Habari za Punde

TAMWA yahamasisha wanawake kuchukua fomu za uongozi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wanawake chukuweni fomu za Kugombea Uongozi - TAMWA Wakati vyama vya siasa vikifungua milango kukaribisha wananchama wa vyama vyao kuchukua fomu za kugombea katika nafasi tano za uongozi Tanzania,ikiwemo ya Urais wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania, Zanzibar, Ubunge,
Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Udiwani; Chama cha Waandishi wa Habari  cha wanawake (TAMWA Zanzibar) kinawashauri wanawake wa vyama vyote kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo.

Zanzibar kama sehemu ya Jamuhuri ya Muungano Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa Sensa ya idadi ya watu na makaazi ya mwaka 2012 Zanzibar ina idadi ya watu wapatao 1,303,569 na kukisiwa kufikia 1,671,598 kwa mwaka 2020 ambapo wanawake ni zaidi ya asilimia 50.

Hata hivyo uwingi huo wa wanawake hauendani na nafasi zao katika vyombo vya kutunga sheria na kufanya maamuzi na wakati mwingi wanawake hao huvunjwa moyo na kupikiwa majungu kwa makusudi wakati wa kugombea nafasi hizo ili hali hiyo isibadilike.

Kutokana na mazingira hayo, ni wastani wa wanawake 200 tu ndio walioteuliwa na vyama vyao kwa Zanzibar kugombea katika maeneo hayo matano ya uchaguzi ya mwaka 2015 ambapo kwa nafasi ya Uraisi iliendelea kutokuwa na mwanamke tokea kurejea kwa vyama vingi. 

Hivyo, tunawaomba wanawake wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba na pia kuwaongoza wananchi katika nafasi mbali mbali sambamba na wenzao wanaume.

Imekuwa ni kawaida, wanawake kuelekezwa kugombea katika viti maalum tu ambavyo kijinsia huwa havioneshi usawa wa kijinsia na umoja wa wanawake bali huchangia kwa kiasi kikubwa kuleta mgawanyiko wa wanawake.

Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015 ni wanawake watatu tu ndio walioweza kuchaguliwa kupitia kwenye majimbo katika nafasi za ubunge sawa na asilimia 6, wawakilishi saba sawa na asilimia 14, madiwani 23 sawa na asilimia 20 na nafasi ya Uraisi ambayo ni moja tu imeendelea kushikiliwa na mwanamme.

TAMWA Zanzibar pia ingependa kuishauri jamii kuwaunga mkono wagombea wanawake ili waweze kuonesha uwezo wao na hivyo kuleta uwiano katika jamii pamoja na maendeleo kwa ujumla.

Tunapenda pia kuisisitiza Tume ya Uchaguzi (ZEC) kuweka mfumo maalum wa kupokea maoni kutoka kwa wananchi hasa wanawake wanaokumbwa na udhalilishaji katika kipindi hichi cha heka heka za uchaguzi.

Dkt. Mzuri Issa
Mkurugenzi,
TAMWA, ZNZ

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.