Na Shamimu Nyaki –
WHUSM 06/05/2020- Dodoma
Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaratibu ujenzi wa Sanamu ya Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere katika viwanja vya
jengo la Amani na Ulinzi la Julius Nyerere lililopo katika Makao Makuu ya Umoja
wa Afrika (AU) Jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Akizungumza wakati wa
uwasilishaji wa Hutoba ya Makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2020/2021 Bungeni
Jijini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe amesema kuwa ujenzi wa sanamu hiyo ni utekelezaji wa Azimio la
Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) uliofanyika Jijini Harare, Zimbabwe mwaka 2015.
“Ujenzi wa Sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere
katika Umoja wa Afrika (AU) ni makubaliano ya mkutano wa wakuu wa nchi wa SADC
ambao walikuabaliana kuwa ujenzi huo lengo lake ni kutambua na kuenzi mchango
wa waanzilishi wa SADC katika kulikomboa Bara la Afrika” alisema Dkt.
Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe
ameongeza kuwa ujenzi wa Sanamu hiyo utatumia malighafi ya Shaba nyeusi (bronze
statue) ambapo ameeleza kuwa Kamati ya Kitaifa ya Uratibu na Kamati ya Ujenzi
wa Sanamu za Kuwaenzi Waasisi wa Taifa kama inavyotakiwa katika sheria ya
Kuwaenzi Waasisi wa Taifa ya mwaka 2004 zimeshaundwa na kuanza kazi tangu 2018.
Kwa upande wake
Meneja Mradi wa mradi huo Dkt. Emmanuel Ishengoma ambaye pia ni Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya
Sanaa katika Wizara ya Habari, Utaaduni, Sanaa na Michezo amesema kuwa hatua za
awali za ujenzi wa Sanamu hiyo tayari zimeanza na mradi unatekelezwa na Kampuni
ya SAMCRO ya nchini Afrika Kusini chini ya usimamizi wa SADC na Tanzania na
utagharimu takriban Dola za Marekani 267,992.60 ambazo ni sawa na takriban
Shilingi 615,000,000 ambazo zitatolewa na SADC na gharama za usimamizi kutolewa
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Ishengoma
ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu ambapo
Sehemu kubwa ya kazi hiyo itafanyika nchini Afrika Kusini na ikiishakamilika na
kuridhiwa na Tanzania pamoja na SADC itasafirishwa na kusimikwa katika Makao
Makuu ya AU huko Addis Ababa Ethiopia.
Ujenzi wa Sanamu hiyo
umetokana na wazo alilolitoa Rais wa zamani wa Zimbabwe Hayati Robert Mugabe
katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kuhusu mkakati wa
kuwaenzi viongozi waanzilishi wa SADC ambao walishiriki katika kulikomboa Bara
la Afrika.
No comments:
Post a Comment