Habari za Punde

DK.MWINYI AWAPA MATUMAINI WAKULIMA KARAFUU PEMBA

NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.

NGOMBEA wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaahidi wakulima wa zao karafuu kisiwani Pemba kuwa, pindi akipata ridhaa kushika nafasi hiyo, atahakikisha zao hilo linaongezeka thamani ili kuwanufaisha wakulima na kuongeza pato la taifa.

Alisema ataweka miundombinu bora ikiwemo kujenga viwanda vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hili hapa nchini badala ya kuiuza nchi za nje pekee.

Alisema zao hilo endapo litawekewa mazingira bora wananchi watapata fedha nyingi na serikali itakuwa na pato ambalo litasaidia kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo sekta ya Afya,elimu,kilimo,uvuvi,maji safi na salama na miundombinu ya barabara na umeme.

Hayo aliyasema wakati akizungumza na  wakulima wa zao  karafuu, chumvi na viungo kwenye ukumbi wa hoteli ya Wesha nje kidogo ya mji wa Chake chake kisiwani Pemba, alisema nia hiyo anayo kwa dhati.

Katika maelezo yake mgombea huyo pia alisema kuwa atapambana na baadhi ya watendaji wa Shirika la Biashara Zanzibar wanaotuhumiwa kuwapunja wakulima pindi wanapopima karafuu zao katika mzani wanapewa fedha ndogo kuliko karafuu wanazopima.

 Alisema haridhishwi kuona wakulima hao ambao wanapata usumbufu wa kulishughulikia zao la taifa, na kisha kujitokeza watendaji wanaolipwa na serikali, kuwaibia kwa makusudi wakulima wakati wanapoliuza  zao hilo kwa kisingizo cha mizani.

Alisema alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo, ili kuwatumikia wananchi wote wakiwemo wakulima hao, ili wafaidike na jasho lao.

Alisema, kwa vile ana nia ya kuimarisha uwajibikaji, ndio maana kama watendaji hao hawataki kubadilika, atawawajibisha kisheria.

Kuhusu mikopo kwa walima wa zao hilo, ya kuishughulikia mashamba yao, aliwahidi kuwa hilo linawezekana na akiamini kuwa, linaweza kuongeza tani za uvunaji wa zao la karafuu.

“Nalo jambo la kuwapatia mikopo ya kuyashughulikia mashamba yenu ni jema, maana naamini hilo linaweza kuongeza tani za mwaka 2015 zilizokuwa 3,321 na mwaka 2018 kuwa tani 8, 277 na kufikia tani nyingi zaidi,’’alieleza.

Kuhusu wakulima wa viungo na wale wazalishaji wa chumvi kisiwani Pemba, amewahidi kuwapatia mitaji na mikipo yenye masharti nafuu.

Alisema haiwezekani mkulima wa iliki, chumvia au vanilla kutakiwa kupeleka waraka wa nyumba kama ithibati ya kupewa mkopo.

“Mkinichagua kuwa rais wa Zanzibar, nitazungumza na mabenki kuona wanapunguza masharti ya mikopo au wakati mwengine serikali kuwa ndio dhamana, ili nao wapate kujiendeleza,’’alifafanua.

Alisema, jengine analotarajia kulifanya pindi akiwa rais wa Zanzbar, ni kuhakikisha anaweka mazingira imara zaidi kwa wakulima hao, ikiwa ni pamoja na kuangalia upya suala bei, ili iendelee kuwanufaisha wakulima hao.

Alisema hadi mwaka 2018 kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 iliyosimamiwa na rais wa awamu ya saba, Dk. Ali Mohamed Shein, kulikuwa kunazalishwa tani 8,277 ambapo kama akipata ridhaa atahakikisha kuna ongezeko la uzalishaji hadi kufikia tani 10,000 kwa mwaka.

