Habari za Punde

Wananchi kisiwani Pemba wajitokeza kuchukua vitambulisho vyao


BAKAR MUSSA –PEMBA.

WANANCHI wa mikoa miwili ya Pemba, wamejitokeza katika vituo mbali mbali walivyojiandikisha kuchukuwa vitambulisho vya kupigia kura ili kujiweka tayari kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo baadae.

Akizungumza na Waandishi wa habari huko katika kituo cha uchukuaji wa vitambulisho hivyo katika  Skuli ya Chanjamjawiri , Makamo mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Zanzibar, Mabrouk  Jabu Makame, alisema zoezi liko vizuri watu wamejitokeza kwa utulivu mkubwa huku kukiwa na utaratibu mzuri ambao kila mmoja anaweza kupata kitambulisho bila ya usumbufu.

Alieleza kuwa Vitambulisho hivyo vimeanza kutolewa na Tume hiyo kupitia vituo mbali mbali ili kupunguza msongomano watu kwani kwa yule ambae hatopata ndani ya Vituo vyao atapatiwa katika vituo vya Tume ya Uchaguzi zilizoko kila Wilaya .

Makamo mwenyekiti huyo, aliwataka watendaji kuwa na uharaka pale mwananchi anapoingia katika chumba cha kuchukulia kitambulisho ili waepukane kutopoteza muda mwingi .

“ Tume inawashukuru Wananchi wa Pemba, kwa kujitokeza kwa wingi katika vituo hivyo kwa ajili ya kuchakuwa vitambulisho vyao na kuweka utaratibu mzuri wa foleni zinazowafanya wapate haki yao hiyo kwa urahisi zaidi,”alisema.

Mussa Kombo Mussa mkaazi wa Matale Chake Chake Pemba, alisema wameweka utaratibu mzuri wa kupeena namba kwa kila anaefika ili kuwafanya wananchi wasipate tabu na hilo limewafanya wapate vitambulisho vyao kwa muda mfupi tokea kuingia kituoni.

Aliwataka Wananchi wenzake kujitokeza kwa wingi kuchukuwa vitambulisho vyao na wavione kuwa hiyo ni mali yao ambayo itawafanya waweze kupiga kura kwa kumchagua kiongozi wanaemtaka kwa maslahi ya nchi yao.

“ Huwezi kupiga kura kama huna Kitambulisho cha kupigia kura , nawasihi Wananchi wenzangu tujitokeze kuvichukuwa ili tusije tukalalamika baadae,”alisema.

Nae bibi Ramla Abas Siwatu , mkaazi wa Matale alisema utaratibu unaotumika katika kuchukuwa vitambulisho ni mzuri kwani ni muda mdogo tu wakuingia chumbani na kupatiwa kitambulisho chako.

“ Mimi na wenzangu tumekuja mapema tokea saa  12 za asubuhi , ingawaje tulikuwa tunajuwa vituo vitafunguliwa saa 2 , hii ili tupa imani kuwa tupate mapema lakini tunashukuru baada ya kufunguliwa tu , tulipata bila ya usumbufu,”alieleza.

Hanifa Juma Khamis  wa kituo cha Skuli ya Chanjamjawiri , alieleza kuwa wanashukuru kuwa vitambulisho wanapatiwa bila ya usumbufu ingawaje watu ni wengi waliojitokeza katika siku hiyo ya kwanza kufuata haki yao hiyo .

Aliwataka wananchi wenzake kuacha dharau wajitokeze kuchukuwa vitambulisho hivyo kwani ndio silaha pekee ya kuwapeleka katika kuchaguwa Viongozi wanaowapenda.

Zainabu Moh’d Karenga, kituo cha Wawi Chake Chake Pemba, amesema wanashukuru utaratibu unaotumika kwa kuchukuwa vitambulisho vya mpiga kura ni mzuri kiasi ambacho wanapoingia vituoni tu wanapatiwa haki hiyo bila ya usumbufu wowote.

Nae Nassor Iddi Suleyum wa kituo cha Vikunguni,alieleza kufurahishwa kwake na utaratibu unaotumiwa na Tume ya Uchaguzi ya ZEC juu ya kuwapatia vitambulisho vya mpiga kura na kuwataka wananchi ambao hawajajitokeza kufanya hivyo ili kujiweka tayari na Uchaguzi.

Zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya kupigia kura limeanza tarehe 18 na linatarajiwa  kumalizika tarehe 19/7 mwaka huu  kwa Pemba na wale ambao watakosa kuvipata vituoni humo wanatakiwa kuvifuata katika Ofisi za Uchaguzi  Tume ya Uchaguzi za kila Wilaya.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.