Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya
Bw.Richard Mganga.
Na
Shamimu Nyaki - WHUSM
Serikali imetoa takriban Milioni 150 kukarabati miundombinu
ya viwanja vya michezo pamoja na ujenzi wa kisima cha maji katika Chuo cha
Maendeleo ya Michezo Malya ambacho ndio chuo pekee nchini kinachozalisha walimu
wa sekta hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mkuu wa Chuo
hicho Bw.Richard Mganga amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano cha
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli chuo kilipatiwa
fedha hizo kwa ajili ya kukarabati viwanja vinavyotumika chuoni hapo lengo
ikiwa ni kukuza na kuendeleza Michezo nchini.
“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa
kutupatia kiasi hicho cha pesa ambacho kimetusaidia kukarabati viwanja vya
michezo vikiwemo vya mpira wa pete, mpira wa wavu, mpira wa kikapu na mpira wa
mikono ambavyo vinasaidia kufundisha walimu wetu”,alisema Bw. Mganga.
Bw. Mganga ameongeza kuwa katika bajeti ya mwaka
2020/2021 chuo hicho kimetengewa takriban Milioni 300 kwa ajili ya kujenga
madarasa matatu na hosteli moja ambazo
zitasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi katika chuo hicho.
Kwa upande wake mwalimu wa Chuo hicho Bw. Somo Ahmed
Kimwaga amesema kuwa chuo hicho kinatoa mafunzo ya michezo kwa ngazi ya Cheti
na Diploma katika fani ya Uongozi wa Michezo na Ualimu wa Uongozi katika Michezo
kwa Waalimu kutoka halmashauri zote nchini.
Ameongeza kuwa chuo hicho kimezalisha wataalamu
wengi katika michezo akiwemo Bw. Robert Chitanda anayefundisha timu ya polisi
Morogoro ambaye pia ni Mwalimu Msaidizi katika timu ya Taifa pamoja na
Bw.Alfred Selengia ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania
(TAVA).
Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kipo katika
Wilaya ya Kwimba Jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment