Habari za Punde

THBUB yatembelea wagonjwa hospitali ya rufaa Dodoma


Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Enid Chiwanga (kushoto) akiongea na ujumbe wa THBUB (mbele yake) uliotembelea Hospitali ya rufaa  jijini Dodoma 
Kamishna wa THBUB, Dkt. Fatma Khalfan (kulia) na Kamishna Amina Talib Ali (kushoto) wakitoa mkono wa pole kwa mmoja wa wazazi waliojifungua katika Hospitali ya rufaa  jijini Dodoma walipotembelea kuwaona wagonjwa 
Ujumbe wa THBUB ukiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Enid Chiwanga (katikati) huku wakionyesha ishara ya “mwanamke hodari”muda mfupi mara baada ya ujumbe wa THBUB kumaliza ziara yake katika hospitali hiyo.

Na Mbaraka Kambona,
Katika kuelekea kilele cha kuadhimisha siku ya wanawake duniani, ujumbe wa wanawake kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) umetembelea Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi iliyopo katika  Hospitali ya rufaa  jijini Dodoma mapema leo Machi 6, 2020.

Ujumbe huo  uliotembelea  hospitali hiyo uliongozwa na Makamishna wawili, Dkt. Fatma Khalfan na Amina Talib Ali kwa lengo la kuwafariji wakina mama wagonjwa na wazazi waliolazwa katika hospitali hiyo.

Kamishna wa THBUB, Dkt. Fatma Khalfan akiongea wakati wa kukabidhi bidhaa mbalimbali walizopeleka kwa ajili ya wagonjwa alisema kuwa lengo la ziara yao ni kwenda kuwafariji wagonjwa kina mama katika hospitali hiyo kwa kuzingatia  wiki hii ni ya kuadhimisha siku ya mwanamke duniani.

Dkt. Fatma alisema kuwa Afya ni muhimu sana kwa mwanadamu na kwamba jamii haitaweza kujenga uchumi wake kama watu wake hawana afya nzuri.

Aliongeza kwa kusema kuwa kwa niaba ya uongozi wa THBUB wanaipongeza serikali kwa jitihada zake za makusudi katika kuboresha sekta ya afya nchini hususani matibabu mazuri kwa kina mama na watoto.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imeendelea kutekeleza utoaji wa haki ya afya kwa vitendo kwa kuendelea kuboresha na kujenga miundo mbinu mbalimbali ya zahanati na vituo vya afya ikiwemo kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa nchini.

Aidha, Dkt. Fatma alisema kuwa pamoja na jitihada kubwa za serikali katika kuboresha sekta ya afya bado kuna changamoto ambazo zinaikabili sekta hiyo na hivyo kutoa wito kwa wadau kushirikiana pamoja na serikali  katika kutatua changamoto hizo.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Enid Chiwanga wakati akiupokea ujumbe huo alitoa shukrani kwa uongozi wa THBUB kwa uamuzi wao wa kutembelea wagonjwa katika hospitali hiyo na kusema kuwa wamefarijika kwani ziara hiyo itatoa tumaini jipya kwa wagonjwa waliopo katika hospitali hiyo.

Kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani mwaka huu ni Machi 8, 2020 na kwa mwaka huu maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kumbukizi ya miaka 25 tangu wanawake wakutane katika mkutano wa Beijing nchini China mwaka 1995.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.