Habari za Punde

Wanawake Wajasiriamali Msingi wa Uchumi wa Viwanda- DKT. JINGU

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiangalia bidhaa  za wajasirimali wa Baraza la Biashara la Wanawake Tanzania (TWCC) katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar Es Salaam.
Wajasiriamali wa kikundi cha cha Jiko Matawi wakimkabidhi zawadi ya Jiko Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu alipotembelea Banda la  Baraza la Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC)katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar Es Slaam.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewataka Wanawake wajasiriamali nchini kuchangamkia fursa na kuanzisha viwanda vidogo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kutekeleza Uchumi wa Viwanda.

Katibu Mkuu Jingu ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipotembelea mabanda ya wanawake wajasiriamali katika Maonesho ya 44 ya kimataifa ya Biashara maarufu kama SabaSaba.

Amesema kuwa hivi sasa kuna mwamko mkubwa kwa wanawake wafanyabiashara wadogo kuanzisha viwanda ikiwa njia mojawapo ya kujikwamua kiuchumi.

Dkt. Jingu amesema falsafa ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli imetekelezeka kwa vitendo na kusababisha mageuzi makubwa yaliyoiwezesha Tanzania kufikia Uchumi wa Kati mwaka 2020 badala ya lengo lililowekwa la mwaka 2025.

"Niseme tu, wanawake wamekuwa na mchango mkubwa kuchochea maendeleo hadi hapa tulipofika. Kundi hili ni muhimu sana katika kuendeleza na kukuza uchumi wa  taifa" alisema 

Dkt. Jingu amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019 Serikali kupitia utaratibu wa Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya makundi maalum, imewezesha utoaji wa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 39.7 kwa wanawake wajasiriamali zaidi ya Laki 8 na elfu 70.

Ameongeza kuwa Katika kuhakikisha Serikali inawawezesha  wanawake,  katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2020 zaidi ya Shilingi Bilioni 5.6  zimewanufaisha wanawake wajasiriamali zaidi ya elfu 17 kupitia dirisha maalum la Benki ya Posta Tanzania (TPB)

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Biashara la Wanawake Tanzania (Tanzania Women Chamber’s of Commerce) Jacquiline Maleko amesema Serikali kwa kushirikiana na TWCC imewafikia wanawake wengi kuwaunganisha na masoko ya bidhaa zao pamoja na kuwawezesha kupata vibali mbalimbali

"Humu tunao wafanyabiashara wazuri sana wenye viwango na hata wanauza bidhaa zao katika nchi za Ulaya na Marekani ni hatua kubwa sana” alifafanua.

Mmoja wa wajasiriamali kutoka Kikundi cha, Matawi Jiko Fausta Ntara ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha wajasiriamali hasa wanawake kupata mitaji na  masoko ambavyo vimewasaidia kujikwamua kiuchumi.

"Tunafuraha sana kwakuwa tumekuwa katika moja ya watu muhimu katika kulifikisha taifa letu katika uchumi wa kati" alisema

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.