Habari za Punde

CCM JIMBO LA HANDENI MJINI WAPONGEZANA, KIGODA ASHINDWA KUTETEA JIMBO

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.
MWENYEKITI wa CCM wilayani Handeni Athumani Malunda amepongezwa kwa kumudu kusimamia na kumaliza bila shaka kikao cha uchaguzi wa kura za maoni za kuwania nafasi ya Ubunge katika jimbo la Handeni mjini.

Akizungumza baada ya kutangaza matokeo ya wagombea hao Katibu wa CCM wilayani humo Salehe Kikweo alisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa wazi na haki na kila Mgombea pamoja na wajumbe waliopiga kura wameridhishwa na matokeo yaliyotokea.

Kikweo alibainisha kwamba kulikuwa na jumla ya watia nia 41 waliochukua fomu na kurudisha na wajumbe waliopiga kura walikuwa 521 huku kura moja ikiharibika na 500 kupigwa za ndio 

"Nimpongeze mwenyekiti wetu kwa kusimamia zoezi hili vizuri, na sasa natangaza matokeo lakini ikumbukwe kwamba hapa ni maoni tu ya wajumbe wa kamati, bado mchakato huu utaendele ngazi ya Taifa na huko tutampata Mgombea wetu atakaye kwenda kutupeperushia bendera yetu ya chama cha mapinduzi katika uchaguzi mkuu hapo Octoba" alisema Kikweo.

Wakizungumza na Nipashe baadhi ya wajumbe waliopiga kura walielezea kuwa uchaguzi wa kura za maoni kulikuwa wa huru na haki ambapo kila mmoja alishuhudia kura hizo zikihesabiwa hadharani jambo ambalo walisema wanamshukuru Rais Magufuli kwa kazi anazotekeleza kwani hilo ni moja ya utekelezaji wake.

"Kitendo cha kura kuhesabiwa huku kila mmoja anaona kimeamsha hisia za wananchi wengi ambao awali hawakuwa na imani na matokeo ya kura hizi, hii ni moja ya utekelezaji wa rais wetu, tunamshukuru na kumpongeza pia, Mungu aendelee kumuongsoza katika imani aliyonayo" alisema mjumbe mmoja.

Sambamba na hilo wajumbe hao walitoa pongezi kwa viongozi wa chama kwa kushikilia misimamo yao katika kuongoza uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na kuwapongeza waliokuwa watia nia kwa umoja na upendo waliouonyesha kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi huo.

Aidha baadhi ya wagombea wa kiti hicho walidai kwamba wameridhishwa na matokeo hayo na kama kuna mwenye tofauti atakuwa hana imani na chama chake huku wakieleza kwamba matokeo hayo ni ya kura za maoni na kwamba wanasubiria maamuzi ya mwisho ya nani awe kutoka ngazi ya Taifa.

Baada ya kura hizo kupigwa na matokeo kutoka aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Omary Kigoda alishika nafasi ya nne kwa kupata kura 58 wakati Reuben Kwagirwa akiibuka kidedea kwa kura 132 na Hafidh Kabanda akipata kura 92, huku Marian Mwanilwa akipata kura 75 na Abdi Kipacha akipata kura 42 na John Kida akiambulia kura 18.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.