Habari za Punde

NCHI WANACHAMA WA SADC KUIMARISHA SERA NA KUJENGA MIKAKATI YA PAMOJA YA KUKUZA AJIRA KWA VIJANA

Naibu Katibu Mtendaji mwenye dhamana ya Utangamano wa Kikanda, Dkt. Thembinkosi Mhlongo (wa pili kutoka kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano (Kulia) ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe. Kushoto ni Mwakilishi wa Sekretarieti ya SADC, Bw. Maxwell Parakokwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kijamii na Rasilimali Watu SADC Bi. Duduzile Simelane.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuelekea Mkutano wa Mawaziri wa SADC sekta ya Kazi na Ajira.
Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bw. Ally Msaki akielezea jambo kuhusu masula ya ajira wakati wa Mkutano huo. Kushoto ni Kamishna wa Kazi - Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Francis Mbindi.
Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano huo wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika Mkutano huo wa Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira. 
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Machi 2, 2020 Jijini Dar es Salaam.
Na; Mwandishi Wetu
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimejizatiti kuimarisha Sera na kujenga mipango ya pamoja itakayowezesha kukuza ajira kwa vijana katika Ukanda huo.
Akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa Jumuiya hiyo wanaosimamia Sekta ya Kazi na Ajira hii leo Machi 2, 2020 Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe alisema kuwa Mkutano huo umewakutanisha Wataalamu wa sekta ya Kazi na Ajira kwa lengo la kuandaa nyaraka mbalimbali zitakazo jadiliwa katika Mkutano wa Mawaziri ambao utafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 5 hadi 6 Machi, 2020 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Alieleza kuwa ajenda zitakazo jadiliwa ni pamoja na masuala ya kisera kuhusu ukuzaji wa ajira kwa vijana, pia masuala yanayohusisha uhamaji wa nguvu kazi ndani ya jumuiya ya SADC ambapo itasaidia pia kutoa fursa ya kukuza ajira kwa nguvukazi ya nchi wanachama.
“Itambulike kuwa uimarishwaji wa sera katika sekta ya kazi na ajira utasaidia kwa kasi kikubwa kuwa chachu ya maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa afrika endapo itasimamiwa vizuri,” Alisema Massawe
Aliongeza kuwa kauli mbiu ya Mkutano huo isemayo “Kukuza Soko la Ajira na Mahusiano Mema Sehemu za Kazi kwa Maendeleo Endelevu” inaelezea umuhimu wa sekta ya kazi na ajira katika kuongeza tija ya ukuaji wa soko la ajira kwa nchi wanachama.
Naye Naibu Katibu Mtendaji mwenye dhamana ya Utangamano wa Kikanda, Dkt. Thembinkosi Mhlongo alieleza kuwa mapendekezo yaliyotolewa katika mkutano uliofanyika mwezi Novemba 20, 2019 ulioshirikisha wataalamu na wadau wa utatu umechangia katika kujenga miongozo sahihi na sera zitakazo wawezesha nchi wanachama wa SADC kukuza sekta ya kazi na ajira.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bw. Ally Msaki alisema kuwa Mkutano wa Mawaziri utakao funguliwa rasmi tarehe 5 Machi, 2020 utawawezesha Mawaziri wa Nchi wanachama wa SADC kujadili kwa pamoja ajenda mbalimbali zitakazokuwa zimepitiwa kwenye kikao cha wataalam kwa lengo la kuimarisha sekta ya kazi na ajira nchini na jumuiya hiyo kwa ujumla.
Hadi sasa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zilizoshiriki katika Mkutano huo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Namibia, Eswatini, Lesotho, Jamhuri ya Shelisheli na Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.