Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Shein Azma ya SMZ Kuaza Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Binguni Mkoa wa Kusini Unguja .


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein. akimsikiliza Eng.Ramadhan China akitowa maelezo ya ramani ya  michoro ya majengo ya Hospital ya Kisasa Binguni Mkoa wa Kusini Wilaya ya Kati Unguja alipofanya ziara kutembelea eneo hilo. 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanza ujenzi wa hospitali ya rufaa na kufundishia huko Binguni, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja hivi karibuni.

Dk.  Shein amesema hayo leo wakati alipofanya ziara ya kulitembelea eneo linalokusudiwa kujenga hospitali hiyo huko Binguni na kupata maelezo kutoka kwa wataalamu na uongozi wa Wizara ya Afya.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali iko tayari kuanza kwa ujenzi huo baada kukamilika mipango yake ya muda mrefu,  hivyo tayari imeamua ujenzi huo kuanza hivi karibuni.

Rais Dk. Shein alisema ujenzi huo utafanywa na Kampuni Ujenzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kupitia fedha za mkopo ambapo kwa kuanzia matayarisho yake yatafanywa kwa fedha za Serikali.

Alieleza kuwa maandalizi yako tayari na ndio maana viongozi wote wa Baraza la Mapinduzi wakiwemo Mawaziri na Manaibu Mawaziri wakaamua leo kwenda katika eneo hilo na kupata maelezo juu ya ujenzi huo.

Viongozi hao waliongozwa na Rais Dk. Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Baada ya kuangalia eneo hilo na kupata maelezo Rais na ujumbe wake wa Baraza la Mapinduzi pamoja na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walitembelea eneo linalokusudiwa kujengwa jengo la Uchunguzi wa Virusi vya maradhi makuu lililopo ndani ya Taasisi ya Afya hapo Binguni.

Akiwa katika jengo hilo, Rais Dk. Shein alipata maelezo na taarifa ya maandalizi ya ujenzi huo kutoka kwa wataalamu na Viongozi wa Wizara ya Afya.

Dk. Shein alisema Serikali imeamua ujenzi huo kuanza baada ya hatua za maandalizi kukamilika ikiwemo upatikanaji wa fedha, michoro na ramani na hivyo akaitaka timu ya wataalamu kukaa pamoja ili kuwa na sauti moja katika utekelezaji wa kazi hiyo na kupata ufanisi.

Alisema dhamira ya Serikali ya kujikita katika kufanya uchunguzi wa maradhi mbalimbali ipo pale pale, kwa kigezo kuwa hakuna tiba muafaka bila kufanyika uchunguzi.

Aidha alisema, juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa Corona zimepata mafanikio, tofauti na ilivyotarajiwa wakati ugonjwa huo ulivyoingia nchini na kubainisha dhamira ya Serikali zakutokuficha takwimu za wagonjwa wanaopata maradhi hayo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kupokea ushauri wowote unaolenga kuunga mkono juhudi zake katika kukabiliana na ugonjwa huu, kwa misingi kuwa wale wanaotoa ushari wafuate taratibu na miongozo iliyowekwa.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa si busara viongozi wakaanza kushindana kwa masuala ya maradhi na kueleza kuwa yeye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, hivyo hana haja ya kushindana na wale wanaopita kueneza maneno yasio na msingi juu ya maradhi ya Corona.

Alieleza haja kwa viongozi wanaohusika kukaa pamoja na kuzungumza pamoja kwa azma ya kukubaliana na mambo ya msingi

Aidha, Dk. Shein alisema ujio wa mashine ya uchunguzi wa Covid 19 utasaidia sana juhudi za serikali kuukabili ugonjwa huo na kubainisha kuwa mashine hiyo inaweza kuwekwa mahala popote itakapoonekana inafaa.

AbdiShamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822  E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.