Habari za Punde

Zanzibar COVID-19 Update. Wagonjwa wengine wawili wakutwa na Virusi vya Corona


Na Ramadhani Ali – Maelezo    
  
Zanzibar imefikisha jumla ya wagonjwa tisa walioambukizwa virusi vya Covid - 19 hadi kufikia leo tarehe 10 Aprili na wanaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha Kidimni na afya zao zinaendelea kukimarika.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakili, Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed amesema sampuli zilizopelekwa kwa ajili ya uchunguzi jana watu wawili wamegundulika kuwa na ugonjwa wa Korona.

Alieleza kuwa mgonjwa wa kwanza ni Mtanzania ana umri wa miaka 33 mkaazi wa Mwanakwerekwe aliripotiwa tarehe 7 mwezi huu akisumbuliwa na homa kali, mafua na kifua na baada ya kuchukuliwa kipimo alionekana ameambukizwa.

Alisema mgonjwa mwengine pia ni mtanzania mwenye umri wa miaka 24 mkaazi wa Mtendeni Zanzibar aliripotiwa akiwa na mafua na kikohozi na alichukuliwa sampuli ambayo imeonyesha kuwa ameambukizwa.

Waziri Hamad Rashid alieleza kuwa wagonjwa wote wawili hawana historia ya kusafiri nje ya nchi kwa siku za hivi karibuni.

Aliweka wazi kuwa Wizara inaendelea kuwafuatilia watu wa karibu waliowahi kukutana na wagonjwa hao ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi mapya.

Alisema hadi kufikia jana mchana jumla ya watu 86 waliokutana na wagonjwa wanafuatiliwa kwa karibu na kuna watu 252 waliorudi kutoka nje ya Tanzania wamewekwa Karantini Unguja na Pemba.

Waziri wa Afya amewaomba wananchi kuchukua tahadhari zote na kuzingatia maelekezo ya Serikali na weataalamu wa afya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa COVID – 19 kwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji ya kutiririka na sabuni, kuepuka mikusanyiko na kubaki majumbani kwa wale ambao hawana ulazima wa kutoka.

Amesema Corona imeingia hatua ya pili nchini baada ya kumaliza hatua ya kwanza ya kuingizwa na watu kutoka nje, sasa maradhi yameingia ndani ya jamii na udhibiti wake ni mgumu hivyo kila mtu anatakiwa kuchukua tahadhari kubwa zaidi kuliko kusubiri yatuathiri kwa kiwango kikubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.