Mgombea huyo alieleza kuwa, serikali ya awamu ya nane ijayo, atakayongoza, itaendelea kuimarisha hali za kipato cha wakulima wa zao la karafuu ni kuanza kuchakata mafuta ya majani ya mkarafuu.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdulla Juma Mabodi, alisema Dk. Hussein ni mchapakazi hodori na ndio maana, kwa nafasi yake ya Waziri wa Ulinzi bado nchi iko salama.

Alisema ana sifa zote za kuwa rais wa Zanzibar, na hasa kwa vile amekuwa akiyapenda makundi kama ya wakulima wa zao la karafuu, mwani, viungo na hata wanaozalisha chumvi.

“Kura zenu ni muhimu sana ili Dk. Hussein Mwinyi aingie madarakani na kuona anaondoa changamoto zenu, katika sekta ambazo mmeamua kujiajiri,’’alifafanua.

Dk.Mabodi, alisema mgombea huyo wa kiti cha urais wa Zanzibar ni mbunifu na mwadilifu anayependa kusimamia haki na fursa za wananchi anaowaongoza.

“Mgombea wetu amehudumu wizara ya ulinzi kwa zaidi ya miaka 11 hivyo mkimpa ridhaa ya kuwa rais basin chi yetu itaendelea kuwa na amani ya kudumu kwani ana uzoefu mkubwa katika  masuala ya ulinzi na usalama wan chi”,alisema mabodi.

Awali akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake wa karafuu, Sharif Maalim, alisema wakati umefika kwa wakulima kushajihishwa ili waweza kuzalisha miche kwa wingi kwa kutumia vilatu vyao.

Alisema jengine ambalo ni changamoto ni kutolewa mikopo wakati wa uvunaji pekee, jambo ambalo linahitajika mikopo kwa ajili ya kuyashughulikia mashamba.

“Na hiyo mikopo ilinyotolewa ina urasimu mkubwa, jambo ambalo haliwasaidia sana wakulima wetu, kwani wakati mwengine huchelewa sana hadi kumfikia,”alieleza.

Aidha mkulima huyo wa karafuu, alisema serikali ijayo lazima iangalie upya suala la kikosi kazi cha kudhibiti magendo ya karafuu, na badala yake fedha hizo, zihamishiwe kwa wakulima ili kuondoa changamoto zao.

“Sisi wakulima sasa tumeshamua kuziuza karafuu zetu ZSCT, kwa vile serikali iliongeza bei, lakini kuna tatizo la kupunjwa kutokana na kuwepo kwa mezani, ambazo zimeshapitwa na muda,’’alieleza.

Kwa upande wake mwakilishi wa wazalishaji chumvi kisiwani Pemba, Mohamed Salum Juma, alisema wanahitaji mitaji zaidi ili kuongeza pato katika sekta hivyo.

Alisema, wamekuwa wakiteswa na ukosefu wa vifaa kama vile pauro, majembe, mabero na vipimia joto, jambo ambalo hujikuta na pato dogo na kuelewa na kazi ngumu.

‘’Lakini hata suala la soko ni changamoto kubwa, maana hivi sasa wapo wakulima wanapaekti hadi 500 za chumvi hawajui wapi wauze, kwani sisi ni tofauti na wazalishaji wa karafuu,’’alifafanua.

Mkulima wa viungo Abdull-karim Hafid Said, alisema changamoto kubwa ni ukosefu wa vitendea kazi, kama vile mashine ya kusukumia umwagiliaji, mbegu na pembejeo kwenye sekta yao.

Alisema, wamekuwa wakikumbana na masharti kama vile ya kuwa na waraka wa nyumba au mali kubwa, ili upatiwe mikopo, jambo ambalo hushindwa kufikia malengo yao.

Pamoja na hayo mabwana mashamba na mabibi mashamba wametakiwa kwenda mashambani kutoa taaluma ya masuala mbalimbali ya kilimo na sio kubaki maofisini huku wakulima wakibaki bila taaluma ya kutosha.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.