Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Aendelea na Ziara Yake Wilaya ya Kahama.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake wakikagua maendeleo ya Ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Kisasa wa Chinjio la Nyama katika eneo na Ndembezi nje kidogo ya Mji wa Shinyanga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga Mjini Nd. Geofrey Ramadhan akitoa Taarifa fupi juu ya Ujenzi wa Chinjio la Wanyama Ndembezi Mkoani Shinyanga.
Daktari wa Mifugo Manispaa ya Shinyanga Mjini Dr. Tito Gagize akielezea jinsi uzalishaji wa Nyama za Mbuzi na Ng’ombe ndani ya Chinjio la Ndembezi utakavyokuwa.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Wafanyabiashara wenye Uwezo Nchini wameshajiishwa kuchangamkia fursa ya Uwekezaji wa Kiwanda cha Ngozi kinachofikiriwa kujengwa katika Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga ili kwenda sambamba na uwepo wa Kiwanda cha Machinjio kinachotarajiwa kuanza kazi baadae Mwaka huu.
Shajiisho hilo limetolewa na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokagua Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa ya Ndembezi nje kidogo ya Shinyanga Mjini akiwa katika ziara ya Siku Tano Mkoani huo.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM anayesimamia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Ndani ya Mkoa wa Shinyanga alisema yeye kwa upande wake amekubali kubeba jukumu la kuungana na Viongozi wengine kutafuta Wawekezaji watakaoweza kuitumia fursa hiyo muhimu.
Alisema Mkoa wa Shinyanga Kimazingira umebarikiwa kuwa na Mifugo mingi ya Wanyama wanaoweza kuwa Rasilmali muhimu katika Uwekezaji wa Viwanda vyote viwili kutokana na upatikanaji wa Nyama kutokana na Ng’ombe na Mbuzi  na hatimae kuzalisha Ngozi.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Shinganga inayoungwa mkono na Serikali Kuu kwa kuanzisha Mradi huo muhimu wa Machinjio ya Kisasa ya Kimataifa uliozingatia Rasilmali kubwa za Mifugo inayopatikana ndani ya Mkoa huo.
Alisema Wafanyabiashara Wadogo wa Vitongoji vya Mji wa Shinyanga kupitia Mradi huo watapata fursa ya kuendeleza Miradi ya ujasiri Amali kupitia bidhaa zitakazozalishwa na Kiwanda hicho na kuwatoa hofu Wananchi  wa Imani Tofauti za Dini kuondoa wasi wasi kutokana na Nyama itakayozalishwa kuzingatia matakwa ya Dini katika Uchinjaji wa Wanyama wanaopelekwa hapo.
“ Wafanyabiashara Wadogo Wadogo wanaojishughulisha na kazi za Ujasiri Amali watapata  bidhaa zinazozalishwa katika Kiwanda hicho cha Machinjio kwa kuendesha  Biashara zao kama Supu na Mishkaki”. Alisisitiza Balozi Seif.
Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga halkadhalika aliwaomba Wafanyabiashara wa kati na Wafugaji wanaohitaji kuchinja Mifugo yao kuitumia Machinjio hiyo kwa kupeleka Mifugo yao kwa vile taratibu zitakazotumika katika Sehemu hizo ikiwemo masuala ya Afya zitakuwa salama.
Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa Mradi huo Mkubwa wa Machinjio Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga Mjini Nd. Geofrey Ramadhan alisema Mradi huo uliopata Ufadhili wa Benki ya Dunia wa zaidi ya Shilingi Bilioni  3.8 ulianza Mwaka 2013.
Nd. Ramadhan alisema hatua za Ujenzi zinaendelea kwa maeneo ya Mabwawa, Uzio, sehemu za Vipoza Baridi, Mabwawa ya Maji machafu pamoja na sehemu maalum za Mapumziko ya Wanyama kabla ya kuingizwa maeneo Maalum ya Uchinjwaji.
Alisema chinjio hilo la Kisasa litakalokuwa na uwezo wa kuchinja Ng’ombe100 hadi 500 na Mbuzi 150 kwa Siku kutegemea Mahitaji halisi ya Matumizi ya Nyama hizo litagharimu Gharama ya Jumla Shilingi Bilioni Tano Nukta Saba hadi kukamilika kwa kila hitaji.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Rajab Telak alisema Mradi huu umebuniwa na Serikali kutokana na Fursa kubwa iliyopo ndani ya Mkoa huo ya Rasilmali ya Mifugo ambayo inaweza kutoa ajira na kupunguza ukali wa Maisha ya Wananchi wa kipato cha kawaida.
Mh. Zainab alieleza kwamba Masoko ya Shinyanga yamekuwa yakishuhudiwa yakizalisha Nyama za Ng’ombe na Mbuzi huku ngozi zitokanazo na Nyama hizo huzagaa ovyo bila ya kutengewa utaratibu Maalum kutokana na ukosefu wa Kiwanda kinachoweza kuratibu biadhaa hiyo.
Aliwatahadharia Wahandisi wa Mradi huo kuhakikisha kwamba Kazi waliyopewa wanaikamilisha kwa mujibu wa Mikataba iliyowekwa, vyenginevyo atalazimika kuchukuwa hatua zitakazostahiki kutokana na Mikataba hiyo.
Alisema Serikali ya Mkoa haitaridhia kuona Mradi huo unachelewa ambao kwa mujibu wa Ujenzi Wahandisi wamechelewa kukamilisha kutokana na sababu mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.