Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akimtambulisha na kumkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM Mgombea Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya CCM Mhe. Dk. Hussein Mwinyi, wakati wa hafla ya Mkutano wa Uzinduzi wa Kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi ambaye pia ni Makamo
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali
Mohamed Shein amewataka wanaCCM pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kumchagua
Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar kwani ana sifa zote wa
Urais.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika mkutano wa
uzinduzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika katika viwanja
vya Kibandamaiti maarufu viwanja vya Demokrasia ambavyo vipo Jijini Zanzibar
ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi na
kuhudhuriwa na mamia ya wanaCCM waliofurika katika viwanja hivyo.
Katika maelezo yake, Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM
Zanzibar alisema kuwa CCM imemchagua Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea nafasi ya
Urais kutokana na sifa zote za kuwa Rais hasa ikizingatiwa kuwa yeye si
mwanagenzi wa siasa kwani amewahi kuwa kiongozi katika nyadhifa mbali mbali ndani
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa kutokana na uwezo alionao Dk. Hussein
Mwinyi anauwezo mkubwa wa kuipaisha Zanzibar na kuleta maendeleo hasa pale
akiendelea kushirikiana na mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.
John Pombe Magufuli pamoja na Mgombea wake Mwenza Mama Samia Suluhu Hassan na
wagombea wengine wote wa chama hicho katika nafasi mbali mbali.
Rais Dk. Shein alieleza sifa mbali mbali za Dk.
Hussein Mwinyi ikiwa ni pamoja na kuwa muungwana, mwenye heshima kwa wakubwa na
wadogo, asiye na mbwembwe za uongozi na pia ni Daktari aliyebobea katika fani
yake.
Aidha, alieleza kuwa Dk. Hussein ni mgombea nafasi
ya Urais pekee ambaye atayalinda Mapinduzi ya Januari 12, 1964 pamoja na
kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umeleta mafanikio makubwa
nchini.
Makamo Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo
kumuombea kura Dk. Hussein Mwinyi pamoja na
wagombea wengine wote wa CCM huku akitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea
Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa CCM wa Mkoa wa Mjini Kichama pamoja na
kuwakabidhi Ilani ya chama hicho ili waende wakainadi.
Rais Dk. Shein alisema kuwa mikutano ya Kampeni ya
Chama hicho itaendelea katika maeneo mengine mbali mbali katika Mikoa, Wilaya
ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuelekea Kisiwani Pemba.
Nae Mgombea Nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi
ya CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi alieleza mafanikio yaliopatikana katika
utekeleza wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 chini ya uongozi wa Rais Dk.
Shein na kuaahidi atayaendeleza katika Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025
aliyokabidhiwa.
Hivyo, Dk. Hussein alieleza haja kwa wanaCCM na
wananchi kukichagua chama hicho ili kuendeleza mafanikio hayo huku akieleza
azma yake ya kuyaendeleza Mapinduzi pamoja na kuutunza na kuulinda Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
Aidha, alieleza azma yake pamoja na vipaumbele
vyake iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuiimarisha
sekta ya uchumi wa bahari (bule economy), hasa uvuvi wa bahari kuu kwa lengo la
kuinua ajira kwa vijana sambamba na kuimarisha pato la Taifa.
Pamoja na hayo, Dk. Hussein aliyaeleza mambo
mengine atakayoyapa kipaumbele ikiwa ni pamoja na kuiimarisha sekta ya utalii,
sekta ya uvuvi, viwanda ufugaji wa samaki, kuwasaidia wavuvi, kuimarisha sekta
ya kilimo na sekta nyenginezo.
Dk. Hussein pia, alieleza kuwa atahakikisha katika
kuendelea zoezi la upatikanaji wa mafuta na gesi atahakikisha mikataba
itakayofungwa inawanufaisha wananchi wa Zanzibar sambamba na kuhakikisha
Wazanzibari wanapata fursa kubwa ya ajira katika sekta hiyo.
Alieleza kuwa katika kuhakikisha uchumi unaimarika
ni lazima miundombinu ya barabara, bandari na uwanja wa ndege yote hiyo
inaimarisha pamoja na kuhakikisha vinapatikana vyanzo vipya vya umeme kazi
ambayo ataiendeleza kwa lengo la kukuza uchumi na maendeleo ya Zanzibar.
Sambamba na hayo alieleza azma yake ya kuimarisha
huduma za jamii zikiwemo elimu bora bila ya malipo hadi Sekondari, kuongeza
ufaulu kwa wanafunzi na kupitia upya mitaala ya elimu ikiwemo elimu ya ufundi
ili vijana waweze kujiajiri wenyewe, kuongeza udahili, fedha kwa wanafunzi
vyuoni huduma za afya kuanzia msingi hadi Rufaa, kukuza bajeti ya afya, maji
safi na salama.
Sekta ya kilimo, kikiwemo kilimo cha biashara na
chakula vyote ataviimarisha sambamba na
kuviendeleza na kuanzisha viwanda vikiwemo vya kusindika.
Pia, alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa
kusimamia amani na utulivu huku akiahidi na yeye kwa upande wake iwapo atachaguliwa kuwa
Rais wa Zanzibar ataiendeleza kwani anatambua umuhimu wake kwa maendeleo ya
jamii na taifa kwa jumla.
Dk. Hussein aligusia suala zima la utawala bora
katika kukuza uchumi na kusisitiza suala zima la uwajibikaji na kueleza kuwa
hatowavumilia wale wote waliokuwa hawawajibiki na kuhakikisha kwamba watu hawatofanya
kazi kwa mazoea.
Mapema Naibu Katibu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma
Mabodi alieleza kuwa Dk. Hussein Mwinyi ana uwezo mkubwa wa kuuinua na
kuuendeleza uchumi wa Zanzibar.
Aidha, alieleza kuwa uwezo alionao Dk. Hussein
Mwinyi katika kusimamia amani na utulivu pamoja na Muungano ni mkubwa sana hasa
ikizingatia historia yake ya uongozi wake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mkutano huo ulikwenda sambamba na burudani kutoka
kwa wasanii mbali mbali wa ndani ya nje ya Zanzibar wakiongozwa na msanii nguli
Bongo Flava Ali Kiba pamoja na mwana dada anaeinukia katika miondoko hiyo Zuhura
Othman Soud (Zuchu) wakiungana na wasanii wa Bongo Movie na makundi mengine
kadhaa ya wasanii.
Viongozi mbali mbali wa CCM walihudhuria akiwemo
Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muunganow a Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan,
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi
wengine wastaafu akiawemo Rais Mstaafu Ali Hassan Mwiny, Rais Mstaafu wa
Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, Makamo wa Rais Mstaafu Dk. Mohamed Kharib
Bilali na viongozi wengine wa CCM kutoka Tanzania Bara.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment