnavyofahamu, tarehe 8 Machi, tutasherehekea siku ya kimataifa ya wanawake kwa Kaulimbiu isemayo " Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya Sasa na Baadae." Hivyo, uzinduzi huu umekuja kwa wakati mzuri sana kuelekea kwenye utekelezaji wa kauli mbiu hiyo, Nimefurahi kusikia kwamba mtandao huu unakusudia kuwafikia na kuwashirikisha wanawake wa umri tofauti, wenye uzoefu mbalimbali, kutoka vijijini hadi mijini, katika sekta mbalimbali.

Dhana hii ya “Kizazi cha Usawa” imetoka kwenye Kampeni ya Kimataifa ya UN Women kwa ajili ya kusherehekea miaka 25 tangu kufanyika kwa Mkutano wa Wanawake jijini Beijing. Kampeni hii inasisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vizazi vipya vya wanawake na wanaume katika kufikia usawa wa kijinsia.

Kauli mbiu hiyo inajinasibisha pia na malengo yaliyowekwa katika Ajenda 2063 (Afrika Tunayoitaka) na Malengo ya Maendeleo Endelevu, 2030 (SDGs).  Ili kufikia malengo hayo, ni lazima tuwahusishe na kushirikisha vijana. Mtandao huu wa viongozi wanawake unaweza kutimiza jukumu muhimu katika kuhakikisha kuwa kuna mafunzo endelevu ya pamoja kuhusu  mahusiano ya kijinsia kati ya Vijana wa kike na wa kiume. Ni muhimu tutumie nafasi zetu za ushawishi ili kuwezesha kizazi kijacho kiishi na Imani kwamba Binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahiki heshima.  (Katiba za Nchi)

Ndugu Wanachama wa Mtandao wa Viongozi Wanawake wa Afrika hapa Tanzania,
Nataka kuwathibitishia na kuwatia moyo kuwa mnachokifanya leo ni kitu cha kujivunia sana. Natambua kwamba kufikia hapa haikuwa kazi rahisi, na kuchaguliwa kwenu kuwa sehemu ya mtandao huu ni ushahidi wa mafanikio ya kila mmoja wenu katika safari za kuchangia ujenzi wa Taifa hili.  Hongereni sana!

Aidha, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu naomba kuwapongeza kwa mara nyingine UN Women, Umoja wa Afrika na Kamati ya Mkakati ya Uendeshaji wa Mtandao wa Wanawake Viongozi Tanzania kwa kazi kubwa mliyoifanya kufanikisha uzinduzi huu kwa kiwango cha kuridhisha. Mimi binafsi na kwa niaba ya Serikali inayoongozwa na jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba niwahakikishie kuwa tutawaunga mkono na tuko tayari kushirikiana nanyi katika shughuli zenu.

Ndugu zangu, Naomba mniruhusu nitumie fursa ya kuonana nanyi tukumbushane kwamba, sisi ni wanawake, Maisha yetu yamezungukwa na mambo mengi Mwana, Mke, Mama na Kiongozi, ukweli ni kwamba hatuwezi kufanya yote wenyewe (Building Carrier and Parenting) (Don’t die with guilty apply coping mechanisms) Hatuwezi kufanya haki na kuwajibika ipasavyo (Mfano Wanu) kwa kila anaetutegemea. Wanaoathirika zaidi ni waume zetu, kuweni wapole na wavumilivu, tuwahakikishie tu kwamba kwenye orodha ya watu tunaowajali na wao wamo. Nayasema haya si kwasababu mimi ni Mmahiri sana, ila waswahili wanasema “Hakuna Kungwi mchafu”

Kwa upande wa kazi zetu, ili tusimame vyema kwenye nafasi zetu inabidi tuwe na:

Umahiri- kujua kwa ustadi mkubwa eneo unalolisimamia (Jiongezee ujuzi wa Kazi yako),

Ushupavu na Kujiamini – Ongea kutokana na unalolijua na unaloliamini (Usibabaishwe),

Mawasiliano mema – Uwe na Uratibu na uhusiano wa kilichoko akilini/Moyoni na kinachotoka mdomoni. Ongea kwa murua ili ueleweke.

Uaminifu na Uadilifu – Kuelekea kwenye ukweli na uhakika ambao umeshaufanyia kazi na unaufahamu vilivyo.

Wito wangu kwenu, kama Wanawake na viongozi katika maeneo yenu ni kutumia mambo haya matano niliyoyaeleza pamoja na yale mnayoyajua, kuwasemea, kuwatetea na kuwaunganisha wanawake wote wa Tanzania bila kujali itikadi zao. Tumieni Mtandao huu kama chombo cha kuwawezesha wanawake wengi zaidi vijijini na mijini kuwa viongozi bora. Niwakumbushe tu kuwa nanyi mnatazamwa na wanawake na wasichana wengine kama mfano katika uongozi. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba hata wanaume waliokuja kutuunga mkono hapa leo nao wanatutazama na kuhoji iwapo tunaishi na yale tunayoyadai na kuyapigania. Hivyo, hatuna budi kuongoza kwa mfano ili Mtandao huu uzidi kuheshimika na kutambulika kwa wanawake wengi zaidi.

Mwisho kabisa, napenda tena kuishukuru Kamati ya Maandalizi ya shughuli hii kwa kunipa heshima ya kuzindua mtandao huu, na kunipa fursa ya kuwapongeza Wanawake wa Tanzania kwa kufanikiwa kuanzisha Mtandao huu.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa
 MTANDAO WA VIONGOZI WANAWAKE AFRIKA TAWI LA TANZANIA UMEZINDULIWA RASMI.

MUNGU WABARIKI WANAWAKE WA TANZANIA
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.